Sunday, September 10, 2017

MWANRI ATOA MWEZI MMOJA KWA WAMILIKI WA KIWANDA CHA MANOGA KUHAKIKISHA KINAANZA KAZI.

Baadhi ya mitambo ya Kiwanda cha Pamba cha Manonga wilayani Igunga ambayo ilikuwa ikutumika kuchambua Pamba na kuzalisha mafuta yake ambayo hafanyi kazi kwa kipindi kirefu baada ya wamiliki wake kusimamisha uzalishaji. Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri( hayupo katika picha) jana ametoa mwezi mmoja mitambo hiyo ianze kufanya kazi.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri (aliye mbele) akiangalia mmoja wa mitambo baaya kutembelea Kiwanda cha Pamba cha Manonga jana wilayani Igunga kwa ajili ya kujionea hali halisi kilivyo hivi na mahitaji yake ili kianze upya uzalishaji.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri (kulia) akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU) Robert Mayongela Jongera (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Igunga John Mwaipopo (kulia) baada viongozi mbalimbali kutembelea Kiwanda cha Pamba cha Manonga jana wilayani Igunga kwa ajili ya kujionea hali halisi kilivyo hivi na mahitaji yake ili kianze upya uzalishaji.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri (kulia) akiwasisitiza wamiliki wa Kiwanda cha Pamba cha Manonga kilichopo wilayani Igunga kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja mitambo ya kiwanda hicho iwe imeshaanza kazi. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Igunga John Mwaipopo. Mkuu wa Mkoa alitoa maelezo hayo jana alikwenda kutafuta sababu za kwanini hakiendelei na uzalishaji kwa zaidi ya miaka 20.

Na Tiganya Vincent-RS-Tabora.

SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imetoa mwezi mmoja kwa wamiliki wa Kiwanda cha Pamba cha Manonga kuhakikisha wamekikarabati ili kiweze kuanza tena uzalishaji wa mafuta ya pamba na uchambuzi wa Pamba na kutengeneza ajira kwa vijana mkoani hapo.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri jana wilayani Igunga wakati alipokwenda kujionea hali halisi ya kiwanda hicho ambacho kwa maika zaidi ya 20 hakifanyi kazi.

Alisema kuwa baada mwezi mmoja huo kukamilika atafanya ziara Kiwandani hapo ili kuhakikisha kama ukarabati umeshakamilika na mitambo imeshaanza kufanya kazi na kinyume cha hapo atalazimika kumwandikia Waziri wenye dhamana na viwanda ili wamiliki wake wanyang’anye kwa ajili ya kumpa mwekezaji mwingine.

Mwanri aliwaagiza Wamiliki wa Kiwanda hicho ambao ni Rajani pamoja na Chama Kikuu cha Ushirika cha Igembensabo kupanga ratiba ya mpango kazi wa utekelezaji shughuli zitakazoonyesha mipango ya ufufuaji na muda wa ukamilishaji kwa ajili kufanikisha zoezi hilo ndani ya muda ulipangwa , vinginevyo watashindwa.

“Tengenezeni ratiba itakayowasaidia katika upangaji wa mambo yenu,Mfano siku fulani mnakwenda TANESCO kwa ajili ya kuomba umeme three phase ili kuachana na ule single phase ambao mnasemaje hauwezi kuwasaidia katika uendeshaji wa kiwanda chenu…kisha mnapanga siku ya kufuatilia upatikanaji wa maji kiwandani mtaona mambo yanakwenda mbamumbamu na ukarabati ukamika kwa wakati” alisisitiza Mwanri.

“Nataka nikirudi hapa nikute mitambo inaunguruma…vingine nitamwita Mheshimiwa Mwijage aje hapa kuchukua kiwanda hiki…sitaki mambo yafike huko fanye kazi ili kiwanda kianze uzalishaji na vijana wetu wapate ajira” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Mmoja wa Wabia katika Umikili wa Kiwanda cha Pamba cha Manonga Urveshi Rajani alisema kuwa watahakikisha kuwa ndani ya mwezi mmoja Kiwanda hicho kinakuwa tayari kwa ajili ya uzalishaji wa mafuta ya pamba na uchambaji wa zao hilo.

Alitoa wito kwa viongozi kuhakikisha wanahamasisha wakulima kulima pamba kwa wingi ili Kiwanda cha kiwe na malighafi za kosha kwa ajili ya uzalishaji wa mafuta na uchambuzi wa zao hilo.

Naye Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU) Jospeh Mihangwa alisema kuwa mitambo ya Kiwanda cha Pamba cha Mananga ni mizuri na inasaidia kuchamba pamba bila kukatakata na hivyo kuwa na soko kubwa duniani.

Alisema kuwa kwa sababu ya ubora wa kiwanda hicho wao kama majirani na Mkoa wa Tabora wako tayari kushirikiana na wamiliki wake kama watahitaji msaada wa mafundi wa kusaidia kukarabati mitambo ili kianze tena uzalishaji kwa sababu kiwanda hicho ni muhimu sana katika uchambuzi wa pamba.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kiwanda hiki ni kizuri sana kina mitambo ya Platt Lumus ambacho wakati wa uchambuaji wa pamba haikati nyuzi na kufanya pamba inachambua hapa iwe na bei kubwa katika soko la dunia…sisi kama watahiji msaada wa mafundi wa kusaidia kufufua tuko tayari kuwasaidia” alisema Meneja huyo Mkuu wa SHIRECU.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga Revocatus Kuuli aliwahakikishia Wamiliki wa Kiwanda cha Pamba cha Manongo wasiwe na wasiwasi kuhusu upatikanaji malighafi ya kutosha kwa ajili ya kiwanda hicho,kwani uongozi umeshajipanga kuhakikisha msimu ujao wananchi walima Pamba kwa wingi na wanavuna pamba nyingi kuliko ya msimu uliopita.

Alisema pamoja na jitihada kuwa za muda mfupi msimu uliopita Wakulima katika Wilaya ya Igunga walifanikiwa kuzalisha kilo 10, 700,000 ,msimu ujao wanatarajia mavuno kuwa mara mbili ya kilo hizo na hivyo kuwa malighafi nyingi kwa ajili ya viwanda..

Kiwanda hicho kinamilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Igembensabo kwa asilimia 20 na M/S Rajani Metals and Machinery Ltd mwenyewe anamikili asilimia 80.

Kiwanda cha Manonga ambacho kilijengwa mwaka 1958 na Kampuni ya wafanyabiashara binafsi na mnamo mwaka 1962 Serikali ilikitaifisha na kuipatia Kampuni ya Wakulima wa Kahama na Nzega (KANZECO) kina miaka zaidi ya ishirini bila kufanya kazi.

No comments: