Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, akiongea na Baraza la Wawakilishi la Kamati ya Ardhi na Mawasiliano kutoka Zanzibar na uongozi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), (hawapo pichani), wakati wa ziara ya kikazi ya Kamati hiyo, jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi na Mawasiliano kutoka Zanzibar, Mhe. Hamza Hassan Juma, akizungumza na wajumbe na watendaji, katika ziara ya kikazi kwenye Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) Eng. Ladislaus Matindi (katikati) akifafanua jambo kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Kamati ya Ardhi na Mawasiliano kutoka Zanzibar, wakati wa ziara ya kikazi kwenye Shirika hilo, jijini Dar es Salaam.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Kamati ya Ardhi na Mawasiliano kutoka Zanzibar wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani (hayupo pichani), wakati wa ziara ya kikazi katika Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi kavu na Majini (SUMATRA), Gilliard Ngewe, akifafanua jambo kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Kamati ya Ardhi na Mawasiliano kutoka Zanzibar wakati wa ziara ya kikazi katika Mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam.
…………………………………………………………….
Serikali imesema kuwa Shirika la Ndege nchini (ATCL), litaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha inaboresha huduma za usafiri wa anga katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Akizungumza katika kikao kilichokutanisha Baraza la Waakilishi la Kamati ya Mawasiliano na Ardhi kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na uongozi wa Shirika hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani, amesisitiza kuwa changamoto ambazo wameziwasilisha katika kikao hicho zitafanyiwa kazi ili kuleta tija kwa pande zote mbili.
“Nawahakikishia wajumbe wa kamati hii kuwa changamoto mlizonazo tutazifanyia kazi haraka kwani ATCL sasa imezaliwa upya na hivyo itahakikisha inaboresha maslahi ya kuliinua na kuliendeleza shirika ili kuweza kukidhi mahitaji ya hapa na visiwani”, amesema Naibu Waziri Ngonyani.
Aidha, Mhandisi Ngonyani ameongeza kuwa katika kuhakikisha huduma za usafiri wa anga visiwani humo zinaimarika, tayari Serikali imeshaanza kulipa deni lililokuwa linadaiwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege la shilingi milioni 241 ambalo shirika hilo linadaiwa kutokana na tozo ya maegesho ya ndege na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hamza Juma, amemwomba Naibu Waziri Mhandisi Ngonyani kuangalia upya suala la ajira katika Shirika la ATCL ili liweze kubeba sura ya Muungano na kuwawezesha wataalam wenye sifa kutoka Zanzibar nao kupata nafasi hizo.
“Tunaomba Shirika na baadhi ya Taasisi zinazofanya kazi kwa kushabihiana na masuala ya Muungano kuzingatia utoaji wa ajira katika nafasi wanazozitangaza kwani Zanzibar ina wataalam wenye sifa lakini hawapati fursa” amesisitiza Mwenyekiti wa Kamati.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Mhandisi Emmanuel Korosso, amesema kuwa Shirika hilo linaendelea kuimarika na kusambaza huduma katika viwanja mbalimbali vya ndege nchini licha ya kuwa na changamoto za uhaba wa marubani.
Katika hatua nyingine, Kamati hiyo imetembelea Makao Makuu ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi kavu na Majini (SUMATRA) na kupendekeza kwa Mamlaka hiyo kutoa kipaumbele katika suala la ajira na vibali kwa mabaharia kutoka Zanzibar ambao wamesajiliwa chini ya Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar (ZMA), kufanyika kwa wakati.
Ziara ya kamati hiyo imelenga kutatua, kupunguza na hatimaye kumaliza kero za Muungano ambazo zinagusa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
No comments:
Post a Comment