Saturday, July 15, 2017

The Desk & Chair Foundation yatoa msaada kwa mtoto Mlemavu

  Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation Tawi la Tanzania Sibtain Meghjee kulia, akimkabidhi Elizabert Tungu baiskeli (Wheel chair) kwa ajili ya  mwanaye Malale Mihayo (aliyekaa) ambaye ana tatizo la mtindio wa ubongo.Kushoto ni Abass Meghjee mmoja wa wafadhili na kiongozi wa taasisi hiyo yenye makao makuu nchini Uingereza. 
 Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foudation Tawi la Tanzania Sibtain Meghjee akimsaidia kumsukuma Malale Mihayo mkazi wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga baada ya kumkabidhi msaada wa baiskeli (Wheel chair) itakayomsaidia kwa usafiri. Mtoto huyo ana tatizo la mtindio wa ubongo.

Na Baltazar Mashaka, Mwanza
Familia ya mtoto Malale Mihayo (12) yenye makazi yake katika Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imeishukuru Taasisi ya The Desk & Chair Foundation (TD&CF) Tawi la Tanzania kwa msaada wa baiskeli (Wheel Chair ) kwa ajili ya mtoto wao mwenye tatizo la Cerebral Polse (mtindio wa ubongo).

Akizungumza na mtandao huu baada ya kukabidhiwa baiskeli hiyo mama mzazi wa mtoto huyo Elizabert Tungu alisema  itampunguzia adha ya kumbeba mwanaye huyo ambaye hana uwezo wa kufanya chochote kutokana na tatizo alilonalo.

“ Mwanangu alizaliwa  mwaka 2008 akiwa mzima wa afya, alipata tatizo hili baadaye akiwa na umri  wa miaka 3 na nusu.Nilimpeleka kutibiwa hospitali huko Arusha na Moshi madaktari wakanieleza anasumbuliwa na tatizo la uti wa mgongo, licha ya kutibiwa hakupata nafuu.Nawashukuru Desk & Chair kwa msaada huu,”alisema.

Bi. Tungu mwenye familia ya watoto sita alisema alimpeleka kwa waganga wa tiba za jadi nako hakupata nafuu na hivyo akalazimika kurejea nyumbani ambapo mwanaye huyo aliendelea kukakamaa viungo vya mwili wake na kupoteza uwezo wa kukaa wala kutembea.

Mtaalamu wa viungo (Physiotherapy) Prisla Paul Mselle alisema Malale alipata tatizo la kukosekana hewa ya oksjeni kwenye ubongo linalosababishwa na uzazi pingamizi  na homa kali kwa  watoto wa umri chini ya miaka mitano na kushambulia tishu ya ubongo kwa kuwa ubongo unakuwa haujakomaa.

Alisema kuwa mtoto huyo kupinda mgongo kumesababishwa na kuchelewa kupata tiba haraka  na hivyo anaweza kupata nafuu kwa kupata vifaa saidizi vya kuchechemua misuli yake ambavyo kwa kitaalamu ni standing board, stratching na standing table lakini hawezi kupona.

“ Baada ya kumbaini mtoto huyo niliangalia uwezo wake na kumwanzishia mazoezi ya kumnyoosha viungo kama magoti, vifundo vya miguu kwa kutumia vifaa vya kitaalamu ambavyo baadhi ni changamoto.Watoto wenye matatizo haya ni wengi changamoto ni kuwabaini,”alisema.

Mtaalamu huyo alieleza kuwa inahitajika elimu ya kutosha kwa jamii nyumba kwa nyumna ili kuweza kuwafichua na kuwabaini watoto wengi wenye ulemavu ambao wanafichwa kwa sababu ya mila potofu kuwa kuzaa mtoto mlemevu ni laana, mikosi pamoja na imani za ushirikina.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation Sibtain Meghjee alisema mtoto huyo ingawa amesaidiwa baiskeli hiyo anakabiliwa na changamoto ya mavazi na mahitaji mengine na kumtaka mzazi wake kumfungulia akaunti huku akiwaomba wadau wengine wajitokeze kumsaidia mtoto huyo kwa hali na mali kwa sababu matunzo yake ni tofauti na ya watoto wengine.

Alisema taasisi hiyo itaendelea kumsaidia lakini kutokana na changamoto ya kuwaibua watoto wenye matatizo hayo aliishauri serikali kuwa na mpango mahsusi wa kuwabaini watoto wenye matatizo ya aina hiyo na kuweka takwimu zao ili kurahisisha jinsi ya kuwahudumia na kuwapa misaada.

No comments: