Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha Vijijini
MBUNGE wa jimbo la Kibaha
Vijijini, mkoani Pwani, Hamoud Jumaa, ametoa msaada wa sh.milioni 2.3 kwa mkazi
wa kata ya Janga, Selemani Mgoto (43) ambaye alipata upofu kutokana na
kudhurika na vidonge vya malaria 'fansidar' mwaka 2012.
Aidha mbunge huyo, amesema ataendelea kumshika mkono Mgoto kwa
kumalizia ujenzi wa nyumba anayojenga. Jumaa pia ,anamjengea nyumba kada
wa chama cha mapinduzi (CCM) ambaye aliwahi kukitumikia chama zaidi ya miaka
30, mzee Shabani Kifaru (80), mkazi wa kata ya Magindu.
Akizungumza wakati akikabidhi fedha hizo, Jumaa alisema
ataendelea kutatua changamoto za jimbo pamoja na kusaidia makundi maalum. Alieleza,
ametoa fedha hizo kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa mtu huyo kuliko chakula
ambacho angekula na kuisha .
Alisema licha ya Mgoto kuathirika macho yake lakini anaishi kwenye
maisha ya kupanga hivyo nyumba anayojenga itamwezesha kuishi vizuri. Nae
Mgoto ,alimshukuru Jumaa kwa msaada aliompatia na kumuomba asichoke kumshika
mkono. Hata hivyo, aliwashukuru wadau wengine ambao wameweza kumsaidia
tangu apate matatizo yake.
"Mbunge una watu
wengi wa kuwasaidia lakini umeniona na mie, naahidi kuzitumia fedha hizi kwa
matumizi lengwa ,nilianza ujenzi huu lakini ninekwama kumalizia "alisema
Mgoto.
Akizungumzia juu ya tatizo lake la macho alisema bado amekwama
kwenda nchini India kupata matibabu. Alisema Muhimbili walimwambia atafute
msaada mtaani lakini amekwama. Mgoto alimuomba waziri wa afya,jinsia,
wazee na watoto Ummy Mwalimu na mbunge huyo waendelee kumpigania apate rufaa ya
serikali ili aweze kupona.
Alisema wataalamu wa afya na hospital zote alizopita
zimemhakikishia kuwa kwa asilimia 98 akipata matibabu atapona. Baada ya
hapo alielekea kwa mzee Kifaru ambae aliwahi kuwa mwenyekiti wa CCM kata ya
Magindu ambae anamjengea nyumba kutokana na kuishi kwenye mazingira
yasiyoridhisha .
"Juzi nimepita hapa kwenye chaguzi za chama nikapita
kumsalimia nikakuta akiwa amefiwa na mkewe na kumkuta anaishi kwenye mazingira
magumu, Imenisikitisha nikaona ni vyema nimsaidie kumjengea nyumba ya
kuishi na ukizingatia umri wake huu hawezi kujishughulisha wala kujenga nyumba,
mimi kama mbunge nimemsaidia" alisema Jumaa.
Kwa upande wake, mzee Kifaru, alisema 1977 alichaguliwa kuwa
kiongozi katika kata hiyo hivyo ni kada wa CCM na muasisi. Alisema
,wabunge wengi wamepita lakini kumpata Hamoud Jumaa anamshukuru kwa msaada
aliompa.
"Mungu amjalie
katika kazi zake, mnajua alinikuta hata mtu akipita nje alikuwa anaona kitanda
ndani, madongo yamedondoka ndipo alipoguswa kunisaidia " alisema mzee
Kifaru.
Mzee Kifaru ,alimsihi
mbunge huyo aendelee na juhudi na kuchapa kazi kwake bila kuchoka ili kuweza
kulisogeza kimaendeleo na kiuchumi jimbo hilo.
No comments:
Post a Comment