Wednesday, September 27, 2017

MAWASILIANO YAONGEZA KASI YA UKUSANYAJI WA MAPATO YA SERIKALI

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King akisisitiza jambo wakati wa ziara ya Kamati ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mnara wa TTCL kwenye kijiji cha Sanga Itinje kilichopo Kata ya Itinje wilaya ya Meatu mkoani Simiyu. Kushoto kwa Mwenyekiti ni Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Eng. Peter Ulanga.


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bwana John Mongella akiongea kuhusu mchango wa mifumo ya mawasiliano katika kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali mbele ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu na watendaji wa kampuni za simu wa mkoani Mwanza (hawapo pichani) wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua ujenzi wa minara, ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini mkoani Mwanza. Aliyeketi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King. 


Meneja wa TTCL mkoa wa Shinyanga Bwana Abdallah Lugage akitoa taarifa kwa Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mnara wa kampuni hiyo kwenye kijiji cha Sanga Intinje kilichopo kata ya Intinje wilaya ya Meatu mkoani Simiyu. Wa tatu kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo Prof. Norman Sigalla King.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, watendaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, wafanyakazi wa TTCL na wanakijiji wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mnara wa kampuni hiyo kwenye kijiji cha Sanga Intinje kata ya Intinje iliyopo wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.


Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli imesisitiza kwa taasisi za Serikali, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla kulipa kodi kwa wakati ili nchi iweze kuongeza mapato yake kwa lengo la kukuza uchumi, kujenga miundombinu ya barabara, reli, bandari, mawasiliano, kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kuweza kuwatumika wananchi.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Prof. Norman Sigalla wakati wa ziara ya Kamati yake ya kukagua ujenzi wa minara, ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini na kwenye maeneo yasiyo na mvuto wa kibishara kwenye mikoa ya kanda ya ziwa ya Mwanza na Mara ambapo Serikali imetoa ruzuku kwa makampuni ya simu za mkononi ili ziweze kutoa huduma za mawasiliano kwa wananchi kupitia Mfuko wa Mawasiliao kwa Wote (UCSAF) ulio chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Ameongeza kuwa Kamati yake inasimamia sekta ya miundombinu yote nchini ikiwa ni pamoja na miundombinu ya mawasiliano ambayo inategemewa na Serikali katika kukuza uchumi na kuiwezesha nchi yetu kufikia uchumi wa kati na kuwa nchi ya viwanda. Prof. Norman Sigalla King amesema kuwa miundombinu na huduma za mawasiliano ni moja ya nguzo kuu za ukuaji wa uchumi, inachochea maendeleo ya taifa letu na kuiwezesha Serikali kuhudumia wananchi wake kwa haraka, wakati, kwa ufanisi na kupunguza gharama za Serikali kuwahudumia wananchi na kuokoa muda. “Serikali imepeleka fedha nyingi kwa ajili ya miundombinu mbalimbali ya nchi yetu kupitia Wizara hii kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2017/2018 ili nchi iweze kusonga mbele”, amesema Prof. Norman Sigalla King.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bwana John Mongela ameieleza Kamati hiyo kuwa mifumo ya mawasiliano imeiwezesha Serikali ya Mkoa wake kuongeza makusanyo ya mapato katika Halmashauri za mkoa huo kutoka chini ya asilimia 46 kwa mwaka wa fedha uliopita na kufikia asilimia 70 kwa mwaka huu wa fedha ambapo Halmashauri hizo zinatumia zaidi ya asilimia 70 ya makusanyo hayo kuendesha miradi ya maendeleo na kutekeleza majukumu mengine ya mkoa. 

“Suala la mawasiliano duniani popote pale ni nyeti sana kwa kuwa shughuli zote zinafanywa na mawasiliano kama vile miamala ya kifedha, ulinzi na usalama wa raia na mali zake ambapo katika ngazi ya Mkoa tumedhibiti kwa kiwango kikubwa ulinzi na usalama wa raia wetu na hali ya mawasiliano kwenye mkoa wetu ni nzuri na tuna Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano,” amesema Mongella. Ameongeza kuwa Mkoa huu ni mkoa wa pili kwa ukubwa wa idadi ya watu na ni mkoa wa pili ambao unaongoza kwa kuchangia kwa kiasi kikubwa mapato na ukuaji wa uchumi wa taifa letu.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Eng. Peter Ulanga amesema kuwa Mfuko umetoa ruzuku kwa kampuni za simu za mkononi ili kufikisha huduma za mawasiliano kwenye mikoa ya kanda ya ziwa na visiwa vyake takribani 36 vilivyopo kwenye kanda hii ili waweze kutumia mawasiliano kwa ajili ya ulinzi na usalama na shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii. 

Ameongeza kuwa kupitia Halotel, UCSAF imepeleka mawasiliano kwenye vijiji 78 vilivyopo kanda ya ziwa na ziara hii inatusaidia kupata maoni ya wadau na kukusanya changamoto ambazo zitasaidia kuboresha jukumu la UCSAF la kufikisha huduma za mawasiliano vijijini na maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara nchini nzima.

Mtaalamu wa miundombinu wa kampuni ya simu ya Halotel wa Mkoa wa Mwanza na Simiyu Bwana Emmanuel Masanja amesema kuwa kampuni yao inajenga minara kwa kukodisha au kupewa ardhi na mamlaka za serikali za vijiji kwa ajili ya ujenzi wa minara hivyo wanaishukuru Serikali kuwapatia ruzuku ya kufikisha mawasiliano vijijini.

Ameongeza kuwa baadhi wa watu wanazuia maendeleo ya ujenzi wa minara kwenye baadhi ya maeneo vijijini ambapo yanasababisha migogoro ambayo inachukua muda mrefu kukamilishwa hivyo kuchelewesha ujenzi wa minara na ufikishaji wa huduma za mawasiliano vijijini.

Bwana Masanja amesema kuwa kampuni yao wanaiomba Serikali iwasaidie kusimamia upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa minara ya mawasiliano kwenye ngazi ya Halmashauri zote nchi nzima ili kuwawezesha wakandarasi kujenga minara kwa wakati ili kuharakisha jitahada za Serikali ya Awamu ya Tano Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufikisha huduma za mawasiliano kwenye vijiji vyote nchi nzima na maeneo yasiyokuwa na mvuto wa kibiashara.

Aidha Mkurugenzi wa Kanda ya Ziwa wa kampuni ya TIGO Bwana Ally Maswanya ameishukuru Serikali kwa kuwapatia ruzuku ya kujenga minara na kufikisha huduma za mawasiliano vijijini kwa kuwa kampuni zetu zinafanya biashara hivyo haikuwa rahisi kwa kampuni za simu za mkononi kuwekeza bali UCSAF imetuwezesha kusambaza mawasiliano vijijini. Vile vile ameiomba Serikali kuwasaidia kufikisha umeme kwenye minara kupitia Wakala wa Nishati ya Umeme Vijijini (REA) kwa kuwa inawapa changamoto ya kuongeza gharama za kuendesha minara hiyo na umeme wa jua hautoshelezi.

Ameongeza kuwa sisi kama kampuni ya Halotel tunapata ushirikiano mkubwa kutoka ofisi za Wakuu wa Mikoa na wilaya kwenye maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kujenga minara bali changamoto ipo kwenye ngazi za Halmashauri za upatikanaji wa ardhi na utatuzi wa migogoro ya ardhi na ukosefu wa ushirikiano wa kutosha kutoka kwa mamlaka husika ili kufanikisha ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini.

Mwenyekiti Prof. Sigalla amesema kuwa nguzo za uchumi mojawapo ni miundombinu kwa maana ya barabara, bandari, reli na mawasiliano na ndiyo maana serikali imepeleka fedha nyingi kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/18. Ametoa rai kwa wananchi kuwa watoe ulinzi kwenye minara yote ya mawasiliano nchini kwa kuwa Serikali inatumia kodi za wananchi kujenga minara. 

Ameongeza kuwa wananchi watumie fursa ya mawasiliano kwa maendeleo na kujenga uchumi wao na maendeleo ya taifa. Pia ameyaomba makampuni ya simu yote nchini ambayo yamepatiwa ardhi na serikali ya kijiji na kujenga minara irudishe faida kwa wananchi wa eneo husika kwa kuwapatia fedha au huduma za kijamii.

Amesisitiza kuwa kampuni za mawasiliano zitumie fedha waliyopewa na Serikali kujenga minara na kufikisha huduma za mawasiliano vijijini kwa wakati kwa kuwa ucheleweshaji wa kutekeleza jukumu hilo unawanyima wananchi haki ya kupata huduma za mawasiliano. Pia ameongeza kuwa kwa namna yoyte ile kampuni haziwezi kulipa gharama za ucheleweshaji wa kujenga minara hiyo na upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi na Serikali kwa ujumla. “Maendeleo ni vita, ukipewa ruzuku na Serikali ya kujenga minara na ukichelewesha ni hasara; hakikisheni mnakimbizana kukamilisha jukumu hilo kwa wakati,” amesema Prof. Norman Sigalla King.

Aidha, ametoa rai kwa kampuni za simu zinazopatiwa ardhi bure na Serikali za vijiji mbalimbali nchini kote kutoa fedha kwa vijiji hivyo sehemu ya fedha wanazopata ili vijiji viweze kunufaika na uwepo wa minara hiyo kwa kuwa kampuni zinafanya biashara. 

Ametanabaisha kuwa minara haina madhara kwa wananchi ukilinganisha na usikilizaji wa simu za mkononi kwa muda mrefu zaidi ya dakika tisa. Amewatahadhirisha wananchi kuwa wananchi wasikilize simu kwa muda mfupi na isizidi dakika tisa.

“wananchi watumie vifaa vya kusikiliza simu masikioni kwa wale ambao wanasikiliza simu kwa muda mrefu na minara inayowekwa na UCSAF ni salama na tumieni simu kwa maendeleo chanya,” amesema Prof. Norman Sigalla King. Pia ameipongeza Wizara kwa kazi kubwa inayofanya ya kujenga na kusimamia miundombinu iliyopo kwenye sekta ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments: