Tuesday, August 1, 2017

TAARIFA ZA MICHEZO KUTOKA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

DK. NDUMBARO, MGONGOLWA WATEULIWA TFF
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, imeteua Kamati ya Rufaa ya Leseni za Klabu, ikiwa ni maandalizi ya kuanza msimu mpya wa mashindano ya soka yanayosimamiwa na kuendeshwa na TFF.
Viongozi na wajumbe waliteuliwa na kupitishwa Jumapili Julai 30, 2017 katika Mkutano wa Kamati ya Utendaji uliofanyika Ukumbi wa Hosteli za TFF, zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam yaliko Makao Makuu ya shirikisho.
Viongozi na Wajumbe walioteuliwa ni Msomi Wakili Dk. Damas Ndumbaro atayekuwa Mwenyekiti; Msomi Wakili Alex Mngongolwa (Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo) wakati Wajumbe ni Meneja wa zamani wa Uwanja wa Taifa, Charles Matoke, Tumainiel Mlango na Ahmed Menye.
Viongozi wa Kamati hiyo watakuwa na majukumu ya kusililiza rufaa kutokana na uamuzi wa Kamati ya Leseni za Klabu inayoongozwa na Msomi Wakili Lloyd Nchunga ambayo inasimamia utekelezaji wa Kanuni ya 11 ya Ligi Kuu.
Kwa mujibu wa kanuni hiyo ya 11, Klabu za Ligi Kuu zinawajibika na kutakiwa kuwasilisha maombi ya kupatiwa Leseni ya Klabu kwa TFF katika muda utakaotangazwa na Kamati ya Utendaji ya TFF na kuhakikisha zinakidhi masharti na vigezo vyote vya msingi kupatiwa leseni ili kuweza kushiriki Ligi Kuu.
Kanuni hiyo ya 11 inasema kwamba Klabu itakayoshindwa kukidhi kiasi cha kukosa Leseni haitashiriki Ligi Kuu kwa msimu husika. Vigezo hitajika kwenye kupata leseni ya klabu ni kuwa na Uwanja wa nyumbani wa mechi, uwanja wa mazoezi, umiliki wa klabu moja, kuwa na timu ya vijana, uwepo wa ofisi rasmi na watendaji wake akiwamo mtendaji mkuu (CEO) na maofisa masoko, habari na mhasibu mwenye taaluma ya uhasibu.
Tayari Klabu zilielekezwa kuwasiliana na Meneja wa Leseni za Klabu, Jemedari Said ambaye ni Ofisa Maendeleo ya Mpira wa Miguu Tanzania wa TFF kwa ajili ya maelezo ya kuchukua na kurejesha fomu kwa mujibu wa taratibu na kanuni za mashindano kabla ya kuanza rasmi mashindano.


LIGI DARAJA LA KWANZA TANZANIA BARA 2017/18
Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara inatarajiwa kuanza Septemba 16, mwaka huu kwa timu 24 zilizogawanywa katika makundi matatu yenye timu nane kila kundi.
Tayari TFF, ilikwisha kutangaza makundi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa timu 24 zitakazochuana msimu huu wa 2017/18 kuwania nafasi tatu muhimu za kupanda daraja kucheza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2018/19.
Kwa mujibu wa makundi hayo yaliyoratibiwa na Bodi ya Ligi ya TFF, kundi ‘A’ litakuwa na timu za African Lyon, Ashati United, Friends Rangers za Dar es Salaam, JKT Ruvu na Kiluvya United za Pwani, Mgambo JKT ya Tanga, Mvuvumwa ya Kigoma na Polisi Moro ya Morogoro.
Kundi ‘B’ zitakuwa timu za itakuwa na timu za Coastal Union ya Tanga; JKT Mlale ya Ruvuma; KMC ya Dar es Salam, Mawezi Market ya Morogoro, Mbeya Kwanza ya Mbeya, Mufundi United ya Iringa, Mshikamano na Polisi Dar za Dar es Salaam.
Kundi ‘C’ ina timu za Alliance School, Pamba na Toto African za Mwanza, Rihno Rangers ya  Tabora, Polisi Mara ya Mara, Polisi Dodoma ya Dodoma, Transit Camp ya Shinyanga na JKT Oljoro ya Arusha.
Kadhalika, TFF imeagiza timu za Ashanti United, Friends Rangers, KMC na Polisi Dar ya Dar es Salaam kuwasilisha majina ya viwanja vitakavyotumiwa na timu zao wakati wa ligi hiyo inayotarajiwa kuanza baadaye mwezi ujao.
Kutaja viwanja hivyo ni matakwa ya Kanuni ya 6 (1) za kanuni Mama ya VPL inayozungumzia Viwanja kadhalika kusomwa pamoja na Kanuni ya 11 inayozungumzia Leseni za Klabu kwamba kila timu haina budi kuwa na viwanja vya mcehi za nyumbani ikiwa ni masharti ya kupata leseni ya klabu.

SEMINA YA MADAKTARI WA TIMU ZA LIGI KUU BARA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imeita semina ya siku moja kwa Madaktari wa timu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara itakayofanyika Ijumaa Agosti 4, mwaka huu kuanzia saa 2.00 asubuhi kwenye Ukumbi wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 73 ya Ligi Kuu, kila klabu ya Ligi Kuu inatakiwa kuwa na daktari wa timu ambaye pamoja na mambo mengine atahakiki afya za wachezaji na viongozi wa timu.
Kila klabu inatakiwa kuhakikisha daktari wake anahudhuria semina hii muhimu itakayoendeshwa na Kamati ya Tiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti wake Dkt. Paul Marealle.
Bodi ya Ligi itagharamia nauli ya basi ya kuja na kurudi Dar es Salaam kwa kila mshiriki. Tunawatakia kila la kheri katika maandalizi ya ushiriki wa semina hiyo ambayo ni sehemu ya maandalizi ya Ligi Kuu ya Vodacom kwa msimu wa 2017/2018.
  UCHAGUZI MKUU TAFCA AGOSTI 10, 2017
Uchahuzi Mkuu wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA utafanyika Agosti 10, mwaka huu mjini Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi), Ramadhani Mambosasa ametangaza orodha ya majina sita ya mwisho ya wagombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo.
Kwa mujibu Mambosasa, wagombea hao kwa sasa hawana budi kuendelea na kampeni hadi Agosti 9, mwaka huu.
Waliopitishwa katika orodha ya mwisho kuwania nafasi mbalimbali za uongozi - ngazi ya taifa ni pamoja na Kidao Wilfred, Lister Manyara, Michael Bundala, Dismas Haonga, Jamhuri Kihwelo, George Komba, Samuel Moja na Maka Mwalwasi na Mohammed Tajdin.
Nafasi zinazowaniwa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mweka Hazina, Wajumbe wa Mkutano Mkuu TFF na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
……………………………………………………………..………………………………
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

No comments: