Wednesday, July 5, 2017

HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUAHIRISHA MKUTANO WA SABA WA BUNGE LA KUMI NA MOJA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 05 JULAI, 2017


UTANGULIZI:                        

1.           Mheshimiwa Spika, leo tumefika mwisho wa Mkutano wa Saba wa Bunge la 11 ulioanza Jumanne ya tarehe 4 Aprili, 2017. Tunayo kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuifikia siku hii, tena baada ya kuwa tumetimiza wajibu wetu wa Kikatiba kikamilifu na kwa umahiri mkubwa. Huu ulikuwa ni Mkutano muhimu sana kwa nchi yetu kutokana na jukumu kubwa la kujadili na kupitisha bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 ulioanza tangu tarehe 1 Julai, 2017. Bajeti hii ambayo ni nzuri na ya kihistoria ni ya pili tu kati ya takribani Bajeti tano za Serikali ya Awamu ya Tano zitakazoandaliwa hadi kifikia Mwaka wa Fedha 2020/2021.

2.           Mheshimiwa Spika, wakati Bunge lako likiendelea, tarehe 13 Aprili, 2017 tulipokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya askari polisi wetu 8 waliopoteza maisha wakiwa wanalitumikia Taifa kwa kuuawa na kundi la wahalifu katika eneo la Jaribu Mpakani, Wilayani Kibiti mkoani Pwani. Askari hao waliopoteza maisha ni Inspekta Msaidizi Peter Kiguu, Koplo Francis, PC Haruna, PC Jackson, PC Zakaria, PC Siwale, PC Maswi na PC Ayoub. Pia, hivi karibuni mwezi Juni, 2017 Askari wetu wawili wa Kikosi cha Usalama Barabarani walivamiwa na kupigwa risasi na majambazi katika Kijiji cha Bungu “B” kilichopo Wilayani Kibiti. Aidha, wananchi wetu wengi wamepoteza maisha kutokana na uhalifu unaofanywa na majambazi waliopo katika maeneo ya Kibiti, Rufiji na Mkuranga.

3.           Mheshimiwa Spika, natumia fursa hii kulaani kitendo hicho cha kihalifu, na kutoa pole kwa Inspekta Jenerali wa Polisi kwa kuondokewa na vijana hao shupavu. Aidha, natoa pole kwa familia za wafiwa wote kwa kuondokewa na wapendwa wao. Mauaji ya Wananchi wetu na askari wetu hayakubaliki na wala hayavumiliki, kwani Askari ndio walinzi wetu sisi pamoja na mali zetu. Aidha, tishio kwa walinzi wa amani na wananchi wetu ni tishio kwetu sote, hivyo, Serikali itahakikisha waliohusika na mauaji hayo wanakamatwa na kuchukuliwa hatua stahiki. Wanaweza kukimbia, lakini hawataweza kujificha daima. Tutawakamata!.

4.           Mheshimiwa Spika, asubuhi ya tarehe 6 Mei, 2017, nchi yetu iliamka na simanzi kubwa kufuatia ajali iliyogharimu maisha ya watu 36, wakiwemo wanafunzi 33, walimu wawili na dereva wao, waliokuwa kwenye safari ya kimasomo Wilayani Karatu. Ajali hiyo imezima ndoto za vijana hao na kuacha vilio kwenye familia zao. Namuomba Mwenyezi Mungu azilaze mahali pema Peponi roho za marehemu. Aidha, nawaomba wazazi, walezi, walimu na marafiki wa watoto hao waendelee kumtumainia Mwenyezi Mungu kwa mtihani huo mkubwa walioupata. Naendelea kutoa wito kwa vyombo vyote vinavyohusika na ukaguzi wa vyombo vya moto vya usafiri kwa wanafunzi na abiria wafanye ukaguzi wa kina na wa mara kwa mara ili kuliepusha Taifa na ajali zinazoweza kuzuilika.

5.           Mheshimiwa Spika, nchi yetu pia ilipata pigo la kuondokewa na watumishi wawili wastaafu waliolitumikia Taifa hili kwa umahiri na uadilifu mkubwa. Watumishi hao ni marehemu Paul Sozigwa, aliyekuwa Katibu wa Rais wa Awamu ya Kwanza; na Marehemu Said Mwambungu, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma. Namwomba Mwenyezi Mungu awape pumziko la amani marehemu wote baada ya kulitumikia Taifa letu kwa utumishi uliotukuka na umahiri mkubwa.

SHUGHULI ZA BUNGE

6.           Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, Bunge lako Tukufu limejadili na kupitisha bajeti za Wizara zote 19 na Bajeti nzima ya Serikali Kuu, kupitisha Maazimio matano (5) ya kuridhia Mikataba mbalimbali ya Kimataifa na kupitisha Miswada ya Sheria mbalimbali, ambayo ni Muswada wa Sheria ya Fedha za Matumizi; Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka, 2017; Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017; Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba inayohusu Maliasili za Nchi, 2017; na Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili.

7.           Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu jumla ya maswali 499 ya msingi na mengine 1,834 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali kupitia kwa Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu. Vilevile, katika kipindi hiki Ofisi ya Bunge iliendesha Semina mbalimbali kwa Waheshimiwa Wabunge kwa lengo la kuwajengea uwezo zaidi na kuwapa uelewa mpana wa masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya nchi yetu.

8.           Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu pia lilipata fursa ya kuchagua Wawakilishi wa Tanzania kwenye Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo Wabunge tisa walichaguliwa. Kati ya Wabunge hao, watano ni wanawake, na wanne ni wanaume. Ni matumaini yangu kuwa Waheshimiwa Wabunge hao wataiwakilisha vema nchi yetu na kwamba watatimiza kikamilifu wajibu wao kwa mujibu wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaelekezwa kufanya kazi kwa karibu na Wabunge hao ikiwa ni pamoja na kuwapa ushirikiano unaostahili ili waweze kutekeleza vizuri majukumu yao kwenye Bunge hilo.

9.           Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kukushukuru wewe binafsi Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na timu yake, Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Waheshimiwa Wabunge na Watendaji na Wataalam wa Serikali pamoja na watumishi wa Ofisi ya Bunge kwa kufanikisha kazi zote zilizopangwa kwenye Mkutano huu tena kwa ufanisi mkubwa.

10.        Ninawapongeza pia na kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa maelezo mazuri ya ufafanuzi waliyotoa wakati wa kujibu maswali mengi ya msingi na ya nyongeza ya Waheshimiwa Wabunge pamoja na kujibu hoja za Kamati za Kudumu za Bunge na hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge binafsi ndani ya Bunge zima. Serikali inathamini sana maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge, na tunaahidi kuendelea kuzingatia maoni na ushauri wao.

AZIMIO LA BUNGE KUUNGA MKONO JITIHADA ZA MHESHIMIWA RAIS

11.        Mheshimiwa Spika, tarehe 14 Juni, 2017 Bunge lako Tukufu lilipitisha Azimio la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hatua anazochukua kukabiliana na upotevu wa mapato ya Serikali katika Sekta ya Madini. Aidha, tarehe 29 Juni, 2017 Bunge lako lilikubali kwa kauli moja kuridhia mabadiliko ya ratiba ya Mkutano huu wa Bunge la Bajeti ili kuongeza siku tano za kazi kwa lengo la kuwezesha kujadili Miswada mitatu ya mwaka 2017 inayohusu kulinda maliasili na rasilimali za Taifa ikiwemo madini. Hii inadhihirisha kwamba Bunge hili ni la wananchi na linazingatia maslahi ya nchi.

12.        Mheshimwa Spika, napenda kuungana na Waheshimiwa Wabunge kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake mahiri, juhudi na hatua stahiki anazoendelea kuchukua ili kuhakikisha kwamba Watanzania na Taifa kwa ujumla wananufaika na rasilimali za Taifa. Nawasihi wananchi wote na viongozi, tuendelee kumuunga mkono Mheshimiwa Rais katika jitihada zake hizo za kulinda maliasili za nchi yetu.

HALI YA ULINZI NA USALAMA:

13.        Mheshimiwa Spika, kwa ujumla hali ya ulinzi na usalama nchini ni shwari. Usalama wa raia na mali zao unaendelea kulindwa, na mipaka yote ya nchi yetu iko salama. Aidha, vikosi vya ulinzi na usalama viko imara na madhubuti katika kulinda mipaka na usalama wa nchi yetu. Hata hivyo, wapo baadhi ya wenzetu wanaotishia usalama wetu kwa kushiriki kwenye vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha. Mathalan, katika miezi ya hivi karibuni, kumekuwa na mauaji ya kuvizia katika maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji.

14.        Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila raia wa Tanzania, wakiwemo wananchi wa Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji wanakuwa huru kufanya shughuli zao za maendeleo bila kuhofia usalama wa maisha yao. Serikali inaendelea kuchukua hatua za muda mfupi na za muda mrefu ili kurejesha hali ya usalama katika maeneo hayo. Tumeongeza doria na vitendea kazi kwa askari. Vilevile, tumefanya maamuzi ya kuunda Kanda Maalum ya Kipolisi katika Mkoa wa Pwani itakayojumuisha Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji na tayari Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo Maalum amekwishateuliwa. Hivyo, natoa wito kwa raia wema katika Wilaya hizo, waendelee kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kuwezesha watuhumiwa wote kukamatwa.

15.        Mheshimiwa Spika, sanjari na mikakati ya kudhibiti uhalifu unaofanywa ndani ya nchi, tunaendelea pia kudhibiti uhalifu unaovuka mipaka (cross border crimes). Ili kutimiza jukumu hilo, tunaendelea kuboresha huduma za uhamiaji na kudhibiti nyaraka zinazotolewa na Idara ya Uhamiaji. Tumeanzisha mfumo wa kuhakiki nyaraka, hususan vibali vya kuishi nchini pamoja na Hati za Kusafiria. Vilevile, tumehuisha utaratibu wa kisheria wa kutoa “migrant pass” kwa wahamiaji walowezi, ili kuweza kuwatambua kwa urahisi. Kwa jitihada hizi, tutaweza kudhibiti nyaraka za kughushi na kudhibiti wahalifu wa kimataifa wanaovuka mipaka.

URATIBU WA MAAFA:

16.        Mheshimiwa Spika, katika msimu wa masika, baadhi ya maeneo ya nchi yetu yalipata mvua za juu ya wastani na hivyo kusababisha maafa na madhara kwa wananchi ikiwemo vifo, majeruhi na uharibifu mkubwa wa makazi na miundombinu. Mikoa iliyoathirika zaidi ni Tanga, Arusha, Kagera, Dar es Salaam na visiwa vya Unguja na Pemba. Kutokana na mvua hizo, watu 15 walipoteza maisha, 78 walijeruhiwa, nyumba 1,845 na majengo 36 ya taasisi mbalimbali yaliharibiwa katika viwango tofauti. Vilevile, miundombinu ya barabara 48 katika mikoa 11 iliathiriwa na hivyo kuzorotesha kwa muda usafiri na usafirishaji katika maeneo husika. Aidha, viwanja vya ndege vya Arusha, Musoma, Ziwa Manyara, Mafia na Sumbawanga navyo viliathiriwa na mvua hizo. Natoa pole kwa waathirika wote kutokana na kadhia hiyo.

17.        Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na athari za mvua hizo, Serikali iligharamia matibabu ya majeruhi na mazishi ya waliopoteza maisha. Aidha, Serikali imetoa misaada ya kibinadamu kama vile chakula, dawa, nguo na kufanya matengenezo ya dharura kwa miundombinu iliyoharibika. Zoezi la ukarabati wa miundombinu iliyoharibiwa na mvua linaendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi.

18.        Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu menejimenti ya maafa hususan kuzuia na kuweka mipango thabiti ya wananchi kujiandaa na maafa ili kupunguza athari za maafa pindi yanapotokea. Aidha, tutaendelea kutoa taarifa za utabiri wa hali ya hewa mara kwa mara na kwa wakati, ili kutoa fursa kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa na wananchi kujiandaa.

Vilevile, tutakamilisha mifumo ya ufuatiliaji wa maafa kwenye kituo chetu cha Uratibu na Mawasiliano wakati wa Dharura; kuainisha na kutambua maeneo hatarishi kwa maafa pamoja na kuendelea kuijengea uwezo Idara yetu ya Uratibu wa Maafa.

BAJETI YA SERIKALI NA MPANGO WA MAENDELEO KWA MWAKA 2017/2018

19.        Mheshimiwa Spika, kuanzia tarehe 4 Aprili, 2017 hadi tarehe 20 Juni, 2017 Bunge lako Tukufu lilipokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Taasisi mbalimbali za Umma, Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na Mfuko wa Bunge na Mfuko wa Mahakama. Aidha, Bunge lilipokea na kujadili Hoja ya Serikali kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2016, Mpango wa Maendeleo pamoja na makadirio ya Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2017/2018 ya jumla ya Shilingi Trilioni 31.7.

20.        Mheshimiwa Spika, niruhusu niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango (Mb.), Waziri wa Fedha na Mipango na Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) kwa hotuba nzuri ya Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/2018. Nawapongeza pia Watendaji wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa umakini mkubwa wa maandalizi ya Bajeti yenyewe. Aidha, nawapongeza kwa kutoa maelezo na ufafanuzi wa kina kwa hoja za Waheshimiwa Wabunge wakati wa kuhitimisha Hoja hiyo. Kipekee kabisa, nawapongeza na kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa hoja za maboresho na kwa kupitisha Bajeti ya Serikali kwa kura nyingi.

21.        Mheshimiwa Spika, kura za Waheshimiwa Wabunge kupitisha Bajeti ya Mwaka 2017/2018 ni kielelezo kwamba, Bajeti hii inajibu kiu ya wananchi ambao ninyi Waheshimiwa Wabunge mnawawakilisha. Kupitia michango yenu na kwa pongezi zenu kwa Serikali, nimepata faraja kwamba mnathamini na kuheshimu usikivu wa Serikali kwa maoni ya wananchi. Serikali hii ni sikivu, makini na inazingatia maslahi ya wananchi walio wengi na hasa wa kipato cha chini. Hivyo, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali siyo tu itaendelea kusikia, bali itasikiliza na kuchukua hatua, kama tulivyofanya kwenye Bajeti ya mwaka 2017/2018 kwa kufuta kodi mbalimbali za kero hasa katika kilimo na mifugo ili kuwawezesha wananchi kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.

22.        Mheshimiwa Spika, baada ya Bunge lako kuidhinisha Bajeti ya Serikali, tutahakikisha tunasimamia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2017/2018. Tayari tumeandaa Mkakati wa Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo, ambao unaainisha hatua za utekelezaji, vigezo vya kupima ufanisi na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa katika kukamilisha miradi husika. Vilevile, tunaandaa mfumo wa kuhifadhi taarifa za miradi ya maendeleo (National Project Databank) ili kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi na changamoto zinazoikabili, kwa lengo la kuikwamua. Sanjari na hatua hizo, Serikali imetoa maelekezo kwamba, Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini viimarishwe na kupewa nyenzo stahiki ili vifuatilie miradi ya maendeleo hatua kwa hatua. Shabaha yetu ni kuhakikisha kuwa miradi inasimamiwa kikamilifu, inaleta tija na kutekelezwa kwa ubora na viwango vilivyoainishwa kwenye Mikataba.

23.        Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba, mipango tuliyojiwekea haiwezi kufanikiwa, endapo tutazembea katika ukusanyaji wa kodi na mapato ya Serikali. Hivyo, Serikali itaendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato; kuimarisha ukusanyaji wa mapato; kudhibiti biashara ya magendo; kuhimiza matumizi ya mashine za kielektroniki katika ukusanyaji mapato na kudhibiti udanganyifu katika ukadiriaji wa ushuru wa forodha. Wito wangu kwa Waheshimiwa Wabunge ni kuhakikisha kuwa mnashirikiana na Halmashauri kubuni vyanzo vya mapato na kuhamasisha ulipaji wa kodi bila shuruti.

24.        Mheshimiwa Spika, kulipa kodi ni uzalendo, tuwahamasishe wananchi wenzetu waone fahari kuwa sehemu ya mafanikio ya nchi yetu kwa kulipa kodi na kuwafichua wakwepa kodi. Ahadi yetu ni kuendelea kusimamia kila senti itakayokusanywa, ili itekeleze jukumu lililokusudiwa. Aidha, tutaendelea kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa Bajeti iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu ili kuhakikisha kwamba fedha zilizotengwa zinatumika kwa umakini na kuleta tija kwa maendeleo ya nchi yetu. Tulipe kodi kwa maendeleo ya nchi yetu!

SEKTA YA KILIMO

Hali ya chakula nchini

25.        Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, hali ya chakula siyo ya kuridhisha sana, bado kuna maeneo yenye upungufu wa chakula. Pia, yapo maeneo yaliyopata mvua nyingi ambayo yamepata chakula cha kutosha. Hii ni kutokana na mazao ya chakula katika maeneo hayo kuanza kukomaa. Aidha, kutokana na wakulima katika baadhi ya maeneo kuanza kuvuna mazao yao, mwenendo wa bei za vyakula hususan mahindi imeanza kushuka katika masoko mbalimbali. Hata hivyo, kutokana na nchi zinazotuzunguka kuwa na upungufu mkubwa wa chakula, na umuhimu wa kuwa na usalama na kujitosheleza kwa hifadhi ya chakula, ni vizuri kila kaya ikahakikisha kwamba inakuwa na akiba ya chakula kwa matumizi ya baadaye. Aidha, tumepiga marufuku usafirishaji mahindi nje ya nchi bila kibali, badala yake tunahamasisha uongezaji wa thamani ya mazao badala ya kusafirisha nafaka ghafi. Hii inatokana na kuwepo na maeneo ambayo hadi sasa hayana chakula cha kutosha. Nashauri Wafanyabiashara wasambaze mahindi huko. Aidha, natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa ya Mipakani kutekeleza agizo la Serikali la kuchukua hatua kwa watakaokiuka agizo hilo.

Mfumo mpya wa Usambazaji wa Mbolea

26.        Mheshimiwa Spika, Serikali inajipanga vyema msimu ujao wa kilimo kwa kusambaza pembejeo na kuhamasisha matumizi ya mbolea. ili kufanikisha azma hiyo, katika bajeti ya Mwaka 2017/18 Serikali imeamua kuimarisha utaratibu wa upatikanaji na usambazaji mbolea kupitia Mfumo wa Uagizaji wa Mbolea kwa Pamoja (Fertilizer Bulk Procurement System).

27.        Mheshimiwa Spika, kupitia mfumo huo, mbolea itaagizwa na waagizaji watakaopitishwa kwenye utaratibu wa zabuni, na wakulima wataweza kununua mbolea hiyo katika maduka ya pembejeo vijijini kwa bei dira itakayopangwa na Serikali. Mfumo huo mpya utaanza kwa kuingiza mbolea ya kupandia aina ya DAP na mbolea ya kukuzia aina ya UREA ambazo zinatumiwa na wakulima wengi. Mbolea za aina nyingine zitaendelea kuletwa kwa utaratibu wa zamani. Napenda kurejea maelekezo yangu kwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwamba isimamie kikamilifu zoezi hili la usambazaji wa mbolea ili kuhakikisha kuwa mbolea inawafikia wakulima miezi miwili au mitatu kabla ya msimu wa kilimo haujaanza.


Maboresho kwenye Sekta ya Mifugo
28.        Mheshimiwa Spika, pamoja na idadi kubwa ya mifugo tuliyonayo nchini, lakini mchango wake kwenye Pato la Taifa na katika kutuingizia fedha za kigeni siyo wa kuridhisha. Kutokana na hali hiyo, tarehe 15 Juni 2017 nilikutana na Maafisa Mifugo wa Wilaya zote nchini kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha sekta ya mifugo nchini ili iweze kuleta tija na kuongeza mchango wake kwenye Pato la Taifa. Miongoni mwa mikakati tuliyojiwekea ni pamoja na kuwawezesha wafugaji kupata maeneo mahsusi ya malisho ya mifugo yao na kuwapatia mafunzo ya stadi za ufugaji bora. Vilevile, tumetoa maelekezo kwa Maafisa Mifugo kuwatembelea wafugaji ili kuwahudumia na kuwapa mafunzo ya ufugaji bora. Aidha, tumezindua Mwongozo wa Ufugaji Bora nchini, ambao utakuwa ni dira ya kuwaongoza wafugaji kuhusu namna ya kuboresha sekta ya mifugo nchini. Lengo letu ni kuwa na mifugo michache lakini yenye tija kubwa. Hata hivyo, tumekemea wafugaji wasilishe mifugo yao katika mashamba yenye mazao ya chakula, na pia kuchungia kwenye misitu iliyohifadhiwa. Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka agizo au katazo hilo.

SEKTA YA ARDHI

Upimaji na Umiliki wa ardhi

29.        Mheshimiwa Spika, ardhi isiyopimwa ina thamani ndogo na ni chanzo cha migogoro isiyo ya lazima. CCM iliona jambo hili, na kupitia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015, iliielekeza Serikali kuhakikisha kuwa kila kipande cha ardhi ya Tanzania kinapimwa. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali imeweka Mkakati na Mpango Kazi wa kuwezesha kufikia lengo la kupanga matumizi bora ya ardhi katika vijiji 1,500 na wilaya 5 kila mwaka. Aidha, Serikali inaendelea kuchukua hatua stahiki za kupunguza gharama za umilikaji wa ardhi nchini. Katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, Serikali imepunguza tozo ya mbele (premium) kutoka asilimia 7.5 ya thamani ya ardhi hadi asilimia 2.5 tu. Natoa wito kwa wananchi kuchangamkia punguzo hili na kujitokeza kupimiwa na kumilikishwa ardhi.

Kuimarisha Huduma katika Ofisi za Ardhi za Kanda
30.        Mheshimiwa Spika, kazi ya upimaji wa ardhi haiwezi kufanikiwa bila ya rasilimali watu. Serikali itaendelea kuimarisha Ofisi za Ardhi za Kanda kwa kupeleka wataalam wa kada mbalimbali na kuwawezesha kwa kuwapatia vitendea kazi stahiki. Lengo letu ni kuwawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali za ardhi katika kanda badala ya kufuata huduma hizo Makao Makuu ya Wizara. Nawasihi watumishi watakaohamishiwa katika Ofisi za kanda pamoja na wale waliopo katika Halmashauri, wafanye kazi kwa ushirikiano na watekeleze majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia sekta ya ardhi na kutoa huduma kwa wananchi bila ubaguzi, bila usumbufu na bila ya kuomba rushwa ya aina yoyote ile.

SEKTA YA WANYAMAPORI

Hifadhi ya Mapori
31.        Mheshimiwa Spika,  asilimia 28 ya eneo la nchi yetu limetengwa kwa ajili ya kuhifadhi rasilimali za Taifa ikiwemo misitu, wanyamapori, na utunzaji mazingira kwa ajili ya matumizi ya binadamu na viumbe hai wakiwemo wanyamapori ambao wanachangia kwa kiwango kikubwa katika shughuli za utalii. Changamoto kubwa iliyopo sasa katika mapori yetu ya hifadhi ni uvamizi wa mifugo, na kwa bahati mbaya kwenye mikoa ya mipakani, mifugo mingi imekuwa inatoka nchi jirani.

32.        Ili kuhakikisha kwamba Hifadhi za Taifa na mbuga zetu za wanyamapori zinalindwa kikamilifu. Mwezi Novemba, 2016 niliagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuweka alama za mipaka (beacons) kuainisha maeneo yote ya hifadhi nchini kwa lengo la kuondoa migogoro iliyopo. Baada ya kuweka alama hizo, Serikali imeanza rasmi zoezi la kuondoa mifugo yote ndani ya hifadhi. Aidha, nimeelekeza kwamba, uwekaji wa alama au nguzo hizo uhusishe Halmashauri za Wilaya na Ofisi za Wakuu wa Wilaya. Ramani zinazoonyesha mapori zitumike. Aidha, mapori yote yaliyohifadhiwa kisheria yaheshimike.

33.        Mheshimiwa Spika, kufuatia kuwepo kwa migogoro baina ya Wafugaji na Wakulima na migogoro baina ya wafugaji na wahifadhi wa mapori, nimeelekeza kwamba ifikapo mwisho wa mwezi Julai 2017 Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wabainishe maeneo yote ya Ranchi za Taifa za Mifugo ambazo hazitumiki na kuzigawa katika vitalu (blocks) kwa wafugaji ili mifugo mingi iondolewe vijijini na ipelekwe kwenye maeneo hayo ili Serikali iweze kutoa huduma za ugani za kisasa huko kwenye hizo blocks.

34.        Natoa wito kwa wafugaji wote nchini kufuata Sheria za Hifadhi za Taifa, Mbuga za Wanyamapori, maeneo tengefu pamoja na vyanzo vya maji. Mifugo yote itakayokutwa ndani ya hifadhi, hatua kali zitachukuliwa na kufikishwa mahakamani. Aidha, tukumbuke kuwa ardhi haiongezeki lakini wafugaji na mifugo vinaongezeka, hivyo ni lazima tufuge kisasa na tufuge mifugo michache yenye tija ambayo tutaweza kuihudumia katika maeneo yatakayotengwa kwa ajili ya ufugaji.

SEKTA YA AFYA

Ununuzi wa dawa na vifaa tiba

35.        Mheshimiwa Spika; kama ambavyo nimekuwa nikisisitiza kuhusu umuhimu wa afya bora kwa wananchi wetu, Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa kununua, kutunza na kusambaza dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 236 zikiwa ni fedha za ndani kwa ajili hiyo. Aidha, Serikali imetenga fedha za ndani kiasi cha Shilingi Bilioni 33 kwa ajili ya chanjo za watoto na makundi maalum. Nitoe rai kwa wazazi/walezi kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo zote zinazotakiwa ili kuwakinga na magonjwa na kuwajengea msingi mzuri wa maisha yao ya baadaye. Aidha, kila mwananchi ajenge utamaduni wa kupima afya yake mapema ili kubaini tatizo lake la kiafya mapema, badala ya kusubiri hadi ugonjwa ufike hatua mbaya ndipo aende hospitali.

Vifo vitokanavyo na uzazi

36.        Mheshimiwa Spika, tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi bado ni changamoto kubwa katika nchi yetu. Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi ni 556 kwa kila vizazi hai 100,000. Hali hii haikubaliki na haivumiliki, kwani wanaopoteza maisha ni Watanzania wenzetu, ni mama zetu, ni wake zetu, ni dada zetu na ni watoto wetu. Tumesikia maoni na michango ya Waheshimiwa Wabunge kuhusu suala hili wakati wa Mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, bajeti ya Wizara ya Afya na Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango.

37.        Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali imewasikia na kwa hakika inaguswa sana na vifo vitokanavyo na uzazi. Ndio maana Serikali imeamua kuongeza fedha za ndani kwa ajili ya kuimarisha huduma za Afya ya Mama na Uzazi. Serikali imeamua kwamba, itanunua, kusambaza na kutoa bila malipo dawa kwa ajili ya uzazi salama katika vituo vya umma vya kutolea huduma. Hii ni pamoja na dawa ya kuzuia kutokwa na damu baada ya kujifungua, dawa kwa ajili ya kifafa cha mimba na dawa kwa ajili ya kuongeza damu. Jumla ya shilingi bilioni 7 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Vilevile, Serikali imejizatiti kuongeza kasi ya ujenzi wa vituo vya afya na zahanati vijijini pamoja na kuimarisha vituo vyote vya kutolea tiba nchini kwa lengo la kuboresha huduma za Afya. Hivyo, napenda kuwahakikishia wanawake wote nchini, kwamba hakuna mwanamke mjamzito atakayepoteza maisha kwa kukosa dawa/sindano ya kuzuia kuvuja damu au kukosa dawa ya kuzuia kifafa cha mimba.

SEKTA YA ELIMU

Kuinua Ubora wa Elimu na Mafunzo
38.        Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba yangu ya kufungua mkutano wa saba wa Bunge lako tukufu, unaoahirishwa leo nilieleza kwa kirefu umuhimu wa watoto wetu kutoa kipaumbele kwa masomo ya sayansi. Nilisema, endapo watoto wetu hawatasoma masomo ya sayansi, watabaki kuwa watazamaji kwenye uchumi wa viwanda. Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu, kwamba, Serikali imeanza kutimiza wajibu katika kuweka mazingira wezeshi kwa watoto wetu kujifunza masomo ya sayansi kwa vitendo.

39.        Tarehe 6 Juni, 2017 nilizindua zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara kwa ajili ya shule za sekondari 1,696 vyenye thamani ya shilingi bilioni 16.9. Vifaa hivyo vinaendelea kusambazwa katika shule za Tanzania Bara ambazo zimekamilisha ujenzi wa maabara. Hivyo, natoa wito kwa wanafunzi kutumia vifaa hivyo kusoma kwa bidii masomo ya sayansi, na kuvitunza ili vinufaishe wanafunzi wengi zaidi. Aidha, Halmashauri zote nchini ambazo hazijakamilisha ujenzi wa maabara zinaelekezwa kukamilisha zoezi hilo mapema, ili vifaa vingine vitakapoletwa visambazwe haraka.

Elimu Jumuishi
40.        Mheshimiwa Spika, sambamba na jitihada za kuinua ubora wa elimu nchini, Serikali imeendelea kutafuta suluhu ya changamoto za kujifunzia zinazowakabili wanafunzi wenye mahitaji maalum. Hivi karibuni Serikali imenunua vifaa kwa ajili ya wanafunzi wasioona na wenye baki ya usikivu na kuvisambaza katika shule 213 za msingi na 22 za sekondari. Aidha, Serikali imenunua vifaa vya upimaji ili kubaini watoto wenye mahitaji maalum ya ujifunzaji kwa mikoa yote Tanzania Bara. Rai yangu kwa wazazi wenzangu kote nchini, ni kutumia fursa hii kuwapeleka shuleni watoto wenye mahitaji maalum badala ya kuwaficha majumbani. Shabaha ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila mtoto wa Tanzania mwenye umri wa kwenda shule, anapata fursa hiyo bila kujali uwezo wake wa kifedha au changamoto za kimwili.

Msimamo wa Serikali kuhusu Ujauzito shuleni
41.        Mheshimiwa Spika, moja kati ya mijadala iliyoibua hisia kali wakati wa mjadala wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ni pamoja na kuwaachisha masomo wanafunzi waliopata ujauzito shuleni. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015, jumla ya wanafunzi 3,637 waliacha masomo kutokana na kupata ujauzito. Kuwaachisha masomo wanafunzi waliopata ujauzito, ni utekelezaji wa Waraka na Kanuni za Elimu za Mwaka 2002 zinazohusu kufukuza na kuondoa wanafunzi shuleni kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo uasherati, wizi, ulevi, kutumia dawa za kulevya pamoja na utoro unaotokana na baadhi ya wanafunzi kwenda kufanya shughuli za biashara ndogo ndogo, kucheza kamali, kuvua samaki, kuchimba madini, n.k.

42.        Mheshimiwa Spika, msimamo wa Serikali wa kutoruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kuendelea na masomo katika mfumo rasmi wa elimu ni kwa mujibu wa sheria na wala sio utaratibu mpya kama inavyopotoshwa na baadhi ya wanaharakati. Msimamo huo wa kisheria unalenga kuwafanya watoto wa kike wajishughulishe na masomo yao badala ya kushiriki kwenye vitendo vya ukiukwaji wa maadili. Lengo hili pia nalo ni la kuwaelimisha wazazi kila mmoja aendelee kumtunza binti yake na kuwafundishe watoto wao mambo mema na maadili mema ndani ya familia. Wazazi wajishughulishe kikamilifu katika kuweka katazo kwa watoto kujihusisha na ngono wakiwa na umri mdogo. Dhamira ya Serikali ni kumlinda mtoto wa kike ili apate elimu kwa ajili ya manufaa yake na Taifa kwa ujumla. Sote tutakumbuka kaulimbiu ya mke wa Rais wa awamu ya nne, Mama Salma Rashid Kikwete aliyesema: “Mtoto wa mwenzio ni mwanao.” Kila mzazi hana budi kujikita kuwalea watoto hawa badala ya kuwafanyisha vitendo ambavyo havistahili.          

43.        Mheshimiwa Spika, kila Mtanzania ana wajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wetu wanapata elimu. Hivyo, ni lazima tuhakikishe mtoto wa kike anapata elimu stahiki na masomo yake hayakatizwi kwa kupata ujauzito. Serikali imewekeza kwenye mtoto wa kike. Kifungu Na. 60 (b) cha Sheria ya Elimu Sura ya 353, kinatoa adhabu ya miaka 30 jela kwa yeyote atakayeoa au kumpa ujauzito mwanafunzi. Aidha, sheria inatoa adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela au faini ya Shilingi Milioni 5, au vyote kwa pamoja kwa anayeshiriki kumuozesha mtoto wa shule. Natoa wito kwa Wakuu wa Wilaya kusimamia utekelezaji wa sheria za nchi zenye lengo la kumlinda mtoto wa kike. Aidha, nawashauri Waheshimiwa Wabunge, mshirikiane na Halmashauri zenu kuweka mikakati ya kudhibiti ujauzito kwa watoto wa shule. Wahamasisheni wananchi watoe ushirikiano kwa vyombo vya dola, ili wanaowapa wanafunzi ujauzito au kuwakatisha masomo ili waozeshwe wapate adhabu stahiki.

SEKTA YA MAJI

44.        Mheshimiwa Spika, katika mjadala wa Bajeti moja ya sekta ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi walionesha kwamba inahitaji kupewa kipaumbele cha pekee ni sekta ya maji. Hakika nakubaliana na mtazamo huo wa Waheshimiwa Wabunge kwani maji ni uhai na kichocheo cha maendeleo katika sekta mbalimbali na nyenzo muhimu katika mapambano dhidi ya umaskini. Kwa kuwa suala la maji lilitolewa ufafanuzi wa kina na Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, naomba Waheshimiwa Wabunge watuelewe kwamba tumewasikiliza na tumewasikia. Serikali inayo nia ya dhati kuhakikisha kwamba vijiji zaidi vinapata huduma ya maji.

UBORESHAJI WA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA NCHINI
45.        Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuhakikisha kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini zinatimiza malengo ya kuanzishwa kwake kwa mujibu wa Ibara ya 145 na 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977. Miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuendeleza juhudi za ugatuaji wa madaraka kwenda katika vyombo hivyo pamoja na kuongeza mgawo wa fedha za ruzuku ya maendeleo inayopelekwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

46.        Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma hiyo, Serikali katika mwaka 2017/2018 imetenga kiasi cha shilingi bilioni 412.38 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo:-

(i)                Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 16.985 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya majengo ya Ofisi na Makazi ya Viongozi katika Mikoa yote mipya. Katika mgawo huo, Mkoa wa Njombe umetengewa jumla ya shilingi bilioni 3.34; Mkoa wa Katavi umetengewa jumla ya shilingi bilioni 3.080; Mkoa wa Simiyu umetengewa jumla ya Shilingi Bilioni 3.775, Mkoa wa Geita umetengewa jumla ya shilingi bilioni 2.978 na Mkoa wa Songwe umetengewa jumla shilingi bilioni 3.812.

(ii)               Aidha, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 61.7 kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri 64, Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 28.7 ni kwa ajili ya kukamilisha majengo ya Ofisi katika Halmashauri 44 na shilingi bilioni 33 ni kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri mpya 20.
Kwa sasa Serikali haina mpango wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala mpaka tukamilishe maeneo tuliyoyaanzisha kwa kuboresha miundombinu.

(iii)             Sambamba na hatua hizo, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto imetoa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa vyenye thamani ya shilingi bilioni 2.9 pamoja na kununua magari ya kubebea wagonjwa katika Halmashauri 67.

(iv)             Vilevile, Serikali imeandaa mpango mahsusi wa kuwajengea uwezo Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Watendaji wa Kata, Vijiji, Mitaa na Vitongoji ili waweze kutoa huduma bora na kwa ufanisi katika kuwahudumia wananchi. Sehemu ya fedha za maendeleo zitatumika kwa ajili ya kujenga uwezo wa watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.
47.        Mheshimiwa Spika, juhudi za Serikali za kuimarisha utendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa zina lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi na kutatua kero zao katika ngazi hiyo. Aidha, jitihada hizo zimelenga kuongeza kasi ya maendeleo Vijijini na kuboresha maisha na ustawi wa wananchi wetu. Kwa msingi huo, natoa wito kwa Viongozi wa Mikoa na Wilaya pamoja na Halmashauri, wahakikishe kwamba malalamiko yote ya wananchi yanatatuliwa haraka katika ngazi husika. Si vyema na haikubaliki kwa wananchi kusafiri umbali mrefu kutafuta suluhu za changamoto zao kwa viongozi wa Kitaifa wakati wa Mamlaka za Serikali za Mitaa zipo, na zina Viongozi wanaolipwa mishahara kwa fedha za walipa kodi. Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wa maagizo yanayotolewa kuhusu suala hili.

MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA

48.        Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na mapambano dhidi ya uzalishaji, uuzaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya nchini. Tumeendelea kubaini mtandao wa waingizaji wa dawa hizo hapa nchini na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahalifu hao. Ili kuimarisha mapambano hayo na kuyaendesha kisayansi, Serikali imekamilisha uteuzi wa watendaji mahiri wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya wanaojumuisha makamishna wanne waliobobea kwenye taaluma zao na wenye uzalendo na uzoefu mkubwa kwenye mapambano haya.

49.        Mheshimiwa Spika, Katika kipindi kifupi tangu mwezi Februari, 2017 Mamlaka hii ilipozinduliwa, imefanikiwa kukamata watuhumiwa 4,809 wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroine (gramu 327.173); cocaine (kilo 26.977); bhangi (kilo 18,334.83); mirungi (kilo 11,306.67) na lita 6,338 za kemikali bashirifu zilikamatwa bandarini. Aidha, Mamlaka kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi za Mikoa imefanya operesheni za kuteketeza ekari 569.25 za mashamba ya bhangi na ekari 64.5 za mashamba ya mirungi na kazi hiyo inaendelea. Kutokana na hatua hizo, jumla ya majalada ya kesi 3,222 yamefunguliwa.

50.        Mheshimiwa Spika, dawa za kulevya zina athari kubwa kwa ustawi wa familia zetu na Taifa kwa ujumla. Hivyo, napenda kurejea wito wangu kwa Watanzania wote kuunga mkono jitihada za Serikali katika mapambano haya kwa kuendelea kutoa taarifa kuhusu watu wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Aidha, naendelea kutoa rai kwa wazazi wenzangu kufuatilia mienendo ya watoto wetu ili wasijiunge katika makundi mabaya ya kujihusisha na dawa za kulevya. Itakumbukwa kwamba waathirika wakubwa wa dawa za kulevya ni vijana wenye umri kati ya miaka 15-35, kundi ambalo ni tegemeo kwa ustawi wa Taifa letu.

51.        Mheshimiwa Spika, Azma ya Serikali ya awamu ya tano ni kutokomeza kabisa mtandao wa dawa za kulevya nchini kwa kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanakuwa endelevu, yanafanyika kisayansi na yanaleta mafanikio. Tuungeni mkono kwenye mapambano haya, ili itokomeze kabisa mtandao huo.

SEKTA YA MICHEZO

52.        Mheshimiwa Spika, wakati vikao vya Bunge hili vikiendelea, tmu yetu ya vijana walio chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys ilishiriki na kutoa upinzani mkubwa kwenye mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika ambapo ilimaliza ikiwa na jumla ya pointi 4 sawa na timu iliyoshika nafasi ya pili. Hata hivyo, kutokana na kanuni za mashindano hayo, Serengeti Boys haikuweza kuendelea na mashindano pamoja na matokeo hayo mazuri.

53.        Mheshimiwa Spika, binafsi nilifuatilia mechi zote za Serengeti Boys nikiri kwamba, vijana hao wana vipaji na uzalendo wa hali ya juu kwa nchi yao. Kwangu mimi vijana wale ni washindi bila hata ya kupewa taji lolote. Naomba nitumie Bunge lako tukufu, kuwapongeza kwa dhati kudhihirisha kwamba hakuna linaloshindikana tukiamua. Msisitizo wangu kwa TFF ni kuendelea kuwatunza vijana hao, na kusimamia vilabu vya michezo nchini kuwekeza kwenye soka la vijana ili tujenge timu imara kwa miaka michache ijayo.

54.        Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa michezo kwa afya, umoja wa kitaifa na kama fursa ya ajira kwa vijana wetu. Wiki iliyopita, mkoani Mwanza yamehitimishwa mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA. Wananchi wa Mwanza na Watanzania kwa ujumla wamejionea uwezo wa kimichezo, vipaji na hamasa kubwa iliyopo miongoni mwa vijana wetu kutumia vipaji vyao. Hivyo, tutaendelea kuratibu michezo shuleni, ikiwa ni pamoja na kusimamia ufundishaji wa michezo kama somo. Maelekezo yetu ni kwamba kila Mkoa uwe na shule angalau mbili zenye mchepuo wa michezo na walimu wenye sifa stahiki za kufundisha michezo. Nawapongeza sana Walimu wetu kwa kusimamia vizuri michezo shuleni. Nitumie fursa hii kuagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini, wahakikishe kwamba kila shule inakuwa na viwanja vya michezo mbalimbali ili kuwapa fursa wanafunzi kushiriki michezo ili kupandisha na kuinua vipaji vyao, na walimu wanahimizwa wasimamie michezo mbalimbali shuleni.

55.        Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuwashukuru wadhamini waliodhamini michezo yetu ya UMITASHUMTA na UMISSETA mwaka huu wa 2017 ambao ni Coca Cola, LAPF na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa mchango wao mkubwa.

56.        Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuunga mkono jitihada za michezo nchini kwa dhamira yake ya kujenga uwanja mkubwa wa michezo hapa mjini Dodoma kwa kushawishi mataifa rafiki kama vile Morocco ambao wanajenga uwanja huo.

Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kusimamia michezo nchini na haitafumbia macho usimamizi mbovu, na utawala wa michezo usiojali maslahi ya Taifa. Serikali imeazimia kuimarisha utendaji kwa vyombo vya michezo nchini ili kila mwenye dhamana awajibike ipasavyo. Kwa msingi huo, leo hii naelekeza kwa Waziri mwenye dhamana ya michezo nchini kulifanyia mapitio na kutathmini upya Baraza la Michezo Tanzania (BMT) ili kujiridhisha na usimamizi wake wa shughuli za michezo nchini. Pale itakapodhirika kwamba usimamizi siyo imara, anayo ruhusa ya kulivunja Baraza hilo na kuunda Baraza jipya.

HITIMISHO

57.        Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha hotuba yangu, naomba nirejee masuala makubwa niliyoyasisitiza wakati nafungua Mkutano wa Saba wa Bunge lako tukufu. Masuala hayo niliyoyasisitiza, ambayo naamini bado yana umuhimu hadi sasa kwa ustawi wa nchi yetu ni kama ifuatavyo:-

(i)         Moja, tuendelee kulinda na kudumisha amani nchini ili wananchi washiriki shughuli za maendeleo bila hofu ya usalama wao.

(ii)        Pili, jukumu la kujenga uchumi wa nchi yetu ni wajibu wa kila mwananchi. Ni lazima kila mwananchi afanye kazi kwa bidii na maarifa, alipe kodi stahiki na afichue wanaokwepa kulipa kodi.

(iii)      Tatu, tujenge utamaduni wa kupima afya zetu na kufanya mazoezi ya viungo ili kujilinda na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo yanaigharimu sana nchi yetu;

(iv)      Nne, tuepuke matumizi mabaya ya rasilimali zetu kama vile maji, madini na misitu ili zinufaishe kizazi chetu na vizazi vijavyo;

(v)        Tano, tuzingatie matumizi ya muda, tuongeze nidhamu na uwajibikaji tuzingatie muda na kupiga vita tamaduni zote zinazohamasisha uvivu na uzembe; na

(vi)      Mwisho, dawa za kulevya ni janga kubwa linaloitafuna kwa kasi nguvukazi ya nchi yetu. Tunahitaji ushiriki wa kila mmoja katika vita hii kwa kufichua mtandao wa wahusika wa dawa za kulevya.

58.        Mheshimiwa Spika, nihitimishe hotuba yangu, kwa kuwatakia safari njema Waheshimiwa Wabunge wanaporejea majimboni kuwaeleza wananchi mambo mengi yaliyojiri hapa Bungeni hususan kuhusu manufaa ya Bajeti na miswada tuliyoipitisha. Waelezeni wananchi matarajio yetu kwao na kuwasihi waendelee kutuunga mkono kwenye jitihada zetu za kuwawekea mazingira wezeshi ya kujikwamua na umaskini. Serikali inaendelea kusisitiza ushirikiano baina ya Waheshimiwa Wabunge na Halmashauri zenu, katika ufuatiliaji wa fedha za maendeleo tunazoleta kwenye Halmashauri, ili zifanye kazi iliyokusudiwa. Aidha, naitakia maandalizi mema Timu yetu ya Bunge itakayoshiriki kwenye mashindano ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yatakayofanyika mwaka huu mjini Dodoma. Tunayo imani kubwa na Timu yetu, tuwakilisheni vizuri, kama ilivyo kawaida.

59.        Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, napenda kutoa hoja kuwa Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 05 Septemba, 2017 siku ya Jumanne, Saa 3:00 asubuhi litakapokutana katika ukumbi huu hapa Dodoma.

60.        Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.



No comments: