Na Hamza Temba - WMU - Muheza, Tanga
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mhandisi Ramo Makani ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga kukutana
na wakulima 879 wa vijiji vitano katika Tarafa ya Amani Wilayani humo kwa ajili
kufanya uhakiki wa malipo ya fidia ya mazao waliyolipwa na Serikali ili kupisha
eneo la hifadhi ya msitu wa Derema.
Mhandisi Makani ametoa agizo hilo jana
katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Msasa IBC, Tarafa ya
Amani, Wilayani Muheza kufuatia malalamiko ya wananchi hao kupunjwa malipo yao wakati
wa ziara yake ya siku moja wilayani humo kwa ajili kutatua mgogoro wa ardhi
uliodumu kwa zaidi ya miaka 15 baina Serikali na wananchi wa vijiji hivyo vya
Kisiwani, Kwemdim, Msasa IBC, Antakae na Kambi.
Akisoma risala ya wakulima hao mbele
ya Naibu Waziri Makani, Mwenyekiti wa Kamati ya wakulima hao, Mohammed Rama
Shesha alidai kuwa jumla ya wakulima 1,128 wa vijiji hivyo wanailalamikia
Serikali kwa kuwalipa viwango pungufu vya malipo ya fidia ya mazao yao tofauti
na viwango vilivyolipwa na Serikali mwaka 2002 kupitia mradi wa FINIDA. Aidha,
alidai kuwa kuna baadhi ya mazao pia hayakulipiwa kabisa fidia hizo.
Akizungumzia viwango vya fidia hizo
Shesha alisema wananchi walilipwa Shilingi 28,800 kwa mche mmoja wa iliki na
Shilingi 11,000 kwa mche mmoja wa mgomba. Alidai viwango hivyo vilibadilika
kuanzia mwaka 2005 ambapo walilipwa Shilingi 3,315 kwa kila mche mmoja badala
ya Shilingi 5,100 kama ilivyoainishwa kwenye viwango vya Serikali hivyo akaomba
walipwe kiasi kilichobakia cha shilingi 1,785.
Akitolea ufafanuzi wa malalamiko
hayo, Naibu Waziri Makani alisema idadi kamili ya wananchi waliohakikiwa katika
eneo hilo ni 879 na sio 1,128 kama alivyodai mwenyekiti huyo. Aidha, alisema viwango
vilivyotumiwa kuwalipa wananchi hao mwaka 2002 sio vya Serikali na kwamba
vilitumiwa na mradi wa FINIDA uliofadhiliwa na Serikali ya Finland kwa ajili ya
kulipa fidia wananchi wa mpakani na hifadhi hiyo ili kufanikisha zoezi la
kuanisha mpaka wa hifadhi hiyo na kusaidia Serikali kutimiza azma ya kuhifadhi
eneo hilo.
Alisema viwango halali vya Serikali
vilivyopo kisheria kwa ajili ya kulipa fidia ya mimea hiyo ni kuanzia Shilingi
5,100 kwa kiwango cha juu kwa mmea uliokoma kufikia kiwango cha uzalishaji,
Shilingi 3,315 kwa mmea wenye mwaka mmoja na Shilingi 2,040 kwa mmea wenye
mwezi mmoja. Alisema viwango vingine vya malipo kwa kiwango cha chini ni
Shilingi 204, Shilingi 102 na Shilingi 51.
Alisema Serikali iliamua kulipa
kiwango cha Shilingi 3,315 kwa mazao yote ikiwemo yale yaliyostahili kulipwa
kiwango cha chini kabisa cha Shilingi 51 ili kuweka uwiano na kurahisha zoezi
hilo la malipo. Alihoji kama kuna mwananchi yeyote aliyelipwa chini ya kiwango
hicho japokuwa kulikuwepo na wengine mazao yao yalistahili kulipiwa viwango
hivyo, hakuna aliyejitokeza.
Kufuatia ufafanuzi huo aliuagiza
uongozi wa Wilaya ya Muheza kutumia kipindi cha mwezi mmoja kuanzia leo
Jumatatu kuonana na wakulima hao ili kuhakiki malipo yao na hatua zaidi ziweze
kuchukuliwa kama kuna yeyote aliyezulumiwa apewe haki yake.
"Kwa wale ambao tayari wana
kumbukumbu zao vizuri wazilete mbele ya Serikali, kupitia wao pengine tunaweza
kupata picha ya jumla pengine kulikua na mapungufu kwenye malipo. Kuanzia
jumatatu ijayo Mhe. DC tulitekeleze hilo la kukusanya nyaraka kwa wale
walizonazo tuweze kuzilinganisha na zile tulizokua nazo Serikalini tujadiliane
nao kwamba ni kitu gani kimebaki tofauti katika maeneo yale yale mliyofanyiwa
uhakiki", alisema Mhandisi Makani.
Alisema kwa wale ambao wamepoteza
nyaraka zao za malipo wataandaliwa utaratibu maalum wa uhakiki kwa kuwa
kumbukumbu zote za malipo zipo kwenye Kompyuta za halmashauri ya Wilaya ya
Muheza.
Alisema lengo la Serikali ya awamu
ya tano ni kuhakikisha inamaliza kabisa migogoro ya ardhi nchini. “Tutahakikisha
tunaboresha zaidi usimamizi wa uhifadhi wa rasilimali zetu za misitu,
wanyamapori na nyinginezo kuhakikisha migogoro hiyo inapungua kwa kasi kuelekea
kwenye sifuri, zero rate", alisema Makani.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Muheza, Mwanaisha Tumbo alisema, Serikali ya Wilaya imepokea maelekezo hayo na itayafanyia
kazi na kwamba maafisa wa Halmashauri watafika katika kila kijiji siku ya
Jumatatu na Jumatano kwa ajili ya kuendesha zoezi hilo la uhakiki.
Akizungumzia zoezi la fidia Mkuu
huyo wa Wilaya alisema pamoja na wananchi hao kulipwa fidia za mazao yao ambayo
yalilipwa kwa awamu tatu, asilimia 50 mwaka 2005, asilimia 25 mwaka 2006 na
asilimia 25 mwaka 2008, pamoja na asilimia 23 kama fidia ya ucheleweshaji wa
deni, Serikali pia itawapa maeneo ya fidia ambapo kila mwananchi aliyeathirika eneo
lake atapewa ekari tatu.
Alisema eneo ambalo limeanishwa kwa
ajili ya kuwagawia wananchi hao ni lililokuwa shamba la mkonge Kibaranga ambalo
lina ukubwa wa hekta 1370 sawa na ekari 3425 na lilikua likimilikiwa na Bodi ya
Mkonge, eneo hilo lilitolewa tamko ya kufutiwa umiliki wake na Mhe. Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli mwezi Julai, 2016.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi
Ramo Makani (katikati), akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Msasa IBC wilaya ya Muheza mkoani
Tanga jana wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo kwa ajili kutatua mgogoro
wa hifadhi ya msitu wa Derema. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mwanaisha
Tumbo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi
Ramo Makani (katikati), akimuonesha mwenyekiti wa kamati ya wakulima wa vijiji vitano vya
tarafa ya Amani, Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga, Mohammed Ramadhani Shesha viwango
halali vya serikali vya kulipia fidia za mazao kwa wananchi waliondolewa katika
eneo la hifadhi ya msitu wa Derema wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani
humo jana kwa ajili ya kutatua migogoro wa hifadhi hiyo. Kulia ni Mkuu wa
Wilaya ya Muheza, Mwanaisha Tumbo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi
Ramo Makani (kulia), akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Msasa IBC wilaya ya Muheza mkoani
Tanga jana wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo kwa ajili kutatua mgogoro
wa hifadhi ya msitu wa Derema.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi
Ramo Makani, (wa tatu kushoto), akiangalia eneo la Msitu wa hifadhi ya Derema
na viongozi wa wilaya ya Muheza Muheza wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani
humo jana kwa ajili ya kutatua mgogoro wa hifadhi hiyo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi
Ramo Makani (kulia), akisalimiana na wananchi wa Kijiji cha Msasa IBC wilaya ya Muheza Mkoani
Tanga jana wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo kwa ajili ya kutatua
mgogoro ya hifadhi ya msitu wa Derema.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi
Ramo Makani (kushoto), akimuonesha mwenyekiti wa kamati ya wakulima wa vijiji vitano vya
tarafa ya Amani, Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga, Mohammed Ramadhani Shesha (kulia)
viwango halali vya serikali vya kulipia fidia za mazao kwa wananchi waliondolewa
katika eneo la hifadhi ya msitu wa Derema wakati wa ziara yake ya siku moja
wilayani humo jana kwa ajili ya kutatua migogoro wa hifadhi hiyo.
No comments:
Post a Comment