Tuesday, September 26, 2017

JICA YAPONGEZWA KWA KUDUMISHA USHIRIKIANO NA TANZANIA

Na.Thobias Robert- MAELEZO.

Serikali imelipongeza Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kwa ushirikiano wake na Tanzania katika miradi mbalimbali ya maendeleo hasa katika sekta za Kilimo Afya na Maendeleo ya Jamii kwa kutumia wataalam na uzoefu kutoka Japan.

Pongezi hizo zimetolewa Jijini Dar es Salaam leo na Mkurugenzi Msaidizi wa ushirikiano wa kiufundi kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw.Msafiri Marwa alipokuwa akiwaaga vijana wa kijapani waliokuwa wanajitolea katika sekta ya Kilimo na Maendeleo ya jamii hapa nchini.

“Serikali ya Japan kupitia shirika lake la JICA imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na serikali ya Tanzania katika sekta mbalimbali kama vile kuwajengea uwezo Watanzania kupitia ufadhili wa masomo ya elimu ya juu nchini Japan na kuleta watu wa kujitolea katika miradi ya maendeleo hapa nchini,” alieleza Bw. Marwa.

Aidha, Bw.Marwa ambaye alimuwakilisha Naibu Katibu Mkuu Utumishi Bi. Suzani Mlawi aliipongeza Japan kwa kutumia rasilimali watu pamoja na rasilimali fedha kupitia JICA kufadhili utoaji wa huduma za kijamii jambo ambalo ni kipimo cha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.

Amewapongeza vijana wa kijapan kwa kazi nzuri waliyoifanya hapa nchini katika kipindi chote cha miaka miwili ya kuwahudumia watanzania hasa katika sekta ya Kilimo na Afya.

“Kwa niaba ya serikali niwapongeze vijana wote mliokuja hapa nchini kwa kufanya kazi na jamii ya Watanzania, mmefanya kazi kwa jitihada kubwa wakati mwingine katika mazingira magumu, niwahakikishie kuwa serikali ya Tanzania itaendelea kuimarisha mazingira ya ushirikiano ili kuendeleza uhusiano ” alifafanua Marwa.

Mkurugenzi huyo pia aliwakumbusha vijana hao kuwa mabalozi wazuri nchini Japani na mataifa mengine watakayokwenda ili kuwavutiwa wawekezaji na watalii kuja kuwekeza katika shughuli za maendeleo pamoja na kuleta watalii wengi kwani Tanzania ina vivutio vingi vya utalii, mazingira rafiki kwa wageni na amani ya kutosha.

Kwa upande wake, Mratibu wa kundi la vijana wa kujitolea kutoka JICA Bw.Ichiro Owa alisema kuwa, anaipongeza serikali ya Tanzania kwa kuwapokea na kuwapa ushirikiano na ulinzi wa kutosha vijana waliokuja kujitolea katika shughuli za maendeleo kwa siku zote ambazo wamekuwa hapa nchini.

“Mpango wetu kwa sasa ni kuleta vijana wengi zaidi wa kujitolea kwasababu ya ushirikiano tulioupata kutoka kwa serikali ya Tanzania ni mzuri kwani tumefurahia usalama amani na utulivu pamoja na ukarimu wa watanzania ” alifafanua Bw. Owa.

Mratibu huyo wa vijana wa kujitolea kutoka Japan alisema ushirikiano kati ya nchi yake na Tanzania ni wa kihistoria na umekuwa wa manufaa kwa pande zote mbili, aliongeza kuwa kwa mwaka huu, JICA ina jumla ya vijana 40 wanaojitolea na matarajio yao ni kuongeza vijana kati ya 60 hadi 70 kwa mwaka ujao.

Vijana wa kujitolea walioagwa katika hafla hiyo ni pamoja na Kyoko Tada aliyekuwa akifanya kazi ya Uuguzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Shu Sato aliyekuwa katika Ofisi ya Kilimo Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro na Yusuke Sakakibara aliyekuwa anafanya kazi ya maendeleo ya jamii katika Wilaya ya Masasi.

JICA ilianza mpango wake wa kuleta vijana wa kujitolea katika shughuli mbalimbali za maendeleo mwaka 1967 ambapo takwimu zinaonyesha kuwa tangu kuja kwa kundi la kwanza kutoka Japani idadi imeongezeka kufikia vijana 1,568.
Mkurugenzi Msaidi wa Ushiririkiano wa Kiufundi kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Msafiri Marwa akimkabidhi zawadi kijana wa Kijapan aliyemaliza muda wake wa kujitolea hapa nchini Bw. Yusuke Sakakibara.
Mkurugenzi Msaidi wa Ushiririkiano wa Kiufundi kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Msafiri Marwa akimkabidhi zawadi kijana wa Kijapan aliyemaliza muda wake wa kujitolea hapa nchini Kyoko Tada katika hafla ya kuwaaga vijana watatu wa kijapan waliomaliza muda wao wa kujitolea hapa nchini iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa vijana wa kujitolea Kutoka JICA nchini Tanzania Bw. Ichiro Owa (kulia) akielezea jambo wakati wa hafla ya kuwaaga vijana waliomaliza muda wao wa kujitolea hapa nchini kutoka Japan iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni mmoja wa waliokuwa wakijitolea Kyoko Tada.
Baadhi ya Raia wa Japan waliokuwa wakijitolea nchini kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) wakiwa katika hafla ya kuwaaga baada ya kumaliza muda wao leo jijini Dar es Salaam. Kutoka kulia ni Yusuke Sakakibara akiifanya Wilayani Masasi, Shu Sato, Kyoko Tada Mratibu wa vijana wa kujitolea Kutoka JICA nchinI Tanzania Bw. Ichiro Owa mara baada ya hafla kuwaga leo jijini Dar es Salaam.
Picha na: Paschal Dotto – MAELEZO

No comments: