Saturday, July 22, 2017

KWA SIMU TOKA LONDON- Mitaani na muziki wa Kizungu

IJUE PIANO – NA MANUFAA YAKE
Na Freddy Macha 
Piano (au kinanda)  ni chombo mahsusi cha  Wazungu. Kitaaluma muziki maana yake ni vitu vitatu : melodi (unayoisikia bila hata kujua maneno na kuipigia uluzi), ridhimu (mapigo), na mpangilio wa sauti (“harmony”). Kipengele cha tatu ndiyo kigumu zaidi....
Kati ya vyombo muhimu  vya kitengo cha utunzi na upangaji (“harmony”) wa muziki ni Piano na Gitaa.
Ila Piano inaongoza Uzunguni.
 Ndiyo maana kila utakapokwenda,  makanisani, mabaa, mashuleni, majumbani na hata vituo vya usafiri hukosi Piano. Kihistoria, watunzi mashuhuri wa muziki ulimwenguni wametumia Piano kupanga vibao vyao vilivyofahamika na kupendwa miaka mingi  zaidi.
 Mifano michache  ni George Gershwin (“Summertime”- 1934),  Stevie Wonder (“Superstition”, 1973 ), Billy Joel  (“I love You Just the Way You are”- 1977) , Herbie Hancock (“Watermelon Man”, 1962), Paul McCartney ( “Nyimbo za Beatles,  “Let it Be”, “Long Winding Road”, “Yesterday”, nk), Prince (”When Doves Cry”, 1984), Gill Scott Heron (Mtunzi mashuhuri wa Mashairi aliyefariki 2011),  na  Alicia Keys , binti , kijana anayewika sasa.
Hata wanamuziki waimbaji walipiga piano, ingawa si sana hadharani. Prince, Michael Jackson, James Brown, nk.
Afrika yetu tunao marehem Fela Kuti na Abdullah Ibrahim (Afrika Kusini) anayeheshimika kama mmoja wa wapiga piano wakubwa duniani wa Jazz. Watanzania marehemu Patrick Balisidja  na Kassim Magati (Sunburst) vile vile. Miaka yake ya mwisho marehem Balisidja alipiga Piano akiwa na King Kiki.
 Kimuziki Piano ni kama kamusi. Ni muhimu kuijua kuelewa nini kinatendeka katika moyo, ngozi na mifupa  ya muziki. Kiafya upigaji Piano huoanisha pande mbili za Ubongo na kuzuia kuchakaa kwake.  Hivyo kwa Wazee na watu wa makamo ni kinga maradhi ya kusinyaa na kulemaa Ubongo mathalan “Dementia” na “Alzheimer”...
Hii ni sababu mkono  mmoja hufanya tendo tofauti na mwingine, unapotwanga Piano.
Kufuatana na maelezo ya mwanasayansi wa Kimarekani,  Roger Sperry (aliyeshinda tuzo la Nobel 1981) upande wa  kushoto wa Ubongo hufikiri,  na kulia  mambo ya hisia na utunzi. Bw Sperry alifikia ugunduzi huo akifanya utafiti wa kiini cha Kifafa.
 Ni vizuri pia kwa watoto wadogo na huwasaidia kufanya vyema katika masomo yote. Ndiyo maana muziki na Sanaa (kijumla) huzingatiwa sana mashuleni Uzunguni. 
Mwafrika jifunze Piano hata kama unaanza kuzeeka, itakufaa.  Na wasisitize wanao kufanya muziki na sanaa, utawajenga kiakili katika hesabu na sayansi pia.

 Rick Schmull akionesha vitu, mitaani London

Mdau nikionja embe. 

Mpiga piano, Billy Joel akiimba wimbo wake maarufu wa mapenzi duniani, kimaudhui na kimuziki.

Wimbo huo ulifanywa maarufu zaidi na marehemu Barry White. Ulidunda sana madisko na redio za  Afrika Mashariki enzi zake 


Mpiga Piano maarufu wa Afrika Kusini, Abdullah Ibrahim. Gwiji wa Jazz

No comments: