Thursday, July 20, 2017

Tumieni fursa zilizopo kuanzisha viwanda kukuza uchumi

Watanzania wametakiwa kutumia fursa zinazoendelea kuwekwa na serikali ya awamu ya tano kujikita katika ujasiriamali na kuanzisha viwanda kwa ajili ya kujenga uchumi viwanda ili kufikia uchumi kati na kuboresha ustawi wa jamii hapa nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji,Profesa Adolf Mkenda alisema hayo wakati wa mkutano wa wadau uliokuwa ukijadili rasimu ya mapendekezo ya kuwa na mkakati wa kitaifa kuendeleza ujasiriamali hapa nchini, kuwa wakati wa watanzania kujikita katika ujasiriamali na kuwekeza katika viwanda umewadia.

“Wakati wa watanzania kuanzisha viwanda kuzalisha bidhaa zinazotokana na mali ghafi za hapa nchini umewadia,” na hakuna wakati mzuri zaidi kuliko kipindi hiki ambacho serikali imweka kipaumbele zaidi katika hili, aliongeza kusema Profesa Mkenda.

Mkakati huo wa kitaifa wa kuendeleza ujasiriamali umeandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali likiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa Linalojihusisha na Maendeleo ya Biashara (UNCTAD).

Profesa Mkenda alifafanua kwamba serikali imeamua kuja na rasimu hiyo kupata mkakati wa uendelezaji ujasiriamali huku ikitambua uchumi wa Tanzania utajengwa na watanzania na wawekezaji wa nje kuja kuongezea tu.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC),Bi. Beng’I Issa alisema Baraza lake linasimamia sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi na suala la uasiriamali ni nguzo muhimu katika uwezeshaji wananchi.

“Pendekezo la mkakati huu wa kuendeleza ujasirimali umeandaliwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na leo ni siku ya pekee kwa wataalaam kutoa maoni yenu ili kupata mkakati wa kitaifa,” na aliwaomba watalaamu hao kutoa maoni yao kukamilisha upatakanaji wake, alisema, Bi. Issa 

  Alisema jukumu la kuaandaa mkakati wa kitaifa wa kuongoza ujasiriamali kufikia uchumi wa kati na wa viwanda ni muhimu kwa vile utawezesha kupata wajasiriamali wenye mafanikio walioongozwa vyema.

Alisema uandaaji wa rasimu hiyo umeangalia mapungufu yaliyopo katika nchi na umekuja na majibu ambayo ni rafiki kwa wajasiriamali.

Alisema hadi kufikia Agosti mwezi ujao maoni yote ya wadau yatakuwa yameingizwa na matarajio yaliyopo ni kwamba mkakati huo utaweza kuwa tayari Octoba 2017 kwa ajili ya kuendeleza ujasiriamali.

Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa Linalojihusisha na Maendeleo ya Biashara (UNCTAD),Bw. Lorenzo Tosini alisema shirika hilo limeweka suala la uendelezaji ujasirimali katika ajenda kuu na Tanzania inapofanya hivyo inaendana na ajenda hiyo.

“Katika kukuza ujasiriamali kuna changamoto mbalimbali ambazo nchi nyingi za Afrika zinakabiliana nazo na kuwepo kwa mkakati huo nchini Tanzania itasaidia katika hili,” na kuongeza mkakati huo pia usaidie kuja na sera inayoleta usawa kwa wajasiriamali.

Alisema vikwazo vikuu katika mataifa haya katika ujasiriamali na biashara ni pamoja na vikwazo vya kisheria, upatakanaji wa mitaji kutoka taasisi za kiedha, na uhafifu wa teknolojia na mawasiliano .
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji,Profesa Adolf Mkenda (katikati) akifuatilia mada iliyokuwa inatolewa na Mwezeshaji, Dkt Donath Olomi hayupo pichani wakati wa mkutano wa wadau uliokuwa ukijadili rasimu ya mapendekezo ya kuwa na mkakati wa kitaifa kuendeleza ujasiriamali hapa nchini, wapili kushoto Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC),Bi. Beng’I Issa, kushoto ni Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa Linalojihusisha na Maendeleo ya Biashara (UNCTAD),Bw. Lorenzo Tosini, wa pili kuli ni Mkurugenzi Msaidizi Mazingira ya Biashara Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Christopher Mramba na kulia ni Mkurugenzi wa Uwezeshaji wa baraza hilo, Bi. Anna Dominick.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji,Profesa Adolf Mkenda (katikati) akiteta jambo na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC),Bi. Beng’I Issa, wakati wa mkutano wa wadau uliokuwa ukijadili rasimu ya mapendekezo ya kuwa na mkakati wa kitaifa kuendeleza ujasiriamali hapa nchini, na kulia ni Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa Linalojihusisha na Maendeleo ya Biashara (UNCTAD),Bw. Lorenzo Tosini.


Wadau kutoka taasisi mbalimbali wakiwa katika makundi wakati wa mkutano uliokuwa ukijadili rasimu ya mapendekezo ya kuwa na mkakati wa kitaifa wa kuendeleza ujasiriamali hapa nchini, aliyesimama ni mwezeshaji wa mkutano huo, Dkt. Donath Olomi.

No comments: