Wednesday, July 12, 2017

DOKTA PHILIP MPANGO AWAHAKIKISHIA WAMACHINGA KUWEKEWA MAZINGIRA MAZURI YA BIASHARA


Na Benny Mwaipaja, WFM-Dar es Salaam
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amewahakikishia wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga kwamba Serikali itaendelea kuwawekea mazingira mazuri ya kufanyia biashara zao ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Dkt. Mpango ametoa kauli hiyo baada ya kukagua zoezi la usajili wa wafanyabiashara hao linaloendelea katika katika Ofisi za TRA wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam ambapo ameshuhudia idadi kubwa ya wafanyabiashara hao wakiwemo waendesha bodaboda, mamalishe na wauza bidhaa mbalimbali wakiendelea kujisajili ili wapate vitambulisho.
“Ndio maana tumeona tuweke utaratibu wa kuwaandikisha na tuwapatie vitambulisho hatimaye tuweke mpango maalumu wa kuwapatia maeneo rasmi ya kufanyiabiashara zenu badala ya kila siku kuwatumia askari mgambo kuwafukuza wakati mnatafuta riziki” alisema Dkt. Mpango.
Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuwawekea wafanyabiashara hao wadogo utaratibu mzuri ii waendelee kufanya kazi zao za kujenga familia na Taifa kwa ujumla bila bughudha kwa kuwa Serikali inathamini mchango wao katika uchumi na maendeleo ya nchi.
“Ni lazima ifike mahali kila mtanzania achoke na umasikini, na sisi Serikali yenu tufanyekazi ya kuwasaidia kujikwamua kiuchumi badala ya kuwakandamiza” aliongeza Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango amesema nchi ya Sweden imeweka utaratibu mzuri wa masoko maalumu kwa ajili ya wamachinga wao kila siku za Jumamosi na Jumapili ambapo watu wengi hufika maeneo hayo kununua bidhaa hali inayoashiria kuwa suala la uwepo wa wafanyabiashara wadogo wadogo ni la nchi nyingi duniani.
“Nawasihi mkawaeleze Watanzania wengine na wafanyabiashara ndogo ndogo wenzenu wajitokeze kwa wingi kujiandikisha ili wasajiliwe na kupewa vitambulisho vitakavyowasaidia kujulikana”alisisitiza Dkt. Mpango.
Amerejea kauli yake ya kuwapongeza Watanzania wote kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli kwa kujitokeza kwa wingi kulipa kodi mbalimbali ikiwemo kodi ya majengo kwa kuwa kodi hizo zinaipa Serikali nguvu na uwezo wa kuwahudumia ipasavyo.
“Mkiona barabara zinajengwa, tunaboresha huduma za afya kwa nunua dawa za kutosha, mjue kuwa kodi yenu hiyo kidogo kidogo mnayotoa ndiyo inayotumika kuwezesha mambo hayo kufanyika (makofi)” Alisisitiza Waziri huyo wa Fedha na Mipango
Dkt. Mpango ameahidi kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi na vitendeakazi katika kituo hicho cha uandikishaji ama usajili wa wafanyabishara wadogo wadogo kilichoko katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Ilala Jijini Dar es Salaam ili kufanikisha kazi hiyo.
Kwa upande wao, wafanyabiashara wadogo wadogo hao wameipongeza Serikali kwa hatua waliyoichukua ya kuwatambua rasmi na kuwaingiza katika mfumo wa ulipaji kodi kwa maendeleo ya nchi.
Wamemwomba Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango awafikishie salamu zao za dhati kwa Mhe. Rais Dkt. John Magufuli, kwamba wanamuunga mkono katika jitihada zake za kuwaletea wananchi maendelo na kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi pamoja na kujenga nidhamu ya watumishi wa umma na matunda yake yameanza kuonekana katika uwajibikaji.

No comments: