Thursday, July 27, 2017

Wakati wabunge nane wa CUF waliovuliwa uanachama watinga mahakamani

Wakati wabunge nane wa CUF waliovuliwa uanachama na kuvuliwa ubunge wao wametinga leo mahakama ya Kisutu jijini Dar es salaam kupinga hatua hiyo.
 Mwenyekiti wa kamati ya uongozi wa chama hicho anayetambuliwa na upande wa katibu mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamadi, ndugu Julius Mtatiro, amelaani kitendo cha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai kubariki kufukuzwa uwanachama wabunge 8 wa viti maalum wa chama hicho kwa kile kilichoitwa kutokutii wito wa uongozi wa chama hicho unaotambuliwa na msajili wa vyama 
Mtatiro ameyasema hayo jana baada ya ofisi ya spika kutoa taarifa kwa uma juu ya hatua ambazo zimechukuliwa na uongozi wa chama cha CUF chini ya mwenyekiti wake anayetambuliwa na msajili w vyama vya siasa Prof Ibrahimu Lipumba.
 Akieleza kwa masikitiko makubwa Mtatiro amesema Jumatatu Lipumba na Sakaya walimuandikia Spika wa Bunge kumjulisha kuwa “Baraza Kuu la CUF” limewafukuza uanachama Wabunge 8 wa Viti Maalum wa CUF kitu ambacho ni kinyume na taratibu za chama cha Cuf kwa sababu katibu mkuu wa Cuf Maalim Seif alishamwandikia Spika Ndugai kumjulisha kuwa baraza kuu halali la CUF ni lile lililochaguliwa mwaka 2014 kwenye mkutano mkuu wa chama hicho.
Jumanne ya wiki hii Ofisi ya Bunge ilitoa taarifa kwa umma kuujulisha kuwa imepokea maelekezo kutoka kwa Sakaya na Lipumba kuwa wabunge hao 8 si wanachama na Ofisi hiyo ikaeleza kuwa bado inatafakari hatua za mwisho za kuchukua.
Jana Jumatano, Ofisi ya Bunge imetangaza uamuzi wake, kwamba inakubaliana na uamuzi wa CUF ya Lipumba na Sakaya na kuwa imewavua wabunge hao 8 ubunge wao wa Viti Maalum, na kuwa imeiandikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuijulisha kujaza nafasi hizo zilizo wazi. 
“Nataka kuwaeleza wanachama na watanzania wote, kwamba viongozi wa chama wanakutana kuendelea kuchukua hatua. 
"Tunajua kuwa vyombo vya Serikali hivi sasa vinafanya kazi kubwa kuhakikisha kuwa aidha CUF inamkubali “MSALITI” Lipumba kuwa Mwenyekiti wake, au CUF isambaratike. Na suluhisho la hali hii haliwezi kuwa kukaa chini na MSALITI.”alisema Julius Mtatiro 
Mtatiro amewatahadharisha wanachama wenzake kuwa wanapopambana na wasaliti waliokubuhu na wako ndani ya nyumba yao, vita yake siyo ndogo lakini amewataka wasimame imara kwa sababu anaamimi kuwa CUF itavuka misukosuko hii. 
"Kwa jicho moja wapo watu wanachekelea na kudhani kadhia hii ni ya CUF tu, mimi natizama hali hii kama Mapambano ya Dola ya kuhakikisha vyama mbadala vinaongozwa na wasaliti ili Dola iendelee kuwatumia kuzamisha demokrasia ushindani wa kisiasa nchini,amesisitiza Mtatiro ambaye kwa sasa yuko masomoni nchini Marekani. 
Mtatiro amesema dola ikifanikiwa kuisambaratisha CUF, vyama vingine vya upinzani havitakuwa salama, taasisi zingine za kiraia hazitakuwa salama pia. Mtatiro ameongeza kuwa mtu anayeyatizama mapambano haya kama vita ya ndani ya CUF hajaisoma dunia.
Haya ni mapambano makubwa, dhidi ya demokrasia ya Tanzania,amesisitiza Mtatiro akisema yeye ni mwanademokrasia imara na hatayumbishwa na Wasaliti, na kwamba CUF kumkubali Lipumba na genge lake itakuwa na maana ya kuiua CUF moja kwa moja Tanzania Bara, maana alipojaribu kukimbia mwaka 2015, ndipo Cuf iliibuka na kuwa chama imara mara 10 Tanzania bara,na kurudishwa kwake kwa nguvu kunakofanywa na dola ni mkakati wa kuimaliza Cuf na suluhisho lake haliwezi kuwa CUF kumtambua Lipumba. 
Mtatiro ameweka wazi kuwa hata dola ikifanya nini, Lipumba ameshadharaulika na hawezi kuisaidia tena dola hii yenye upofu.

No comments: