Sunday, August 13, 2017

RIDHIWAN KIKWETE :AHIMIZA WANANCHI WAJITOLEE KATIKA SHUGHULI ZA MAENDELEO

 Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwan Kikwete ,akizungumza wakati wa uzinduzi wa madarasa sita na ofisi moja ya walimu katika shule ya msingi Pakistan utete kata ya Pera,yaliyokarabatiwa kwa ufadhili wa marafiki wa Pakistan.
Balozi wa Pakistan nchini,Amir khan wa kushoto na Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwan Kikwete,wakizindua majengo ya madarasa sita na ofisi moja ya walimu katika shule ya msingi Pakistan utete kata ya Pera,yaliyokarabatiwa kwa ufadhili wa marafiki wa Pakistan.
Balozi wa Pakistan nchini Tanzania,Amir Khan akizungumza baada ya kuzindua majengo ya madarasa sita na ofisi moja ya walimu yaliyokarabatiwa na marafiki wa Pakistan katika shule ya msingi Pakistan utete iliyopo kata ya Pera,kushoto kwake ni Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwan Kikwete.
Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwan Kikwete kushoto akiagana na balozi wa Pakistan nchini Amir Khan baada ya kuzindua majengo ya madarasa sita na ofisi moja ya walimu katika shule ya msingi Pakistan utete kata ya Pera,yaliyokarabatiwa kwa ufadhili wa marafiki wa Pakistan

Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
MBUNGE wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete,amewahimiza wananchi kujenga tabia ya kujitolea katika shughuli za kimaendeleo pasipo kuachia serikali/halmashauri na wahisani pekee.
Aidha amesema ofisi yake na halmashauri wataendelea kuunga mkono juhudi za wafadhili na wadau wanaojitokeza kushirikiana nao kutatua changamoto zinazowakabili jimboni hapo ikiwemo elimu.
Ridhiwani alitoa rai hiyo, wakati wa uzinduzi wa majengo ya madarasa sita na ofisi moja ya walimu katika shule ya msingi Pakistan Utete iliyopo kata ya Pera,Chalinze wilayani Bagamoyo,yaliyokarabatiwa kwa ufadhili wa marafiki wa Pakistan,kwa gharama ya sh.milioni.30.
Alisema baadhi ya wafadhili wanasaidia endapo wanaona jamii husika ikichukua juhudi  na kufikia hatua mbalimbali .
Aliwataka wananchi wa Chalinze kushirikiana na serikali,halmashauri na wafadhili wanaojitokeza ili kukamilisha miradi ya maendeleo iliyopo kwenye maeneo yao.
“Ajenda kubwa tuliyonayo ni kuboresha na kutatua changamoto katika sekta ya elimu”
“Pamoja na shughuli zinazofanywa na wahisani lakini haina budi wananchi mkajitolea katika shughuli za maendeleo ili tukienda kuomba msaada kwa wafadhili waweze kukubali kirahisi kwa kuona hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa  “alisema Ridhiwani.
Ridhiwani alisema wakati marafiki wa Pakistan wakiwezesha ukarabati huo,lakini halmashauri ya Chalinze imeshatenga fedha kwa ajili ya kujenga matundu ya vyoo nane katika shule ya Pakistan Utete.
Hata hivyo,mbunge huyo alieleza kwamba,pia wanajenga matundu ya vyoo katika shule ya msingi Mbala sanjali na madarasa mawili ya shule ya msingi Makombe.
Ridhiwani alieleza,ujenzi wa matundu ya vyoo utasaidia kuondoa kero ya uchafu wa mazingira ambapo baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakijisaidia ovyo maporini ,vichakani .
“Kwasasa kilichobakia ni usimamizi katika hatua ya ujenzi unaoendelea kwenye shule hizo ”alisema Ridhiwani.
Akizungumzia msaada walioupata kutoka kwa marafiki wa Pakistan,Ridhiwani aliomba ushirikiano ulioonyeshwa usiishie hapo .
Alimpongeza mwenyekiti wa kitongoji Hussein Mramba na diwani wa kata ya Pera kwa jitihada walizozichukua kusukuma jambo hilo.
Ridhiwani hakusita kumuomba balozi wa Pakistan nchini Tanzania,Amir Khan ,kuwasaidia ujenzi wa jengo la kulaza wagonjwa  na mashine za kupima magonjwa katika kituo cha afya Chalinze.

Akizindua majengo hayo,balozi wa Pakistan nchini Khan,alisema amefurahishwa na ushirikiano uliopo baina ya nchi hiyo na Tanzania,na alishauri kuwepo na mahusiano kati  ya wabunge wa Pakistan na Tanzania.

“Nilipoambiwa kuja shuleni hapa ni km 120 kutoka Dar es salaam nikaona nije kutembea na kuona kilichofanyika,Nawapongeza kwa kuanzisha ujenzi huu  ili watoto wapate elimu”alisema Khan.
Alisema ili watoto hao wasome vizuri ni vyema kukajengwa uzio katika shule hiyo ili kuweka usalama zaidi hivyo wanatasaidia kuujenga.
Balozi huyo,aliahidi na kukubali ombi la kusaidia mashine na vifaa vya kituo hicho cha afya lakini kwasasa wanachotakiwa kufanya ni kuandika maombi ya msaada huo.

No comments: