Wednesday, July 5, 2017

SERIKALI YAAHIDI KUBORESHA MIUNDOMBINU KUVUTIA WAWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA FEDHA VIJIJINI


Na Benny Mwaipaja, WFM-Dodoma

Serikali imeeleza kuwa inajitahidi kuboresha miundombinu kama vile teknolojia ya Mawasiliano, Barabara, Ulinzi, Maji na Umeme katika maeneo ya vijijini ili kuweka mazingira bora yatakayovutia wawekezaji kutoka sekta binafsi kuwekeza katika sekta ya fedha ili kupanua huduma hiyo katika maeneo ya mijini na vijijini.

Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Josephine Chagulla (CCM), aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuwapa wanawake elimu kuhusu mikopo pamoja na kufikisha huduma za kibenki maeneo ya vijijini ili waweze kufikiwa na huduma za kifedha.

Mhe. Josephine Chagulla ameeleza kuwa wanawake wengi wa vijijini hawakopesheki kwa sababu benki haziwafikii, pia hawana mafunzo maalumu ya kuwasaidia ujuzi wa namna ya kuzifikia huduma hiyo ya kukopeshwa

Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa, elimu ya fedha inahusisha wadau mbalimbali ikiwemo Serikali na Taasisi zake, ambapo kwa upande wa Serikali, Benki Kuu inaratibu uanzishwaji wa taasisi ya kitaifa itakayokuwa na jukumu la kuratibu, kuwezesha na kusimamia utoaji wa elimu ya fedha kwa jamii.

“Serikali kupitia Benki Kuu imetoa mwongozo wa Uwakala wa Huduma za Kibenki ili kupanua wigo wa huduma za kibenki kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi na kwa gharama nafuu hasa katika maeneo ya vijijini”. Alisema Dkt. Kijaji.

Alisema kuwa baada ya kuunda taasisi ya kitaifa ya Uratibu wa Elimu ya Fedha, kutakuwepo na mfumo rasmi nchini wa utoaji wa elimu ya masuala ya fedha kwa wananchi wote wakiwemo akina mama wa vijijini.” Alisema Dkt. Kijaji.

Dkt. Kijaji alifafanua kuwa, Taasisi za fedha zina utaratibu wa kutoa elimu ya fedha kwa wateja wao wakiwemo wanawake ili kuhakikisha kwamba wateja wao wanaendesha biashara zao kwa ufanisi.

“Serikali inatambua umuhimu wa wananchi kupata huduma za kibenki karibu na maeneo yao, pia inatambua umuhimu wa taasisi hizo katika kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi.” Alieleza Dkt. Kijaji.

Aidha, Dkt. Kijaji aliongeza kuwa Serikali inatambua benki nyingi zinaendesha shughuli zake mijini kwa sababu ya urahisi wa upatikanaji wa miundombinu muhimu kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za kibenki.

Katika swali la nyongeza Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Josephine Chagulla (CCM), alitaka kujua mpango Serikali wa kufungua matawi ya benki ya Wanawake katika mikoa yote ya Tanzania ili kuwasaidia wanawake kupata mikopo kwa urahisi.

Swali hilo lilijibiwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu, ambaye aliahidi kuwasiliana na Wizara ya Fedha na Mipango ili itimize ahadi iliyotolewa na Rais wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete ya kuipatia mtaji Benki ya Wanawake Tanzania ili iweze kufungua matawi nchi nzima na kutoa mikopo yenye masharti nafuu ikilinganishwa na benki nyingine

No comments: