Friday, July 21, 2017

MHE. HUSSEIN BASHE AWEZESHA VIKUNDI VYA WAJASIRIAMALI NZEGA MJINI


Katika Sherehe za Mwenge wa Uhuru zilizofanyika katika Uwanja wa Parking wilayani Nzega mkoani Tabora; Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini Mhe. Hussein Mohammed Bashe amekabidhi hundi ya kiasi cha Shilingi za Kitanzania Milioni Tatu na Laki Tisa (Tzs 3,900,000) kwa ajili ya kuwezesha vikundi mbalimbali vya wajasiriamali vilivyojitokeza kwenye sherehe hizo kuweza kumudu gharama za uendeshaji wa ofisi zao.

Hundi hiyo ilikabidhiwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa Bw. Amour Hamad Amour ambaye hakusita kusifia juhudi za Mheshimiwa mbunge kila mahali alipotembelea miradi ya maendeleo na huduma za jamii iliyokuwa anatekelezwa na Mhe. Hussein Bashe jimboni kwake na ndani ya Halmashauri ya Mji wa Nzega.
Bw. Amour H. Amour anasema.... "Tumetembea maeneo mengi, majimboni na wilayani, tumezunguka tukiukimbiza Mwenge kila mahali; wabunge wamejitokeza kushiriki zoezi hili lakini Mhe. Bashe amekua nasi bega kwa bega na ushirikiano wake umekua ni mkubwa sana. Haitoshi mambo anayoyafanya kwa wananchi wake ni mambo makubwa, ya kuigwa na kuungwa mkono"
Kwa upande waje Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mhe. Godfrey Ngupula alisema...."Kiongozi wa mbio za Mwenge, kuna msemo usemao msifie mtu angali yupo hai; nami leo nasema Mhe. Bashe anafanya kazi kubwa sana. Hapa tulipo tayari Mhe. Bashe amewapa ufadhili na amewalipia ada wanafunzi wote waliofaulu kujiunga na kidato cha Tano kwenye shule mbalimbali za serikali nchini, haitoshi bado anapambana kuhakikisha elimu ndani ya Jimbo la Nzega Mjini inakua na ufaulu unaongezeka"
Mhe. Ngupula anaendelea...."Mhe. Bashe ametoa fedha taslimu na vifaa kwa walimu na wanafunzi wote waliofaulu jimboni kwake. Kwangu mimi mbali na mengine yote haya tu yaatosha kusema kuwa mbunge huyu anafanya mambo makubwa na ya upendo sana kwa wananchi wake"
Aidha Mhe. Bashe amekabidhi jumla ya Tzs 1,900,000 kwa ajili ya kununulia vifaa na madawa kwa kikundi cha Fatilika Leather Shoes ambacho kinahusika na Uchakataji wa Ngozi na utengenezaji wa viatu pamoja na bidhaa nyingine za ngozi.
Uwekezaji wa Mbunge katika kikundi hiki kunatokana na msukumo wake wa kuhakikisha Nzega kunakuwa na kiwanda kikubwa cha Kuchakata Ngozi na kutengeneza viatu; na tayari mpaka sasa kwa kushirikiana na Halmashauri wamefanikisha kukipatia kikundi hiki eneo maalum na majengo kwa ajili ya kuendeshea uzalishaji wa bidhaa na baadae kuwa na kiwanda cha Ngozi na viatu ndani ya Jimbo la Nzega Mjini.
Ikiwa ni mwaka mmoja na nusu wa  ubunge wake Mhe. Hussein Mohammed Bashe amefanikiwa kutoa mikopo na fedha mbalimbali za uwezeshaji kwa zaidi ya vikundi mia moja vya ujasiriamali ndani ya Jimbo la Nzega Mjini.
Uwezeshaji huu unaendana na mipango ya Mbunge  katika kuhakikisha anainua maisha ya wananchi moja kwa moja kupitia vikundi vya wajasiriamali jimboni kwake na ndani ya Halmashauri ya Mji wa Nzega.
Mwaka 2016, Mheshimiwa Hussein Bashe kwa kushirikiana na Airtel Tanzania walizindua mradi wa kutoa mikopo yenye riba nafuu ya asilimia moja. Mradi huu ulianza kunufaisha jumla ya vikundi 20 ambavyo vilikuwa na wajasiriamali 100 na mpaka kufikia mwezi Machi 2017 jumla ya wajasiriamali 200 ndani ya Jimbo la Nzega Mjini walikuwa tayari wamenufaika na fedha kutoka katika mradi huu uliojulikana kama WanaNzengo Airtel Fursa.
Lakini yote hayo hayakutosha; Mheshimiwa Bashe aliendelea kuvisimamia na kuvisaidia vikundi mbalimbali vya wajasiriamali jimboni kwake kwa kuanzisha dawati maalumu linaloshughulikia masuala ya Uwezeshaji katika Ofisi ya Mbunge iliyoko katika Mtaa wa Uzunguni, Nzega Mjini.
Dhamira kuu inayomsukuma Mhe. Bashe ni kuona kuna mabadiliko makubwa ya kiuchumi na hali za maisha ya wananchi wake ili kuweza kuendana na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli katika kuhakikisha nchi yetu inakua ya Viwanda na Uchumi wa Kati huku hali ya maisha ya mtanzania mmoja mmoja ikiimarika na kupunguza utegemezi na misaada ya bajeti kutoka nje.
Mhe. Hussein Bashe anaamini ya kuwa "watu ni masikini sio kwa sababu wamezaliwa masikini ila wamekosa elimu na uwezeshaji ili kuweza kubuni na kuanza miradi na biashara ambazo zitabadili maisha yao"

No comments: