Tuesday, July 11, 2017

Wawili kizimbani kwa kuingilia mawasiliano nchini ma kuisababishia TCRA hasara ya 210.2m

Na Karama Kenyunko blog ya jamii.

RAIA wa Uganda, Edwin Gusongoirye (30) na Mfanyabiashara, Steven Simon (45) wamepandishwa katika kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi kwa kuisababishia serikali hasara ya Sh milioni 210.2.

Gusongoirye ambaye ni mfamasia pamoja na Simoni wamesomewa mashitaka yao sita  mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa.

Hati ya mashitaka hayo, imsomwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Nassoro Katuga na kudai kuwa kati ya Machi 6 na Juni 22, mwaka huu jijini Dar es Salaam, washitakiwa walitengeneza mfumo wa kutumia huduma za mtandao kwa lengo la kukwepa kodi ya kupokea na kusambaza mawasiliano bila kuwa na kibali kutoka TCRA

Imedaiwa kuwa kati ya Machi 6 na Juni 22, 2016, washitakiwa hao kwa pamoja waliendesha mfumo wa kupokea na kusambaza mawasiliano ya Kimataifa bila kuwa na leseni ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Katika shtaka la tatu kuwa, imedaiwa kuwa,  Gusongoirye na Simon waliingiza vifaa vya mawasiliano nchini ambavyo ni maboksi matatu ya simu bila kuwa na kibali cha TCRA.

Aidha, washtakiwa hao wanadaiwa, kabla ya Machi, 2012 jijini Dar es Salaam, walisimika vifaa mbalimbali vya mawasiliano zikiwemo kompyuta mpakato mbili aina ya Dell na Hp bila kibali.

Pia washitakiwa wanadaiwa kutumia vifaa vya mawasiliano ambavyo havijathibitishwa kwa lengo la kupokea na kusambaza viashiria vya mawasiliano bila kuthibitishwa na TCRA.

Machi 6 na Juni 22, mwaka huu, kwa makusudi na washitakiwa kwa pamoja waliisababishia serikali hasara ya Sh milioni 210.2.

Washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi na kwamba mahakama hiyo haiwezi kutoa dhamana kwani mashitaka hayo ni zaidi ya Sh milioni 10 ambayo wanatakiwa kuomba Mahakama Kuu.

Imedaiwa,  upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 25, mwaka huu kwa kutajwa.

  Watuhumiwa, Steven Simon, aliyetangulia mbele na Edwin Gusongoirye, raia wa Uganda, wakipelekwa mahakamani kusomewa kesi yao ya uhujumu uchumi. 

No comments: