Na Karama Kenyunko Globu ya jamii.
Mgombea urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ali Mayay amesema kuwa katika uongozi wake atahakikisha dira ya mpira wa miguu inarejea katika mstari na kuiwezesha nchi kupata maendeleo makubwa katika sekta hiyo.
Mayay amesema hayo leo alipokuwa ananadi sera zake katika siku ya kwanza ya uzinduzi wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa TFF utakaofanyika Agosti 12, mkoani Dodoma. Amesema kuwa kwa sasa hakuna dira ya mpira wa miguu na ndio chanzo cha kuwa na maendeleo duni ya mpira kulinganisha na nchi zingine ambayo kwa sasa zinafaidi matunda baada ya kuanzisha na kutekeleza dira hiyo.
“Kwa sasa wachezaji wengi wa Zambia wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi, timu yao Taifa inafanya vizuri, Tanzania ina wachezaji wengi wenye vipaji, lakini hakuna dira na kusababisha wao pia kukosa dira katika fani yao,” alisema Mayay.
Alisema kuwa akiwa kama mchezaji, ameweza kuona changamoto mbalimbali za mpira wa miguu na kuamua kugombea nafasi iliyo ili kuzitatua na lengo lingine ni kujenga taasisi imara kwa kutumia rasilimali zilizopo kwani tatizo si vipaji, bali ni aina gani ya uongozi unaosimamia mpira wa miguu.
Wachezaji mbalimbali waliong’aa katika medani ya soka hapa nchini, wamepigia chapuo mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa, Taifa Stars Ali Mayay kuchaguliwa katika nafasi ya urais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Mgombea huyo ambaye ni chaguo la wachezaji wa zamani nchini aliungwa mkono na mshambuliaji nyota wa zamani wa Klabu ya Simba, Zamoyoni Mogella ambaye alisema TFF inahitaji mtu kama Mayay anayejua matatizo ya mpira wa miguu kwani ameucheza huo mpira.
Mogella ambaye enzi zake alipewa jina la “Golden Boy” na “Morgan” alisema kuwa wanahitaji kuurudisha mpira kwa wenyewe huku wakiwaomba wagombea kumchagua Mayay kwani ni wakati wa mabadiliko kwa wadau wa soka nchini kwa kumchagua Mayay ambaye anavigezo vyote katika masuala mbalimbali ya soka na uongozi.
“Mayay ni dira ya soka Tanzania, amecheza soka kuanzia shuleni, katika hatua ya vilabu mpaka timu ya Taifa, anajua nini cha kufanya ili kuleta maendeleo ya soka nchini,” alisema Mogella.
Mchezaji wa zamani wa Yanga Mohamed “Adolph” Rishad naye alisema kuwa Mayay ni suluhisho sahihi kwa maendeleo ya soka nchini na si wagombea wengine zaidi wachezaji wa mpira wa miguu wametengwa katika soka na kukosa mwamko katika mchezo ambao wanaupenda.
Amesema kuwa kwa sasa Tanzania ina matokeo mabaya katika soka la kimataifa ni kukosa uongozi wenye mapenzi ya mchezo pamoja na Tanzania kuwa na vipaji vingi vya soka.
No comments:
Post a Comment