Thursday, July 13, 2017

JUMIA YATAJWA MIONGONI MWA MAKAMPUNI 50 BORA YA KITEKNOLOJIA DUNIANI


Na Jumia Travel Tanzania
Jumia Travel kwa mara ya pili mfululizo imeorodheshwa na Taasisi ya Kiteknolojia ya Massachusetts (MIT) ya nchini Marekani kuwa ni miongoni mwa makampuni 50 bora yanayotumia teknolojia katika biashara ili kurahisisha utoaji na upatikanaji wa huduma.
Kwenye orodha hiyo ambayo hujumuishwa makampuni makubwa ya kiteknolojia duniani kama vile Apple, Amazon, Facebook na Alibaba, Jumia kwa mwaka huu wa 2017 imetajwa kushika nafasi ya 44 kutokea nafasi ya 47 iliyoishika mwaka 2016.
MIT imeiatambua Jumia ambayo ilianzishwa mwaka 2012 ikijulikana kama Africa Internet Group (AIG) kwamba ni miongoni mwa makampuni ya awali kuchipukia barani Afrika, ikiwa na thamani ya dola za Kimarekani bilioni moja kutoka dola za Kimarekani milioni 327 ambapo ilimjuisha Goldman Sachs kama mmojawapo wa wawekezaji wake.
Ikiwa inajishughulisha na utoaji wa huduma mtandaoni kwenye maeneo kama vile manunuzi ya bidhaa, usafiri, chakula, makazi na magari ambazo zote zinatumia jina la Jumia, kampuni hiyo inapambana na changamoto za kufanya biashara kwa njia ya mtandao barani Afrika zikiwemo barabara zisizopitika kwa urahisi, wateja wasiotabirika, kukosekana kwa mtandao wa intaneti kwenye baadhi ya maeneo ambapo lengo kubwa ni kuwashawishi watu wa tabaka la kati kufanya matumizi.
Akizungumzia juu ya taarifa hiyo Meneja Mkazi wa Jumia Travel Tanzania, Bi. Fatema Dharsee amesema kuwa ni mafanikio makubwa kuingia na kutajwa kwenye orodha hiyo iliyosheheni makampuni makubwa ya kiteknolojia duniani kwa mara ya pili mfululizo kwani inaashiria ukuaji na kuonekana kwa mchango wao kwenye kuleta mapinduzi ya utoaji wa huduma mtandaoni.
“Licha ya changamoto kadhaa zinazolikabili bara la Afrika lakini bado linaonyesha matumaini makubwa kwenye uwekezaji wa sekta mbalimbali. Kiwango cha ukuaji wa watumiaji na ueneaji wa intaneti miongoni mwa waafrika wengi ni ishara nzuri katika kufanya vizuri kwa biashara za mtandaoni. Kwa mfano, kwenye ripoti ya masuala ya utalii tuliyoizindua mwishoni mwa wiki iliyopita inaonyesha kwamba watanzania wengi wanatumia simu zao za mkononi na kompyuta kwenye kutafuta na kufanya huduma za hoteli kwenye mtandao wetu wa Jumia Travel,” alisema Bi. Dharsee.
“Lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba tunatoa huduma bora na nafuu kwa kila mteja bila ya kujali kipato alichonacho. Kupitia mtandao wetu anaweza kuperuzi na kufanya huduma za hoteli mtandaoni muda wowote na mahali popote alipo kwenye hoteli takribani 1300 nchini Tanzania, zaidi ya 30,000 barani Afrika na zaidi ya 300,000 duniani kote. Na ukiachana na kuwepo hapa Tanzania pia huduma zetu zipo kwenye nchi 40 Afrika kote na tuna ofisi 10 miongoni mwa nchi hizo,” alihitimisha bosi huyo wa Jumia Travel kwa hapa nchini.
Kila mwaka MIT hutoa orodha ya makampuni 50 bora ambayo hutengeneza fursa mpya kwa kuunganisha teknolojia mbalimbali ziweze kutumia katika kurahisisha biashara. Baadhi yao ni makampuni makubwa kama vile Apple na Alphabet (kampuni mama ya Google) huku mengine yakiwa yanachipukia.
Orodha ya makampuni hayo kuanzia nambari 1 - 50 ni: Nvidia, SpaceX, Amazon, 23andMe, Alphabet, iFlytek, KitePharma, Tencent, Regeneron, Spark Therapeutics, Face++, FirstSolar, Intel, Quanergy Systems, Vestas Wind Systems, Apple, Merck, Carbon, Desktop Metal, Ionis Pharmaceuticals, Gamalon, Illumina, Facebook, Udacity, DJI, MercadoLibre, Microsoft, Rigetti Computing, Kindred Al, Sophia Genetics, Tesla, Oxford Nanopore, Foxconn, M-KOPA, ForAllSecure, FlipKart, BluebirdBio, Adidas, IBM, GeneralElectric, Alibaba, HTC, BluePrism, Jumia (Africa Internet Group), VeritasGenetics, Daimler, Salesforce, Snap, AntFinancial na Baidu.    

No comments: