Thursday, August 10, 2017

KATIBU WA CCM MKOA WA DODOMA AHIMIZA UMOJA,UPENDO NA USHIRIKIANO KATIKA KUITEKELEZA ILANI YA UCHAGUZI YA CCM.

PICHA (1)
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Deogratius Ndejembi akizungumza na viongozi wa Chama na Serikali wa Tarafa ya Nzoisa wilayani humo katika semina ya kujenga uelewa wa namna ya kutekeleza majukumu yao kwa pamoja.
PICHA (2)
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)mkoa wa Dodoma Jamila Yusuph akifungua semina hiyo kwa viongozi wa chama na serikali ngazi ya Tarafa ambapo amesisitiza ushirikiano,upendo na umoja katika kuitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM iliyopo.
PICHA (3)
Baadhi ya viongozi wa Chama na Serikali wa Tarafa ya Nzoisa walioshiriki semina hiyo.
PICHA (4)
Katibu wa CCM mkoa wa Dodoma akiongoza viongozi wa Chama na Serikali wa wilaya ya Kongwa kuimba wimbo wa Chama katika semina hiyo,miongoni mwa viongozi hao yupo mkuu wa wilaya hiyo Deogratius Ndejembi,katibu wa CCM wilaya Mfaume Kizigo na mwenyekiti wa halmashauri White Zubeir.
…………………
Chama Cha Mapinduzi(CCM)wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma kimewakutanisha viongozi wa serikali na wa Chama ngazi ya Tarafa katika semina ya siku moja lengo likiwa ni kuwapa uelewa wa pamoja wakati wa  kutekeleza majukumu yao ya kazi.
Akifungua semina hiyo katika kata ya Nzoisa wilayani Kongwa Katibu CCM mkoa wa Dodoma Jamila Yusuph  amewataka viongozi hao kufanya kazi kwa pamoja ili kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho kama ilivyoahidiwa.

Ili hilo litekelezeke amewaasa kujenga umoja na maelewano katika sehemu zao za kazi kwa kuelezana ukweli pale wanapoona kuna jambo haliendi sawa na kutatua kero za wananchi kama walivyoahidi.

Alisema viongozi wa Chama na Serikali wakiwa tofauti ilhali kazi ya kupeleka maendeleo kwa wananchi kutokana na Ilani iliyopo inapaswa kufanya kwa ushirikiano wanakuwa wanawakosea wananchi walioichagua CCM na kuiweka madarakani.

“Huwezi leo mtendaji wa kijiji au Kata unataka kukutana na wananchi lakini mwenyekiti wa CCM Kata au tawi hajui chochote,hujamshirikisha hapo tegemea mkutano wako kutofanikiwa maana Chama ndio kinakuwa na wananchi wakati wote na kina ushawishi,”alisema Jamila.

Aliwataka kufanya kazi kwa bidii ili yale anayoyafanya rais John  Magufuli yaweze kuonekana mpaka nchini kwa kuitekeleza Ilani kwa vitendo,kutatua kero na changamoto za wananchi,kutii sheria za nchi,kukemea kwa vitendo suala la rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.

Akizungumzia kuhusu uchaguzi ndani ya chama uliomalizika katika ngazi ya Kata amewataka wote walioshinda kuwaunganisha wana CCM popote walipo na waimarishe matawi na mashina.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kongwa Deo Ndejembi akizungumza katika kikao hicho aliwahimiza viongozi wa serikali kuitekeleza Ilani iliyopo na viongozi wa Chama wawasimamie ili kuhakikisha viongozi hao wanatimiza wajibu wao katika kutekeleza kile kilichoahidiwa kwa wananchi.

“Mwenyekiti wa Kata au Tawi lazima uulize lini mara ya mwisho kusomwa mapato na matumizi,lazima ujue mkutano umefanyika lini,bila ya kutatua kero za wananchi watanung’unika,watakuwa na nyongo na nyongo hiyo kuitema wataitema kwenye karatasi wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa 2020,

“Kuna watu wanasema mimi ni mkali,lakini jamani mfano wewe afisa elimu Kata,kuna mwalimu yupo mjini siku zote lakini hujui kama anafundisha,wananchi wanakereka na hali hiyo maana watoto wao hawafundishwi sasa nikae kimya?nikiuliza useme mi ni mkali?kwa kweli niiteni tu mkali lakini siwezi kukaa kuona mambo hayaendi halafu nikawa kimya,lazima kila kiongozi atekeleze wajibu wake na Ilani,”alisisitiza Ndejembi.

Naye katibu wa CCM wilaya ya Kongwa Mfaume Kizigo alisema lengo la kuwakutanisha pamoja viongozi hao ni kuhakikisha wanajenga nyumba ya CCM pamoja,kuepuka migogoro kati yao baada ya kila mtu kujua mipaka yake ya kazi na wanatarajia kuitoa katika tarafa zote zilizobaki ndani ya wilaya hiyo.

No comments: