Na Makuburi Ally
Wilayani Chamwino mkoani Dodoma maeneo karibu na Ikulu kunatarajia kuwa na burudani ya aina yake kwa wakazi wa kijiji hicho na maeneo yanayokizunguka, ambapo linatarajia kufanyika Tamasha la 9 la muziki wa asili ya Cigogo 'Chamwino Music Festival'.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Tamasha hilo, Dk. Kedmon Mapana mipangilio ya maandalizi kuelekea tamasha hilo yamekamilika kwa kiasi kikubwa yakiwemo makundi na kamati nzima ya maandalizi imekamilisha asilimia kubwa ya matakwa ya tamasha hilo.
Dk. Mapana anasema mipangilio imekamilika katika maeneo kama ukusanyaji wa fedha zitakazofanikisha tamasha hilo, maandalizi kwa washiriki na wageni waalikwa katika tamasha hilo.
Dk. Mapana anasema kwa upande wa bajeti ya tamasha hilo ambayo ilikuwa ni shilingi milioni 32 lakini zimepatikana milioni 18 kwa sababu kwamba wafadhili wakubwa ni watu binafsi wanaoamini urithi wetu ni muhimu sisi kama binaadam sababu utu wetu umejengeka katika mila na desturi.
"Ukitaka kupata utambuzi kwa wanachofikiria Wagogo jinsi wanavyokula, mahusiano yao ya kijamii na kwa ujumla kwa yote yanabebwa katika nyimbo na ngoma zao, hivyo tumeonelea tuyaweke wazi, ndipo tukaasisi tamasha hilo," alisema Dk. Mapana.
Anasema kwamba ufadhili wa tamasha hilo wameupata kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Chamwino Connect lenye makazi yake nchini Marekani huku wafadhili wengine ni serikali ya kijiji cha Chamwino ambacho kinatoa maeneo ya kufanyia tamasha hilo huku wafadhili wengine ni wasanii wenyewe ambao hujitolea kwa kiasi kikubwa ili kukuza utamaduni wao.
Dk. Mapana anasema maandalizi mengine ni kwa wasanii ambao wanashiriki tamasha hilo, yamekamilika kwa kiasi kikubwa kwani awali makundi yaliyopatikana yalikuwa 70 na wamefanikiwa kubaki na makundi 50 yaliyothibitisha kushiriki.
Anasema katika makundi hayo wanawafuatilia mienendo yao katika sanaa kwani wanataka kile cha asili katika muziki na sanaa husika na mambo mapya ambayo wanaweza kuyaonesha katika tamasha hilo.
Anasema kauli mbiu ya tamasha la mwaka huu ambayo imekuja katika muda muafaka kwa sababu serikali ya awamu ya tano imejipanga kupambana na Rushwa ambayo ni Piga rushwa kupitia Sanaa kwani ujumbe huo utafika kwa watu zaidi ya 10,000 kupitia tamasha hilo, ingawa wahusika wanatakiwa kuwa na dhamira ya utekelezaji .
Aidha Dk. Mapana anaweka bayana makundi shiriki ya tamasha hilo yanatoka katika Wilaya za Kongwa, Dodoma mjini na Chamwino na makundi mengine yanatoka nje ya mkoa huo.
Makundi hayo ni pamoja na Mbeta (Morogoro), Happy African Art (Iringa), Kipauli (Njombe), Samba Group na Tulia Traditional Dance Festival (Tukuyu- Mbeya), Mandoo na Shada (Bagamoyo) na Muungano (Singida).
"Kwanini tumeshirikisha na makundi mengine katika tamasha letu ni kujifunza pia tamaduni za mikoa mingine ili kuimarisha mila na desturi," alisema Dk. Mapana.
Dk. Mapana anakumbusha kwamba matamasha yaliyopita walishirikisha makundi kutoka maeneo mbali ya Tanzania ambako tamasha la mwaka juzi lilishiriki kundi la Taarab kutoka Zanzibar ambalo baada ya tamasha walitengeneza wimbo wenye vionjo mchanganyiko wa bara na Zanzibar.
Anasema katika maandalizi ya tamasha hilo kamati 70 ya maandalizi ya Chamwino Arts Centre imefanikisha kutunga wimbo wa halaiki ambao unahamasisha Umoja na amani kwa Tanzania ambao utaimbwa katika tamasha hilo.
Anasema kwa upande wa Malazi wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kukodi nyumba zaidi ya 50 zilizowazi kijijini hapo na kuwataka wasanii kuwasili kijijini wakiwa hawana shaka na malazi.
Anaweka bayana wageni wanaotarajia kuwepo kwenye tamasha hilo ni pamoja na wageni wanne kutoka Nzega Arts Centre ya Tabora ambao wanafika katika tamasha hilo kwa ajili ya kujifunza zaidi maandalizi ya tamasha lao la Sukuma- Nyamwezi.
Wageni wengine ni wanafunzi 12 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wanaokwenda kujifunza kuandaa matamasha ya muziki wa asili, wageni 12 kutoka vyuo vikuu nchini Marekani; 11 kutoka Chuo Kikuu cha Seattle Pacific na mmoja kutoka New Wark.
Mgeni mwingine ni kutoka Uganda kwenye taasisi isiyo ya kiserikali ya Soul Expression ambayo pia inahitaji kuunganisha nguvu ya pamoja na Kituo cha Sanaa cha Chamwino.
Huku mgeni mwingine mshiriki anatoka Visiwa vya Mayotte, Anima Abdallah ambaye aliwahi kuimba pamoja na wanamuziki nguli barani Afrika, Pepe Kalle, Papa Wemba na Koffi Olomide ambaye pia anajipanga kwa dhamira ya kuunganisha tamaduni za Mayotte na kituo cha sanaa cha Chamwino.
Dk. Mapana ambaye ni Mkuu wa Sanaa wa Chuo Kikuu ch Dar es Salaam, anamuweka bayana mgeni rasmi katika tamasha hilo ni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.
Anaeleza faida za matamasha ya muziki wa asili na kueleza kwamba yanasaidia wasanii na jamii kuendelea kuutunza utamaduni wao ambako pia wanataka Tanzania kuwa na utamaduni unaoishi.
"Tunayajali makundi ya sanaa tunayofanya nayo kazi kwani matamasha yaliyopita tulikuwa tunayafuatilia kwa karibu makundi hayo kwa zaidi ya miezi mitano ili kuendeleza mikakati ya kudumisha na kuendeleza utamaduni wetu," alisema Dk. Mapana.
Faida nyingine inayopatikana wameshapeleka makundi tisa katika matamasha ya nje ya Tanzania kwa lengo la kupanua wigo wa ufikishaji wa sanaa yetu nje ya nchi.
Makundi matano yalishawahi kushiriki matamasha nchini Poland ambayo ni Nyerere Muheme Group, Yerusalem, Ndagwa na Yeriko (Yote ya Chamwino) na Milungu Group (Kijiji cha Kawawa) huku kundi moja la Ufunuo Majereko limeshawahi kushiriki tamasha nchini Ujerumani, Ndagwa liliwahi pia kushiriki tamasha nchini Ufaransa.
"Katika hayo makundi, washiriki wote elimu yao ni ya darasa la saba ambao hivi sasa mawazo na akili zao na upeo pia vimebadilika kupitia ziara za nje ya nchi ambako wanajifunza mambo mbalimbali," alisema Dk. Mapana.
Faida nyingine wanayoipata ni kwamba wamejenga umoja mkubwa kwa wakazi wa Dodoma na maeneo mengine na pia wameongeza upendo na amani ambako pia anaeleza kwamba wao hawafanyi mashindano.
Anaeleza faida nyingine ni kufanikisha elimu ya kutosha kwa kila aliyehudhuria kupata maono mapya kupitia sanaa zinazofanyika kijijini Chamwino huku faida nyingine ni kuendeleza kurithisha elimu ya muziki wa asili, utamaduni, mila na desturi kwa sababu linashirikisha watoto, vijana na watu wazima.
Dk. Mapana anaweka bayana faida nyingine ya tamasha hilo ni kuisaidia serikali kutimiza wajibu wake kwani idadi kubwa ya watalii wanaongezeka kujionea sanaa ya Tanzania ikiwa ni nchi ya Amani na utulivu ndio maana wanakuja kujonea tamaduni zetu ambazo zinaonesha mwelekeo mzuri wa maendeleo.
Dk. Mapana anamalizia kuweka bayana faida nyingine ambayo inachangia ukuaji wa uchumi wa kijiji cha Chamwino kwa sababu katika tamasha hilo wenyeji wanauza chakula, vinywaji na wapishi pia wanapata fedha sambamba na biashara ndogondogo.
"Milioni 18 zilizopatikana kupitia tamasha hilo zinazama pale kijijini hivyo ni sehemu yetu ya uchagiaji wa maendeleo," alisema Dk. Mapana
No comments:
Post a Comment