Katika kuadhimisha maonesho hayo ya Nane Nane yanayofanyika viwanja vya Nzuguni
nje kidogo ya mji wa Dodoma, banda la Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania-
Tawa limekuwa kivutio kikubwa kwenye maonesho hayo ambayo yameanza rasmi
tarehe 1/8/2017.
Kivutio hicho kimetokana na kuleta wanyamapori mbalimbali wakiwepo Simba, Chui,
Nyati, Chatu, Nyoka mbalimbali, Ndege mbali mbali, Fisi na Tausi. Kwa mara ya kwanza
maonesho haya ya kuleta wanyamapori hai yalikuwa yanafanywa na Idara ya
Wanyamapori. Safari hii TAWA wameamua kuongeza idadi ya wanyama ambayo
haikuwapo hapo awali. Mfano Nyati na Mamba.
Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa habari na Mahusiano wa TAWA Bw. Twaha
Twaibu aliwaeleza Wandishi wa Habari kuwa TAWA inashiriki kwa mara ya kwanza
katika maonesho haya. Aliendelea kusema TAWA ni Mamlaka iliyoanzishwa kwa Amri
ya Serikali na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali Na.135 la tarehe 9 Mei, 2014.
Uanzishwaji wa Mamlaka hii ni utekelezaji wa kifungu cha 8 cha Sheria ya kuhifadhi
Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009. Mamlaka ya Wanyamapori imeanza kazi rasmi
tarehe 1/Julai/2016. Makao Makuu yake kwa sasa yapo mjini Morogoro.
Bw. Twaibu alielezea Wanahabari kwa kusema Mamlaka ilianzishwa na Serikali kama
chombo cha utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa niaba ya Serikali chini ya
uangalizi wa Serikali na kuwa na mfumo unaonesha utekelezaji wa majukumu kwa
ufanisi zaidi. Kama ilivyo kwa Mamlaka Serikali nyingine nchini, lengo la kuanzishwa
TAWA ni kutekeleza majukumu ya Idara ya Wanyamapori hasa ya Usimamizi wa
Wanyamapori nchini. Majukumu ya TAWA ni kusimamia shughuli za utawala, ulinzi,
usimamizi wa raslimali ya Wanyamapori katika maeneo yote nje ya Hifadhi za Taifa na
Hifadhi ya Ngorongoro.
Wandishi wa Habari walitaka kupata kauli ya TAWA na Wizara ya Maliasili na Utalii
kuhusu ujenzi wa mradi wa uzalishaji umeme wa Stiglers Gorge uliyoko ndani ya Pori la
Akiba Selous, kama TAWA na Wizara wanasemaje?
Bw. Twaibu aliwaeleza wanahabari kuwa kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na TAWA
kama Wasimamizi Wakuu wa Pori la Akiba Selous (Urithi wa Dunia) wanaunga mkono
maamuzi ya Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuri kujenga mradi mkubwa wa uzalishaji wa
umeme katika Mto Rufiji kwenye Pori la Akiba la Selous ambao ukikamilika unatarajiwa
kuzalisha zaidi ya megawati 2,100.
Aidha Bw.Twaibu akiwa kama mhifadhi na mtu wa habari amesisitiza kuwa ujenzi wa
mradi huo hauna tafsiri kwamba Tanzania haithamini masuala ya uhifadhi bali
unazingatia uhifadhi wenye manufaa kwa jamii na maendeleo ya taifa na hasa dhamira
ya Serikali ya rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli kuelekea Tanzania ya Viwanda
ambayo inahitaji nishati ya umeme itakayotosheleza mahitaji ya Taifa.
Twaibu amesema Tanzania inatambua umuhimu wa uhifadhi ndiyo maana imetenga
eneo la zaidi ya asilimia 28 ya eneo lote la nchi kavu Tanzania bara kwaajili ya uhifadhi
wa aina mbalimbali ukiwemo wa wanyamapori na misitu ya vyanzo vya maji ambayo ni
muhimu kwa shughuli za kijamii na kiuchumi “ni nchi chache sana duniani zenye eneo
kubwa la uhifadhi kama Tanzania,” alisisitiza Twaibu.
Ametoa mfano wa nchi ya Qatar ambayo amesema ilikuwa na eneo la uhifadhi
lililokuwa kwenye orodha ya maeneo ya Urithi wa Dunia) kutokana na uwepo wa baadhi
ya viumbe adimu lakini walipogundua mafuta, waliamua kujitoa kwenye urithi wa dunia
ili wachimbe mafuta na kuinufaisha nchi hiyo na maendeleo ya wananchi wake.
Alipoulizwa kuhusu TAWA inakabiliana vipi au inasemaje kuingiza mifugo kwenye
Maeneo ya Mapori ya Akiba na Tengefu. Bw. Twaibu alisema tatizo la mifugo kwenye
maeneo yaliyohifadhiwa TAWA inatekeleza Sheria Na.5 ya Mwaka 2009 ya
Wanyamapori kutoruhusu kuingiza mifugo kwenye maeneo ya Hifadhi.
TAWA kwa
kushirikiana na vyombo mbalimbali vya ulinzi na Mahakama inasimamia Sheria hii
iliyotungwa na Bunge la Jamahuri ya Muungano wa Tanzania ambazo zinakataza mifugo
kuingia hifadhini kinyume cha Sheria.
Bw. Twaibu amewaomba wananchi kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo katika
Mapori ya Akiba kwa kutolea mfano Pori la Akiba Selous ambalo ndilo pori kubwa kuliko
yote Barani Afrika lenye ukubwa wa eneo za mraba zaidi ya 50,000. Kuna vivutio vya
utalii na wanyamapori mbalimbali wakiwemo Tembo wakubwa kuliko wote hapa nchini,
kuna Nyati, Twiga, Viboko, Swala, na Ndege mbalimbali linasimamiwa na TAWA.
Twaibu amewaomba pia wananchi wa Dodoma pia wanaweza kutembelea pori la Akiba
ambalo lipo ndani ya Mkoa wa Dodoma pori la Akiba Swagaswaga katika wilaya za
Kondoa, Singida Vijijini na Chemba kuna wanyama mbalimbali.
Na mwisho amewaomba wananchi wote wa Dodoma waje kutembelea Banda la Wizara
ya Maliasili na Utalii kujionea vivutio mbalimbali vya utalii wakiwepo wanyampori hai,
ambao watapewa maelezo ya kutembelea maeneo wanakoishi na jinsi ya kufika
maeneo hayo kama utalii wa ndani.
No comments:
Post a Comment