Na Mathias Canal, Singida
Vijana wametakiwa kusimamia misingi ya Nidhamu ndani na nje ya Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi kwa kuhuisha mshikamano ili kulinda misingi ya Utaifa na uwajibikaji kwani wao ndio nguvukazi ya Taifa na ushindi wa Chama Cha Mapinduzi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya siasa Wilaya wakati akizungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Ikungi kwenye mkutano wa uchaguzi wa viongozi wa Jumuiya hiyo katika ukumbi wa shule ya Sekondari Ikungi.
Mhe Mtaturu alisema kuwa Dhana ya Demokrasia ni jambo muhimu linalohitaji kuheshimiwa na kuenziwa ndani ya Chama na Jumuiya zake hivyo kuimarisha nidhamu, mshikamano na upendo ndio silaha pekee itakayoleta heshima ndani ya jumuiya ya vijana wa CCM ili iweze kusonga mbele zaidi na kuwa na mafanikio makubwa katika kuimarisha kipato cha vijana.
Alisema kuwa Nia ya UVCCM ni kujenga na kudumisha haiba njema ya kuendelea kuheshimu misingi ya demorasia ya kweli, yenye kuchunga adabu na kufuata nidhamu, miiko na maadili kwa kila mwanachama anayetaka kutumia haki ya kuchagua au kuchaguliwa.
Alisema kuwa mkutano huo unapaswa kuchagua viongozi waadilifu watakaohuisha misingi ya mshikamano na ujenzi wa CCM Mpya ili kuondoa malumbano yenye kupandikiza chuki na kupalilia mifarakano isio na ulazima.
Alisema wapo baadhi ya vijana wanatumia vibaya nafasi zao katika Jumuiya hiyo kwa kuwachafua wenzao kwenye mitandao ya kijamii na wakati mwingine wapo wanaothubutu kuwatukana wenzao matusi ya nguoni kinyume na ustaarabu, ubinadamu na misingi na Maadili ya Chama Cha Mapinduzi.
Wapo baadhi yao hujivika kofia ya Jumuiya wakitumia njia hatari na batili, kwa kukebehi, kutuhumu wenzao kinyume na utaratibu huku baadhi yao hata kufikia kutoa madai yanayovuka mipaka na kubeba taswira ya Jinai au madai.
“Ndugu zangu Kwa miaka yote wanajumuiya na viongozi wote wa CCM wamekuwa wakiishi kwa kuzingatia misingi ya Umoja, Upendo, mashauriano na kudumisha Maelewano hivyo nakushaurini nyote kuvienzi ili kuwa na CCM Mpya itakayowaletea wananchi maendeleo na kuendelea kuongoza dola” Alisema mHe Mtaturu
Mhe Mtaturu alisema Uchaguzi ni kipimo cha kupevuka na kielelezo cha ukomavu wa demokrasia ya kweli bila mizengwe au hila ndani ya chama na Jumuiya kwa lengo la kusimamia shabaha na misingi sahihi itokanayo na miongozo, maelekezo na kuheshimu utaratibu unaohimizwa na Chama Cha Mapinduzi .
Alisema Ili kuonyesha kutii na kufuata maelekezo yanayotolewa mara kwa mara na Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Joseph Magufuli kila mwanachama anapaswa kujitambua, kujiheshimu, kufuata misingi ya katiba na kuepukana na rushwa ili kulinda heshima ya Chama Cha Mapinduzi.
Mhe Mtaturu pia alizitaja fursa zilizopo katika Wilaya ya Ikungi ambazo vijana wanaweza kuzitumia ili kuimarisha kipato chao kuwa ni pamoja na Kilimo cha Korosho, Mpunga, Pamba na Ufugaji wa kuku.
Pia aliwasihi vijana kuanzisha vikundi mbalimbali vya ujasiriamali na kuvisajili ili waweze kupatiwa mikopo ya asilimia 5% kwa vijana inayotolewa na Halmashauri za Wilaya kote nchini.
“Nawakumbusha kuwa tumeanzisha Mfuko wa Elimu Wilaya ili kuboresha elimu katika Wilaya yetu kwa hiyo nawasihi vijana wote kujitokeza kwenye kata zenu ili kushiriki shughuli ya ufyatuaji matofali ambayo tumeelekeza kila Kata kufyatua matofali 10,000” Alisema Mtaturu
Mhe Mtaturu pia aliwasihi vijana kushiriki kufanya kazi za kijamii ikiwa ni pamoja na kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM 2015-2020, kushiriki kuona shughuli mbali mbali za uzalishaji Mali kupitia makundi ya vijana na kuwasaidia kwa kuwaunga mkono ili kuongeza mtaji wa miradi yao.
Sambamba na hayo pia aliwatakia uchaguzi mwema wenye amani na utulivu, ambapo aliwasihi pindi watakapomaliza uchaguzi huo kuwa wamoja na kuvunja makundi ili kuendelea kuimarisha Jumuiya hiyo na Chama Cha Mapinduzi.
No comments:
Post a Comment