Na Rajab Mkasaba, IKULU ZNZ
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ameeleza kuwa miongoni mwa changamoto zinazowakabili wateja wa Benki nyingi hapa nchini ni msongamano wa wateja pamoja na ucheleweshaji huduma na kuitaka Benki ya CRDB kuwa na mikakati katika kupambana na kadhia hiyo.
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko Chake Chake
Pemba, katika sherehe ya ufunguzi wa Tawi jipya la Benki ya CRDB likiwa Tawi la
280 ndani ya mtandao wa benki hiyo kutoka matawi 19 iliyokuwa nayo mara tu
baada ya kuanzishwa mnamo mwaka 1996.
Katika hotuba yake, Dk. Shein alisema kuwa
wananchi wanaeleza kwamba, miongoni mwa changamoto zinazosababisha msongamano
ni kuwa benki za hapa nchini bado haziendani na kasi ya mabadiliko yanayotokea
katika sekta ya fedha.
Alieleza kuwa katika Siku ya Sherehe za
Maadhimisho ya Mei Mosi, mwaka huu yaliyofanyika katika viwanja vya Mahonda,
Unguja, Wafanyakazi walipendekeza kuwa Serikali ikae na uongozi wa benki mbali
mbali ili ione namna ya kupunguza kero hii kubwa ya msongamano na kuchelewa
kutolewa huduma, hasa ifikapo mwisho wa mwezi.
“Leo nimeona ni busara nikuleteeni mawazo hayo ya
wafanyakazi, ambao pia, ni baadhi ya wateja wa benki zenu. Wahenga wanasema
‘Mjumbe hauawi’ ndio maana na mimi nimeufikisha ujumbe kama nilivyoambiwa”,
alisema Dk. Shen.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa ni matumaini yake
kuwa CRDB, itakuwa na mikakati imara ambayo itaweza kupunguza msongamano wa
ucheweleshaji wa huduma katika matawi yake.
Dk. Shein aliongeza kuwa miongoni mwa sifa za
Watanzania ni kuwa wako mstari wa mbele katika kutafuta huduma bora sifa ambayo
imethibitika juu ya namna walivyozipokea huduma za uwekaji, upokeaji na utoaji
wa fedha kwa njia ya mitandao.
Aliongeza kuwa kwa matumizi ya huduma hizo,
Tanzania ni miongoni mwa nchi iliyopiga hatua kubwa na kuwa mfano Barani
Afrika, hivyo wananchi Pmba watajitokeza kwa wingi kufungua akauti na kufuata
huduma wanazozitoa na kuitaka CRDB kuendelea kutoa huduma bora.
Pia, alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa uongozi wa
benki kuendelea kubuni mipango imara ya utoaji wa elimu kwa umma kuhusu umhmu
wa kutumia benki na kuitaka CRDB kuwapa wateja wao na wananchi elimu juu ya
umhimu wa kuweka akiba, kukopa, kurejesha na kufanya shughuli za malipo kupitia
benki.
Dk. Shein alieleza kufurahishwa kwake na Benki ya
CRDB kwa kuwa na utaratibu na mfumo wa kutoa huduma zake kupitia simu za
mkononi, mfumo ambao unawaondolea wananchi ulazimu wa kwenda kwenye matawi ya
benki ili kupata huduma na badala yake hupata huduma zote kupitia simu za
mikononi.
Kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na
wananchi wote wa Unguja na Pemba Dk. Shein alitoa shukurani za dhati kwa Benki
ya CRDB kwa kuchangia madawati 150 yenye thamani ya TSZ milioni 20 kwa ajili ya
skuli za msingi za Chake Chake pamoja na michango kadhaa waliyowahi kuitoa
sambamba na waliyoahidi kuitoa.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa uzinduzi
wa Tawi hilo ni kielelezo cha juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibatr
katika kushajiisha wawekezaji wa ndani na nje kuja kuwekeza katika sekta ya
fedha kwa kutambua kuwa huduma za benki ni msingi muhimu katika mabadiliko ya
kweli katika sekta zote za kiuchumi na kijamii.
Alieleza kuwa CRDB ni miongoni mwa Benki kubwa
katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo, kufunguliwa kwa Tawi la Benki
hiyo kisiwanai Pemba ni habari njema, Pia ni benki yenye kuaminika yenye
ubunifu na kuendesha shughuli zake kwa umakini na umahiri mkubwa tangu
ilipoanzishwa mwaka 1996.
Aliongeza kuwa kukua kwa sekta ya Benki kisiwani
Pemba kutachochea ari na mwamko wa wananchi wa kuwa na utamaduni wa kuweka
fedha na amana zao Benki huku akitoa wito kwa wananchi kujiunga na SACCOS ili
wapate kuongeza nguvu za uzalishaji na kuirejesha mikopo kwa wakati ili na
wenzao waweze kufaidika.
Dk. Shein alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya uvuvi sambamba na hata zilizofikiwa ili wavuvi
pamoja na sekta hiyo izidi kuimarika na kuleta tija kwa wavuvi pamoja na Taifa
kwa jumla.
Mapema Kaimu Waziri wa Fedha na Mipango Salama
Aboud Talib ambaye ni Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira alieleza kuwa
Serikali ya Mapindzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano wake na Benki
hiyo huku akisisitiza haja kwa benki hiyo kushirikiana na ZSTC katika
kuimarisha zao la karafuu.
Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya
CRDB Ally Hussein Laay, alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa kisiwa cha Pemba kimeendelea kujenga uchumi imara na
hivyo kuongeza umuhimu wa kuwa na mfumo thabiti wa fedha na ndio maana CRDB
ikaamua kuanzisha tawi hilo huko Pemba.
Alieleza kuwa katika tawi hilo jipya pamoja na
uwepo wa huduma zote za kibenki ikiwemo akauti, mikopo, bima na ushauri wa fedha
na uwekezaji, benki hiyo pia, imo mbioni kuazinsha huduma maalum inayozingatia
sheria na misingi ya dini ya kiislamu “Islamic Banking”.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dk.
Charles Kimei alisema kuwa ukubwa wa amana za benki hiyo tayari umeshafikia TZS
trilioni 4.1 hadi mwezi Juni mwaka huu 2017 na tayari imeshafungua matawi
katika nchi ya Burundi.
Aidha, alitoa pongezi zake kwa Dk. Shein kwa
mashirikano makubwa inayoyapata Benki hiyo kutoka Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar huku akieleza kuwa mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka jana benki ya CRDB
ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 3.3 kwenye sekta za kilimo,
usafirishaji, utalii, viwanda na ujenzi wa miundombinu.
Alieleza kuwa baadhi ya miradi mikubwa
iliyofaidika na mikopo hiyo ni ujenzi wa uwanja wa ndege wa kisasa wa
Dar-es-Salaam (terminal 3), mradi mkubwa wa umeme vijijini (REA), Ujenzi wa
Soko kuu la Mwanjelwa-Mbeya na mingineyo mingi ikiwemo ya watu binafsi.
No comments:
Post a Comment