Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngoyani ametoa Miezi sita kwa
wakazi wa Mpanda Mkoani Katavi kuondoka katika maeneo ya hifadhi za Reli ili
kupisha maboresho yanayoendelea kufanywa na Shirika la Reli Tanzania (TRL)
kwenye miundombinu yake.
Ametoa agizo hilo
wakati akiongea na wafanyakazi wa taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo Mkoani
Mpanda na kusema ni wakati sasa kwa wananchi kufuata sheria kwa kutovamia
miundombinu hiyo.
“Ninatoa miezi sita
kuanzia sasa, itakapofika Mwezi Januari mwakani wananchi wote watakaokuwa ndani
ya hifadhi ya reli watabomolewa nyumba zao kwa kuzingatia sheria zinazolinda
miundombinu,” alisisitiza Eng. Ngonyani.
Naibu Waziri Eng.
Ngonyani ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Mpanda kusimamia zoezi la wananchi kuhama
na kuhakikisha kila aliyevamia miundombinu hiyo anabomoa nyumba yake kabla ya
sheria kufata mkondo wake.
Aidha, Eng. Ngonyani
amewatahadharisha wafanyakazi wa Wakala wa barabara nchini (TANROADS)
kuzingatia maslahi mapana ya Taifa wakati wa kutafuta zabuni kwa kufanya hivyo
watakuwa wanamuunga Mkono Mhe. Rais Dkt. John Magufuli.
Katika hatua nyingine
Eng. Ngonyani amekagua barabara ya Kanazi-Kizi-Kibaoni (76.6KM),
Sumbawanga-Kanazi (75KM) ambapo ameiagiza TANROADS Mkoa wa Rukwa kuweka mizani
katika barabara zinazojengwa ili kudhibiti magari makubwa yanayozidisha uzito
na kusababisha uharibifu kwa barabara katika Mkoa huo.
“Ni wakati sasa
wanaotoa huduma za usafirishaji wa mizigo kufuata sheria na kubeba mzigo wa uzito unaostahili
sababu madereva hao hao wakienda nchi za jirani wanafuata sheria kwa umakini,
SUMATRA simamieni utoaji wa leseni kwa magari ya abiria na mizigo kwa
kuzingatia uzito wa magari ili kuziweshesha barabara zetu zidumu,” alisisitiza
Eng. Ngonyani.
Kwa upande wa Meneja
wa TANROADS Mkoa wa Rukwa, Eng. Msuka Mkina amemuhakikishia Naibu Waziri kuwa Wakala
utahakikisha Mizani inawekwa sehemu za barabara ili kubaini Magari yanayozidisha uzito na
kuyachukulia hatua za kisheria.
Naibu Waziri Eng.
Ngonyani yupo katika Ziara ya kukagua Miundombinu ya barabara, Viwanja vya
Ndege, Ujenzi wa Nyumba za viongozi, huduma za mawasiliano ya simu na Madaraja katika Mkoa wa Katavi na Rukwa.
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani akitoa maelekezo
kwa Meneja wa Kampuni ya Simu (TTCL) mkoa wa Rukwa na Katavi Bw. Peter Kuguru wakati
alipokagua eneo ambalo Mkongo wa Taifa umeharibika kwa kuliwa na panya Wilayani
Nkasi Mkoani Rukwa.
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani (Katikati)
akiangalia ramani ya Mkongo wa Taifa wakati alipokagua eneo ambalo Mkongo wa
Taifa umeharibika kwa kuliwa na panya Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa.
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani (Kulia) akitoa
maelekezo kwa Mkandarasi anayejenga barabara ya Kanazi-Kizi-Kibaoni (76.6KM)
Wakati alipokagua ujenzi wa barabara hiyo kwa
kiwango cha lami.
Meneja
wa Kampuni ya Simu (TTCL) mkoa wa Rukwa na Katavi Bw. Bw. Peter Kuguru (aliyenyoosha
kidole) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Eng. Edwin Ngonyani wakati alipokagua eneo ambalo Mkongo wa Taifa umeharibika
kwa kumegwa na panya Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa.
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani (Kulia) akipokea
maelezo ya kifaa maalumu cha kugundua sehemu ambayo mkongo wa Taifa una tatizo
kutoka kwa Bw. Juma Ngimba (Kulia), wakati alipokagua eneo ambalo Mkongo wa
Taifa umeharibika kwa kuliwa na panya Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa.
Muonekano
wa barabara ya Kanazi-Kizi-Kibaoni (76.6KM), ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha
lami umekamilika.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment