Sunday, July 16, 2017

Wahitimu waliosoma China waombwa kuisaidia Tanzania katika uchumi wa viwandaWAZIRI wa Mambo ya Nje, Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Balozi Augustine Mahiga amesema wanafunzi wahitimu kutoka vyo vya nje ya nchi waunde umoja wa mataifa waliyotoka ili kuwa na jukwaa la kuvuna wataalamu pamoja na wao kutambuana.

Alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizindua Chama cha wanafunzi waliosoma China (CAAT), jijini hapa ambapo alibainisha vyama vingi vya aina hiyo vimeanzishwa na kupotea kutokana na kukosa msukumo kutoka serikalini.
“Nyinyi mtakua kiungo kati ya wasomi kutoka China, serikali na jamii, hiki ni chama cha kwanza cha wanafunzi waliosoma  China. Matarajio yangu ari iliyowafanya kujipanga pamoja itabaki daima na naamini chama hiki kitakua jukwaa la wanafunzi wanaoendelea kusoma na waliohitimu,” alisema Balozi Mahiga.
Aliongeza kuwa: “Najua kuna Wachina nchini walioanzisha viwanda na wangependa kupata vijana wasomi, hii ni fursa pekee ya kuendeleza sekta binafsi na kudumisha urafiki wetu. Ningeshauri idara za serikali na sekta binafsi kuwa karibu na chama hiki.
“Nimezungumza nao na nimeona aina ya utaalamu waliokuwa nao, utaalamu huu utasaidia kuleta tija kwa idara mbalimbali na wizara pamoja na taasisi za umma. Nitaangalia namna wizara yangu itakavyokisaidia chama hiki ili tusiwaache peke yao ubunifu waliofanya ni wa ahali ya juu kabisa.”
Balozi  msaidizi wa China nchini, Bw.

Gao Haodong alisema wnafunzi hao wameonyesha mfano mzuri wa kuleta maendeleo katika taifa linalokua kwa kasi kiuchumi kwa sababu hata China ilikuwa na utaratibu kama huo katika miaka yao ya mwanzo ya kukua.
“Cama hiki kinakumbusha chama cha umoja wa Wachina waliosoma ughaibuni katika miaka ya 1950, wanafunzi waliotoka Ulaya na Marekani wanaaminika kuwa sehemu ya watu waliochochea mabadiliko ya kiuchumi China. Wakati huo China ilikuwa chini kimaendeleo kuliko Tanzania ya sasa.
“Historia ya China haitofautiani na mataifa mengine ya Afrika, naamini hata Tanzania inaweza kukua. Naamini ambacho kimefanywa na China hapa Tanzania kinaweza kufanyika zaidi ya tulichofanya. Nasema haya kutoka ndani ya moyo wangu kuwa tuna mengi ya kujifunza kutoka kwa marafiki wetu wa Tanzania,” alisema Bw.Gao.
Akizungumzia kuhusu hali anayoiona nchini akilinganisha na taifa lake Bw.Gao.
alisema: “Nimejifunza mambo mengi kupitia hotuba za Mwalimu Julius Nyerere. Alikuwa ni mtu mwenye maono na fikra pevu. Ingawa China ni taifa la pili kwa ukubwa duniani lakini haijafanikiwa kuwaweka watu wake pamoja, tazama Tanzania inavyoishi kwa pamoja na kuelewana katika amani na utulivu hasa suala la kuondoa ukabila.”
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama hicho cha wanafunzi waliomaliza masomo China, Dkt.Liggy Vumilia alisema katika umoja huo kuna wataalamu mbalimbali ambao wakitumiwa vizuri wanaweza kuleta tija na kusaidia azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kuwa na uchumi wa kati kupitia viwanda.
“Tuna uwezo mkubwa wa kufanya kazi na kampuni za kichina zilizopo nchini kwa sababu tunajua namna wanavyoishi na aina ya watendaji wanaotaka. Vilevile tunao uwezo wa kuisaidia serikali kufikia Tanzania ya viwanda ambapo China wamekuwa rafiki wa asili. Sisi tuliopata bahati ya kwenda kusoma china tuna nafasi kubwa katika kuimarisha umoja huu.
“Kwa kutumia utaratibu huu wa kuwasomesha Watanzania China kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuleta maendeleo nchini, mataifa mengi yaliyoendelea yamefanikiwa kutokana na vyama hivi vya Alumni kwa sababu ni eneo lililo na wataalamu wanaojulikana walipo.”alisema Dkt.Vumilia.

No comments: