Saturday, July 15, 2017

Naibu Waziri Dk. Kigwangalla aagiza uboreshaji wa huduma za Afya Tunduru

Naibu waziri wizara ya Afya, Jinsia, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto Dk. Hamisi Kigwangalla ametoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tunduru kuhakisha wanaboresha huduma za Afya katika Wilaya hiyo hasa kituo cha Afya Mkasale ambacho kimebainika kuwa na huduma mbovu huku pia kikiwa na uchakavu kwenye majengo yake hali ambayo inaweza kuhatarisha usalama na afya za watumishi na wagonjwa wanaohudumiwa hapo.

Akiwa katika ziara ya kikazi ya ukagazi wa utekelezajiwa agizo la uboreshaji wa vituo vya afya katika kila Kata nchini lilitolewa Desemba 2016, Dk. Kigwangalla akikagua kituo hicho cha Mkasale , aliweza kujionea mazingira hayo ambapo licha ya kupewa taarifa alitaka mara moja Uongozi wa Halmashahuri

hiyo kushughulikia suala ndani ya miezi mitatu ikiwemo Mkandarasi wa Maji kuhakikisha anaingiza mifumo ya maji ndani ya kituo hicho, pia aliagiza uongozi wa kijiji kushiriki katika kufanya usafi wa mazingira yanayozunguka kituo hicho cha Mkasale.

Awali akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Tunduru baada ya ziara hiyo ya kukagua vituo vya Afya na Hospitali ya Wilaya, Dk Kigwangalla amesema Serikali inaendelea na uboreshaji wa huduma za afya na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma zenye ubora na kwa wakati na lengo la serikali ya awamu ya tano ni kupunguza kwa asilimia kubwa changamoto zinazoikabili wilaya ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo vya kinamama wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, kukamilisha maboma yote ya vituo vya afya, zahanati na hospitali ambazo hazijakamilika, na kuhakikisha kuwa vifaa tiba na dawa zinapatikana za kutosha.

“Hata hivyo nawasihi wananchi tumuunge mkono Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kwa vita aliyoianzisha ya kulinda rasilimali za nchi yetu, kwani taifa limekuwa likiibiwa kwa muda mrefu sana ila umefika muda kuhakikisha kuwa rasimali za nchi zinatunzwa na kulindwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.” Alieleza Dk. Kigwangalla wakati akiwahutubia wananchi hao.

Aliendelea kusema kuwa ili mwananchi aweze kushiriki katika shughuliza uzalishaji ni lazima awe na afya njema na ili awe na afya njema ni lazima wananchi kwa kushirikiana na serikali kuboresha vituo vya kutoa huduma za afya na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

“Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya kwa kuhakikisha kuwa dawa zinakuwepo za kutosha katika hospitali na vituo vya afya na katika mwaka wa fedha 2017/2018 serikali imetenga bajeti ya kutosha kuhakikisha kuwa vifaa tiba vinakuwepo katika vituo vya afya na hospitali zote nchini” Alieleza Dk. Kigwangalla katika mkutano huo.

Samabamba na hayo serikali inahakikisha kuwa huduma za mama na mtoto zinatolewa bure kwenye hospitali za umma zote nchi ili kupunguza vifo vya wamama wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Dk Kigwangalla aliuagiza uongozi wa kijiji cha mkasale na mkotamo kutengeza barabara ya kuelekea katika kituo cha afya mkasale kutoka na barabara hivyo kuwa chafu sana hali inayoweza kuleta madhara kwa watumiaji hasa kwa wadudu kama nyoka.

"Nakuagiza mwenyekiti wa kijiji mara baada ya kumaliza kikao hapa upange ratiba na wananchi wako namna bora ya kuweza kutengeza barabara inayokwenda katika kituo cha afya mkasale na pia mupange ratiba ya kufanya ausafi katika kituo kwani kazi ya usafi ni ya wananchi"alisema Dk kigwangalla.

Aidha, katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma zilizo bora uongozi wa wilaya umeagizwa kufanya kuhakikisha vituo vyote vya afya vilivyopo wilayani Tunduru, vinajenga vyumba vya upasuaji katika vituo vyote vya afya, kukarabati maabara zote, na kuhakikisha kunakuwepo na mfumo wa maji safi wenye uhakika katika vituo vyote vya afya, kufanya matengenezo kwa vifaa vilivopata hitilafu ili kuboresha huduma.
Naibu waziri wizara ya Afya, Jinsia, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto Dk. Hamisi Kigwangalla akilakiwa na wananchi wa Kijiji cha Mkasale wilayani Tunduru, Mkoani Ruvuma wakati wa ziara yake hiyo 
Naibu waziri wizara ya Afya, Jinsia, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto Dk. Hamisi Kigwangalla akimsabahi mmoja wa watoto waliofika na wazazi wake wakati wa kumpokea katika Kijiji cha Mkasale wilayani Tunduru, Mkoani Ruvuma wakati wa ziara yake hiyo.
Naibu waziri wizara ya Afya, Jinsia, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza katika mkutano huo wa wazi kwa wananchi wa Halmashauri ya Tunduru, Mkoani Ruvuma


No comments: