Wednesday, August 9, 2017

KATIBU MKUU NKINGA AWATAKA WADAU KUTOA MAONI YA UBORESHAJI WA SERA YA MAENDELEO YA WANAWAKE NA JINSIA TANZANIA

 Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi Sihaba Nkinga (katikati) akifungua kikao kazi cha wadau (hawapo pichani) waliokuta kutathmini Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia kilichofanyika katika ukumbi wa jengo la Wizara Magogoni Jijini Dar es salaam leo 9 Agosti, 2017 kulia  ni Mkurugenzi wa Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali Bw. Marcel Katemba (kulia) na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia Bw. Julius Mbilinyi.
  Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia Bw. Julius Mbilinyi (aliyesimama) akibainisha malengo ya kikao cha wadau (hawapo pichani) wanaokutana kutathmini Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia katika ukumbi wa Ofisi ndogo za Wizara ulioko Magogoni Jijini Dar es salaam leo 9 Agosti, 2017 Kulia ni Katibu Mkuu Sihaba Nkinga.
 Mtaalam mwelekezi anayeongoza kazi ya kutathmini Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia Prof. Linah Mhando, akiwasilisha rasimu ya awali ya taarifa ya mapitio ya Sera hiyo katika kikao cha wadau (hawapo pichani) kinachofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ulioko Magogoni Jijini Dar es salaam leo 9 Agosti, 2017.
Baadhi ya wadau wanaoshiriki kikao kazi cha kutathmini Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia kutoka taasisi mbalimbali wakifuatilia mada mbaimbali katika kikao kinachofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ulioko Magogoni Jijini Dar es salaam leo 9 Agosti, 2017.
Picha na Erasto Ching’oro WAMJW

Na Erasto Ching’oro- WAMJW
Katika kuhakikisha Taifa linakuwa na Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ambayo ni shirikishi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeandaa kikao kazi kwa ajili ya kukusanya maoni zaidi yatakayosaidia kuhuisha sera hiyo.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bibi Sihaba Nkinga mara baada ya kikao na wadau kutoka taasisi mbalimbali katika mwendelezo wa mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya ambayo yatasaidia kubaini mapungufu, na changamoto zilizopo katika Sera iliyopo na hivyo kusaidia uboreshaji wa Sera hiyo kwa kuzingatia mahitaji ya kijinsia kwa ajili ya maendeleo ya wanawake, wanaume, wavulana wasichana na watoto.

“Sera iliyopo ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000 imechukua muda mrefu kufanyiwa tahmini kutokana na ukweli kuwa zoezi la tathmini linahitaji muda wa kutosha sanjari na uhakikika wa upatikanaji wa rasimali fedha kufanikisha kazi hii” alisema Bibi Sihaba.

Kwa upande wake Msauri Mwelekezi Profesa Linda Muhando aliipongeza Wizara kwa kuridhia mchakato wa kutathmini sera hiyo na kujumuisha wadau hatua amabyo itasaidia kupata mchango wa wananchi wengi zaidi na kuwezesha kupata masuala mapya amabyo hayako kwenye sera hiyo na kuyajumuisha katika rasimu ya sera inayofanyiwa mapitio.

Kikao kazi cha tathmini ya Sera hiyo kinatoa fursa kwa wadau kuibua changamoto, mapungufu yaliyopo na kuimarisha uzingatiaji wa mahitaji ya wanawake na wanaume ili kutoa fursa sawa ya upatikani haki na usawa kwa watu wote.



Maandalizi ya uboreshaji wa Sera hii utajumuisha usambazaji wa sera kwa wananchi, kutoa elimu kwa umma ili kufahamu mwongozo wa kisera, na kuiweka katika lugha nyepesi ili kujenga ufahamu wa wananchi katika wigo mpana zaidi. Aidha, ukusanyaji wa maoni ya wadau utasaidia kupanua ushirikishaji wa wananchi katika kuandaa sera na kufanikisha utekelezaji wake kwa kuzingatia wakati.

No comments: