Na Jumbe Ismailly IRAMBA
HALMASHAURI ya wilaya ya Iramba,Mkoani Singida imeshindwa kutekeleza agizo la kamati ya kudumu ya Bunge la kutenga asilimia kumi kutoka kwenye mapato yake ya ndani kwa ajili ya vikundi vya wanawake pamoja na vijana katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha wa 2012/2013 hadi 2014/2015.
Kaimu Mweka Hazina wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba,CARROLINE DALULI aliyasema hayo kwenye taarifa aliyotoa kwenye mkutano wa Baraza maalumu la madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo lilipokutana kujadili hoja za Ukaguzi na Mpangokazi wa utekelezaji wa maoni yaliyotolewa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za serikali (CAG) kwa mwaka 2015/2016.
“Kamati iliagiza Halmashauri kuchangia asilimia kumi kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya wanawake na vijana kwa miaka hiyo iliyotajwa na kiasi kilichoonekana”alifafanua kaimu Mweka Hazina huyo.
Kwa mujibu wa Kaimu Mweka hazina huyo kwa mwaka 2012/2013,2013/2014 na 2014/2015 Halmashauri ya wilaya ya Iramba haijatekeleza agizo la kamati ya kudumu ya Bunge kwani hakuna fedha yeyote ile iliyotengwa na iliyopelekwa kwenye vikundi hivyo.
Aidha Daluli aliweka bayana pia kwamba kwa mwaka 2016/2017 Halmashauri hiyo imechangia shilingi milioni mbili,zikiwemo shilingi milioni moja kwa Mazega Kisimba na shilingi zingine milioni moja kwa kikundi cha Maendeleo Shelui na itaendelea kuchangia kadri fedha zitakapopatikana.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Huduma za jamii wa Halmashauri hiyo,Hamisi Kinota akichangia hoja hiyo ya michango ya vikundi vya wanawake na vijana alisisitiza kwamba kutokana na uchangiaji wa Halmashauri hiyo unadhihirisha wazi kwamba Halmashauri haitaweze kuchangia michango hiyo kwa asilimia mia moja.
Hata hivyo Kinota huku akionyesha hofu ya utekelezaji wa agizo hilo la kamati ya kudumu ya Bunge alibainisha kuwa katika kipindi cha mwaka 2012/2013,2013/2014 na 2014/2015 kati ya shilingi milioni 109,819,388 zilizotarajiwa kutumika,ni shilingi milioni mbili tu ndizo zilizotolewa na hivyo kubakiza zaidi ya shilingi milioni 107,hali ambayo inaonyesha hakuna uwezekano kwa Halmashauri hiyo kumaliza deni hilo kwa asilimia mia moja.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida,Dk.Rehema Nchimbi alishauri kwamba njia pekee ya kumaliza deni hilo la michango ya vikundi vya wanawake na vijana ni kuandika maandiko mbali mbali na kusambaza kwa wafadhili na kudai kwamba kuna watu wenye fedha walio tayari kuwasaidia wanawake na vijana.
“Mtakapopata hizo fedha najua mnaweza kupata hata zaidi ya shilingi milioni mia mbili,mtakapopata hizo fedha mtaaandika kwamba ni fedha ambazo ninyi wenyewe Halmashauri mmezitafuta kwa hiyo itakuwa ni sehemu ya mapato yenu na mtazipeleka kwa wanawake na vijana”alisisitiza Dk.Nchimbi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida,Dk.Rehema Nchimbi akimkabidhi mmoja wa madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba cheti cha mafunzo ya udiwani aliyopata na ambayo yatawawezesha madiwani wote kutambua majukumu pamoja na mipaka yao ya kazi.(Picha zote Na Jumbe Ismailly).
Mkuu wa Mkoa wa Singida,Dk.Rehema Nchimbi akisisitiza juu ya maafisa watendaji wa vijiji 30 walioiba fedha za chakula cha njaa kuhakikisha wanazirejesha ifikapo aug,30,mwaka huu na kupendekeza njia rahisi ya fedha hizo kurejeshwa kuwa ni kuanzishwa kwa Mahakama tembezi itakayomtembelea kila mdaiwa na kuuza mali alizonazo ili kulipia deni la chakula hicho cha njaa walizokula.
No comments:
Post a Comment