Saturday, July 15, 2017

VIJIJI 347 KUPATA UMEME WA REA AWAMU YA TATU MKOANI SIMIYU

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.Dkt.Medard Kalemani akizindua Mradi wa Umeme Vijijini (REA)Awamu ya Tatu Mkoani Simiyu katika Kijiji cha Nangale wilayani Itilima (kushoto) Mkuu wa mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka.
Mmoja wa Wazee 10 waliopewa kifaa cha Umeme kiitwacho UMETA katika Kata ya Ndolelezi Wilayani Itilima na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.Dkt.Medard Kalemani akitoa shukrani wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA)Awamu ya Tatu Mkoani Simiyu uliofanyika katika Kijiji cha Nangale wilaya ya Itilima.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.Dkt.Medard Kalemani akizungumza na wannachi wa Wilaya ya Itilima wakati wa Uzinduzi waMradi wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya Tatu Mkoani Simiyu uliofanyika katika Kijiji cha Nangale wilaya ya Itilima.

……………………………………………………………….


Na Stella Kalinga, Simiyu


Jumla ya Vijiji 347 Mkoani Simiyu vinatarajia kupata Umeme kupitia Mradi wa Umeme Vijijini (REA) awamu ya Tatu ambao utatekelezwa katika kipindi cha miezi 24 kuanzia mwezi Julai 2017.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt.Medard Kalemani wakati wa Uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya Tatu na utambulisho wa Mkandarasi wa mradi katika Kijiji cha Nangale, Kata ya Ndolelezi Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu.

“Mradi wa REA awamu ya tatu utapeleka Umeme katika vijiji vyote vya Mkoa wa Simiyu hilo la kwanza, pili mradi huu utapeleka Umeme katika vitongoji vyote hata vijiji ambavyo vilipelekewa Umeme lakini baadhi ya vitongoji vyake bado havina umeme, sasa katika awamu hii navyo vinapelekewa” amesema Kalemani. 

Ameongeza kuwa Umeme wa REA awamu ya tatu pamoja na kuwanufaisha wananchi katika makazi yao kwenye vijiji vyote 347 vilivyosalia pia utapelekwa katika Taasisi za Umma zikiwepo shule, vituo vya kutolea huduma za afya, visima na mitambo ya miradi ya maji pamoja na nyumba za ibada( makanisa na misikiti).

Aidha, Dkt.Kalemani amewataka wananchi wa Mkoa wa Simiyu kuutumia umeme huo kibiashara hususani katika shughuli za uzalishaji ambazo zitawaongezea kipato badala ya kuutumia kwa ajili ya kuwasha taa majumbani tu.

Ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Simyu kwa kasi nzuri ya utekelezaji wa Sera ya Viwanda ambapo amebainisha kuwa utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA) awamu ya Tatu mkoani humo utasaidia kuwezesha shughuli za viwanda kufanyika vizuri hali itakayowawezesha wananchi kukuza uchumi kwa kuwa mazao yao yataongezewa thamani kupitia viwanda hivyo.

Wakati huo huo Dkt.Kalemani amesema Serikali ina mkakati wa kujenga vituo viwili vya kupozea umeme Mkoani Simiyu, ambapo kimoja kitajengwa Mjini Bariadi na kingine katika Mji wa Lalago wilayani Maswa na kuwahakikishia wananchi kuwa mkoa huo utapata umeme wa kutosha ambao utatumika pia katika viwanda.

Akimkabidhi Mkandarasi wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu ambaye ni Kampuni ya JV White City International kwa Wananchi wa Mkoa wa Simiyu, Dkt.Kalemani amemtaka kuhakisha kuwa anatekeleza mradi ndani ya muda uliopangwa (miezi 24), akiwatumia wakandarasi wasaidizi wenye sifa kutoka ndani ya mkoa na kuwapa ujira wao kama inavyotakiwa pamoja na kununua vifaa vyote zikiwemo nguzo na transifoma hapa nchini.

Amemtaka Meneja wa TANESCO Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Rehema Mashinji kusimamia na kuhakikisha kuwa wakandarasi watakaowaunganishia wananchi Umeme ni wale walioidhinishwa na shirika hilo ili kuepuka Vishoka ambao watawaongezea wananchi gharama zisizo za lazima.

Amesema Serikali ina mpango wa kujenga Ofisi za TANESCO kila Wilaya na kuweka vituo vya kuhudumia wateja katika kila kata na tarafa ambapo yataanzishwa madawati ya huduma kwa wateja.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ameomba Shirika la Umeme TANESCO kuona namna ya kuweka nguvu katika Mkoa huo ili ujitosheleze kwa umeme wa uhakika kuwezesha utekelezaji wa miradi ya viwanda inayoendelea kutekelezwa chini ya Kauli Mbiu ya Mkoa ya “Wilaya Moja Bidhaa Moja Kiwanda Kimoja”

Mtaka ameongeza kuwa Mkoa huo umejipanga kufanya mapinduzi kupitia teknolojia ambapo utatengeneza mpango mkakati wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT Strategy),kujenga ICT Hub ya mkoa na vituo vya mawasiliano katika baadhi ya shule, ili wanafunzi wa madarasa ya mitihani waweze kupata unafuu wa kufundishwa kupitia teknolojia hususani kwenye masomo ya sayansi, hivyo akasisitiza umeme kupelekwa katika shule na Taasisi nyingine za Umma.

Naye Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Simiyu kupitia CCM, Mhe.Leah Komanya ametoa Rai kwa TANESCO kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi ili wajue taratibu zote za kuunganishiwa umeme ikiwa ni pamoja kufahamu gharama ambayo ni shilingi elfu 27,000/= ili wasidanganywe na kutumia gharama kubwa kinyume na mpango wa Serikali.

Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa mradi huo Mkazi wa Kijiji cha Nangale Bw.Mathias Mabula Mageni ameishukuru Serikali kuwafikishia umeme kupitia REA ambapo amesema utawasaidia katika kukuza uchumi kwa kuwa watautumia katika shughuli mbalimbali zitakazowaingizia kipato kama vile kuchomelea vyuma, kuanzisha mashine za kusaga na kukoboa nafaka, kuanzisha saluni za kike na za kiume pamoja na viwanda vidogo.

Mradi wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya Tatu Mkoani Simiyu unatekelezwa na Mkandarasi JV White City International Contractors ambalo ni Kampuni ya Kitanzania kwa kushirikiana na Guangdong Jianneng Electronic Power Engineering Co. Ltd.

No comments: