Friday, September 29, 2017

Serikali Kuzichukulia Hatua Taasisi Zilizokiuka Taratibu za Manunuzi 2016/2017

 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi  ya  Umma (PPRA) Balozi Dkt. Matern Lumbanga (kushoto) akiongea wakati wakimkabidhi Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango Ripoti ya Tathmini ya Utendaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 Leo Mjini Dodoma,  Kulia ni Mjumbe wa Bodi hiyo Prof. Sufian Bukurura.
 Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi  ya  Umma (PPRA) Balozi Dkt. Matern Lumbanga wakati wa makabidhiano ya Ripoti ya Tathmini ya Utendaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 Leo Mjini Dodoma.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi  ya  Umma (PPRA) Balozi Dkt. Matern Lumbanga akimkabidhi Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango Ripoti ya Tathmini ya Utendaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 Leo Mjini Dodoma.
 Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akikata utembe baada ya kupokea Ripoti ya Tathmini ya Utendaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 Leo Mjini Dodoma, Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi  ya  Umma (PPRA) Balozi Dkt. Matern Lumbanga.
 Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akionesha kwa wanahabari na wajumbe wengine wa Bodi(hawapo pichani) kitabu cha Ripoti ya Tathmini ya Utendaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 Leo Mjini Dodoma, , Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi  ya  Umma (PPRA) Balozi Dkt. Matern Lumbanga. 
 Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akiongea na wajumbe wa Bodi ya ya Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi  ya  Umma (PPRA) baada ya kupokea Ripoti ya Tathmini ya Utendaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 Leo Mjini Dodoma ambapo ameahidi kuzichukulia hatua taasisi zote zilizokiuka taratibu za manunuzi zilizoainishwa kwenye Ripoti ya Tathmini ya Utendaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
 Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi  ya  Umma (PPRA) Dkt. Laurent Shirima akiongea, wakati wakimkabidhi Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango Ripoti ya Tathmini ya Utendaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 Leo Mjini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya ya Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi  ya  Umma (PPRA).PICHA NA IDARA YA HABARI-MAELEZO.


Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma

Serikali imesema itazichukulia hatua Taasisi zote zilizokiuka sheria na kanuni za manunuzi ya Umma pamoja na zile zenye viashiria vya rushwa ambazo zimebainika katika ripoti ya tathmini ya utendaji iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa mwaka wa Fedha 2016/17.

Hayo yamesemwa leo Mjini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango alipokuwa akipokea ripoti ya tathimini ya utendaji wa Taasisi za Serikali katika sekta ya Manunuzi iliyofanywa na PPRA kwa mwaka wa Fedha 2016/17.

“Tutazichukulia hatua na kuziwajibisha taasisi zote ambazo zimebainika katika ripoti hii kuwa na viashiria vya rushwa au kufanya malipo yenye utata katika manunuzi yao,” alisema Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango amesema kuwa, zaidi ya 70% ya fedha za Umma zinatumika kununua vifaa na huduma mbalimbali hivyo Serikali haitavumilia kuona fedha hizo zinatumika bila kufuata sheria na kanuni zilizowekwa.

Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa PPRA Balozi Dkt. Matern Lumbanga amezitaja taasisi ambazo zimekiuka sheria na taratibu za manunuzi kwa mwaka 2016/2017 kuwa ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Taasisi ya Mifupa (MOI) pamoja na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Taasisi nyingine ni Shirika la Bima la Taifa (NIC), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mamlaka ya Anga (TCAA), Wizara ya Fedha na Mipango na Halmashauri ya Wilaya Kondoa. 

Balozi Lumbanga amesema kuwa uchunguzi wa zabuni mbili zenye thamani ya shilingi bilioni 160.5 ambazo zilikuwa zinatekelezwa na Wizara ya Fedha na Mipango pamoja TCAA haukubainika mapungufu ya msingi na PPRA ilipendekeza utekelezaji wa miradi hiyo uendelee kama ilivyopangwa.

“Uchunguzi uliofanywa katika taasisi sita zilizobaki ulibaini kuwa Serikali ilipata hasara ya takribani shilingi milioni 12.15 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo, ucheleweshaji wa malipo kwa wakandarasi uliosababisha ongezeko la riba pamoja na faini zilizotokana na ukiukwaji wa taratibu za kijamii na mazingira kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa kazi za ujenzi,” alisema Balozi Lumbanga.

Balozi Lumbanga amezitaja Taasisi zilizobainika na malipo yenye utata kuwa ni Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na Halmashauri ya Kwimba. Ukaguzi wa kupima upatikanaji wa thamani ya fedha ulibaini malipo yenye utata katika taasisi hizo tatu ambazo ni kiasi cha shilingi milioni 483.44 zililipwa kwa wakandarasi kwa kazi ambazo hazikuwa zimefanyika.

Vile vile amesema kuwa, miradi 33 katika taasisi 17 ilibainika kuwa na kiwango kikubwa cha viashiria vya rushwa. Taasisi hizo ni Mamlaka za Maji Safi na Maji Taka za Moshi (Muwasa), Mwanza (Mwauwasa) na Arusha (Auwasa) pamoja na Halmashauri ya Wilaya za Wilaya za Msalala, Kibondo na Moshi.

Taasisi byingine ni Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Chuo cha Ufundi Arusha, Halmashauri ya Mjia wa Kahama, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Halmashauri ya Mji wa MAsasi pamoja na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

Ripoti hiyo ni ripoti ya 11 kuwasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango tangu PPRA ilipoanzishwa.

No comments: