Monday, July 10, 2017

WALIOKULA FEDHA ZA USHIRIKA WATAZILIPA-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitahusika na ulipaji wa deni la fedha za Ushirika na badala yake kila aliyekula fedha hizo atazilipa mwenyewe.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Julai 10, 2017), wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Liwale katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa wilaya.

Waziri Mkuu ambaye yuko katika na ziara ya kikazi ya siku nne Mkoani Lindi, amesema Serikali haiwezi kukubali Ushirika ukafa nchini kwa ajili ya watu wachache wasiokuwa waaminifu.

Amesema watu wote waliopewa dhamana ya kuongoza Vyama vya Ushirika na kuamua kujinufaisha kwa kula fedha za vyama watazilipa.

Waziri Mkuu amewaagiza Viongozi wa Mkoa wa Lindi kufanya ukaguzi katika Vyama vyote vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) ili kubaini ni wakulima wangapi wanadai.

Amesema baada ya kufanya uchunguzi na kubaini idadi ya wakulima wanaodai na kiasi cha fedha wawachukulie hatua wahusika wote kwa mujibu wa sheria.

Awali, Waziri Mkuu alizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale katika Ukumbi wa Tengeneza, ambapo amewataka Watumishi wa Umma Nchini kutojihusisha na vitendo vya rushwa katika utoaji wa huduma kwa Wananchi.

Amesema Watumishi wanawajibu wa kuwahudumia Wananchi bila ya kutengeneza mazingira ya kuomba rushwa na atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Amesema Watumishi wa Umma wanatakiwa kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia maadili ya kiutumishi jambo litakaloondoa malalamiko kutoka kwa Wananchi.

“Lazima Wananchi waone na wanufaike na kazi inayofanywa na Serikali yao, hivyo ni wajibu wa Watumishi kuwatumikia Wananchi popote walipo na si kukaa maofisini.”

Pia amewataka Watumishi hao kupanga mipango itakayoleta tija kwa Wananchi na si vinginevyo.



IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU, JUMATATU, JULAI 10, 2017

No comments: