Saturday, July 22, 2017

SH. BILIONI 1.669 KUTEKELEZA MIRADI YA MAJI ILEJE-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga sh. bilioni 1.669 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika wilaya ya Ileje mkoani Songwe.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Julai 22, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Ileje katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Itumba.

Waziri Mkuu amesema kati ya fedha hizo sh. bilioni moja zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji katika miji miwili ya Isongole na Itumba wilayani Ileje.“Kiasi kingine cha sh. milioni 669 kimetengwa kwa ajili ya maji katika vijiji mbalimbali vya wilaya ya Ileje katika mwaka wa fedha wa 2017/2018.

Hata hivyo, amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa Kampeni ya Rais Dkt. Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kusogeza huduma ya maji kwa urahisi.Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400.

Wakati huo huo Waziri Mkuu ameiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Songwe kuhakikisha inaimarisha ulinzi katika maeneo ya mipaka.Amesema kamati hiyo inatakiwa kuimarisha ulinzi katika maeneo yote ya mipaka ili kuizua wageni kuingia bila ya kufuata taratibu zilizowekwa kisheria.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Bw. Joseph Mkude alisema katika kipindi cha Julai 2016 hadi Juni 2017 jumla ya wahamiaji haramu 38 walikamatwa kwenye wilaya hiyo.Alisema kati ya wahamiaji hao haramu 36 ni raia wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na wawili walikua raia wa Malawi na wote walirudishwa makwao.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, JULAI 22, 2017.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wa wilaya ya Ileje baada ya kuwasili kwenye makazi ya Mkuu wa wilaya hiyo  akiwa katika ziara ya mkoa wa Songwe Julai 22, 2017.
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wabunge Janet Mbene wa Ileje (kulia) na Juliana Shonza wa Viti Maalum baada ya kuwasili kwenye makazi ya Mkuu wa wilaya ya Ileje kuanza ziara wialyani humo Februari 22, 2017. (Picha na ofisi ya Wziri Mkuu). 
 Baadhi ya watumishi wa umma, viongozi wa dini na taasisi binafsi wakimsikiliza  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao mjini Ileje Julai 22, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa umma, viongozi wa dini na viongozi wa taasisi binafsi mjini Ileje Julai 22, 2017. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa jengo la hospitali ya wilaya ya Ileje akiwa katika ziara ya mkoa wa Songwe, Julai 22, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary  (kushoto) wakitazama mbegu za mahindi zinazozalishwa na Kikundi cha SAM cha Ileje wakati alipotembelea banda la kikundi hicho kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara kwenye stendi ya mabasi ya Ileje Julai 22, 2017
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama vifaranga wa samaki wakati alipotembelea banda la Kikundi cha wanawake cha Tukazane cha Ileje  kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara kwenye stendi ya mabasi ya Ileje Julai 22, 2017.

No comments: