Na. Bushiri Matenda- MAELEZO
Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuhakikisha kunakuwa na amani na mshikamano miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.
Akizungumza wakati akifungua mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Jumuiya hiyo leo Jijijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga alisema kuwa Tanzania itaendeleza jitihada zinazofanywa na SADC kwa nchi wanachama katika kuendelea kuimarisha Ushirikianao katika Siasa, Ulinzi na Usalama.
“Nawasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wetu wa SADC ambaye anaamini kuwa mkutano huu unatuleta pamoja katika kujenga ushirikiano wetu zaidi kuhakikisha kuwa tunaendelea kuwa na amani, umoja, mshikamano na ustawi kati ya nchi wanachama,” alisisitiza Dkt. Mahiga
Dkt. Mahiga alisema kuwa nchi wanachama zimeendelea kuwa eneo lenye usalama na ustawi kwa kuzingatia hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa na umoja huo kupitia kamati mbalimbali zilizoundwa kushughulikia mageuzi katika nchi za Lesotho hali iliyosaidia Taifa hilo kufanya uchaguzi wa wabunge mwezi June 2017 kwa amani.
Aliongeza kuwa katika mkutano huo watajadili swala la uhuru wa wananchi wan chi wanachama kutokuwa na vikwazo wanapotaka kuingia nchi nyingine,kuwa na Kikosi maalum cha Jeshi kwa ajili ya ulinzi wa amani,mikakati ya kusimamia masuala ya mawasiliano na habari, hali itakoyochochea maendeleo kati ya nchi wanachama.
Pia SADC kwa kuzingatia kifungu cha 7 (1) cha itifaki ya umoja huo kuhusu mapambano dhidi ya rushwa, nchi wanachama zitakuwa na sera na mikakati inayofanana katika kupambana na rushwa kwa kuzingatia mapendekezo ya Kamati ndogo ya mapambano dhidi ya rushwa yatakayojadiliwa katika mkutano huu.
Katika kutekeleza azma yakuondoa tatizo la rushwa kwa nchi wanachama Balozi Dkt. Maiga alizitaka nchi wanachama kuendelea kutekeleza itifaki hiyo katika kutokomeza rushwa katika nchi wanachama.
Aidha Balozi Maiga amewaalika wajumbe wa mkutano huo kutembelea vituo vilivyopo hapa nchini ikiwemo mlima Kilimanjaro, Serengeti, Visiwa vya Zanzibar na Mafia ili kujionea vivutio vilivyopo katika maeneo hayo.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa SADC Mhe. Stergomena Tax amesema kuwa Umoja huo utaendelea kushughulikia mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, pia amewaomba nchi wanachama na washirika wa maendeleo kuendelea kuchangia katika Jumuiya hiyo ikiwemo Umoja wa Ulaya (EU) .
Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa nchi wanachama unafanyika Jijini Dar es Salaam ukilenga kujadili maswala ya Siasa, Ulinzi, Usalama na Ushirikiano ndani ya Jumuiya hiyo.
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dr. Stergomena Tax akitoa neno la utangulizi wakati wa mkutano wa 19 wa Kamati ya Mawaziri wa Nchi za Jumuiya hiyo inayojadili ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama mapema hii leo Jijini Dar es SalaamA.
Waziri wa Mambo ya nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Mawaziri wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (hawapo pichani) wakati akifungua mkutano wa 19 wa Kamati hiyo unaojadili ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama mapema hii leo Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Mawaziri wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakimsikiliza Waziri wa Mambo ya nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (hayupo pichani) wakati akifungua mkutano wa 19 wa Kamati hiyo unaojadili ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama mapema hii leo Jijini Dar es Salaam. (Picha na Eliphace Marwa – MAELEZO)
No comments:
Post a Comment