Na Chalila Kibuda, Lindi.
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Michael Isamuhyo ameiomba Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kubuni mpango maalum wa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana wanaoingia katika mafunzo ya JKT ili wakitoka katika makambi waweze kupata fursa za ajira katika maeneo mbalimbali.
Meja Isamuhyo alitoa ombi hilo Jumatatu, Agosti 7, 2017 alipotembelea kwenye banda la VETA, katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa kwenye uwanja wa Ngongo, mkoani Lindi.
Alisema vijana wanapoingia katika makambi ya JKT hupata mafunzo ya uzalendo na ukakamavu kwa kipindi cha takribani miezi mitatu na kisha kuingia katika mafunzo ya stadi za maisha na stadi za kazi kwa kipindi kipatacho miezi 18.
Alifafanua kutokana na mgawanyiko huo wa mafunzo ya JKT, VETA kwa kushirikiana na jeshi hilo wanaweza kuweka mpango maalum wa kutumia kipindi cha miezi 18 ya mafunzo ya stadi za kazi na stadi za maisha kuandaa mafunzo ya ufundi stadi ili kuwapatia vijana ujuzi utakaowawezesha kuajirika baada ya kuhitimu JKT.
Alisema JKT wamekuwa wakitoa mafunzo ya ufundi stadi mbalimbali, lakini changamoto imekuwa ni kukidhi vigezo vya kutunuku vyeti vinavyotambulika na VETA, kwani kipindi cha miezi minane ni kifupi katika kukidhi matakwa ya mitaala ya VETA.
Alisema kutokana na vijana hao kushindwa kupata vyeti vinavyotambulika na VETA ambayo ni mamlaka ya kitaifa inayodhibiti na kusimamia mafunzo ya ufundi stadi, inakuwa vigumu kwao kukubalika katika ajira au kujiendeleza katika maeneo mbalimbali ya stadi walizozipata.
Alishauri kuwa, kama mazungumzo na mipango mizuri itawekwa na VETA kwa ushirikiano na JKT, kipindi hicho cha miezi 18 ya mafunzo ya JKT kinaweza kupangwa vyema katika namna ambayo vijana watatimiza masaa yanayohitajika kufuzu mafunzo ya ufundi stadi katika ngazi husika, hivyo kutunukiwa vyeti vinavyotambulika na VETA.
Akijibu juu ya suala hilo, Meneja Uhusiano wa VETA, Sitta Peter alimshukuru Mkuu wa JKT huyo kwa ushauri na mawazo mazuri na kuahidi kuyafikisha katika Menejimenti ya VETA kwa majadiliano na utekelezaji.
Alikiri kuwa ni kweli kundi hilo la vijana wanaoingia katika mafunzo ya JKT ni nguvukazi muhimu ikiwa wataandaliwa vyema katika mafunzo ya ufundi stadi baada ya mafunzo ya ukakamavu na uzalendo yanayotolewa na JKT.
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Michael Isamuhyo akipata maelezo kutoka Mtaalam wa Kutathimini mafunzo wa VETA Joyce Mwinuka juu ya VETA inavyofanya kazi katika kuwajenga vijana katika mafunzo ya elimu ya ufundi stadi katika maonesho ya Nanenane katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Michael Isamuhyo akipata maelezo kutoka kwa Meneja uhusiano wa VETA, Sitta Peter wakati mkuu wa JKT alipotembelea maonesho ya Nanenane katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Michael Isamuhyo akipata maelezo wa tofari ambazo zinaokoa gharama kutokana mazingira ambayo kila mwananchi anaweza kumudu wakati mkuu wa JKT alipotembelea maonesho ya Nanenane katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.
Shamba darasa la JKT ndani maonesho ya Nanenane katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.
No comments:
Post a Comment