Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Mpango, amefanya ziara ya kushitukiza katika Ofisi za Mamlaka ya
Mapato Tanzania-TRA, eneo la Vingunguti Jijini Dar es Salaam na kuagiza
kuongezwa kwa wafanyakazi na vitendea kazi katika ofisi hiyo baada ya
kukuta msongamano mkubwa wa watu waliojitokeza kulipa kodi ya majengo.
Dkt. Mpango ambaye alitumia muda
wake mwingi kusikiliza kero za baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam
waliojitokeza kwa wingi kulipa kodi hiyo, ameiagiza Mamlaka ya Mapato
Tanzania kuongeza wafanyakazi kumi pamoja na mashine za kieletroniki za
kukusanyia kodi pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa kuwahudumia wazee na
watu wenye ulemavu.
“Nimeagiza wafanyakazi waongezwe,
viti 50 kwa ajili ya kutumiwa na wazee pamoja na akina mama wenye
watoto vitaletwa, pamoja na kuongeza mashine za kielektroniki 5 kutoka 3
zilizokuwepo ambapo sasa zitakuwa mashine 8, hatua hii itaondoa
changamoto hii” alifafanua Dkt. Mpango
Amerejea pongezi zake kwa
Watanzania kwa kujitokeza kwa wingi kila mahali nchini kote kulipa kodi
ya majengo akikielezea kitendo hicho kuwa ni cha kizalendo na
kitaisaidia nchi kuondokana na umasikini kwa kuwa itakuwa na uwezo wa
kuwahudumia wananchi wake kikamilifu.
Dkt. Mpango amewahakikishia Wazee
waliotimiza umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea kwamba Serikali
imewaondolea kodi ya majengo kwenye nyumba zao wanazoishi kutokana na
kutambua mchango wao mkubwa katika kulitumikia Taifa wakati wa ujana
wao.
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar
es Salaam waliojitokeza kulipa kodi katika Ofisi hiyo ya TRA,
Vingunguti, wamepongeza utaratibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt
Philip Mpango wa kuwajibika na kutumia muda wake kuwatembelea na
kuwahudumia wananchi na pia wamemmwagia sifa kem kem Rais Dkt. John
Pombe Magufuli kwa hamasa kubwa aliyowapa na kwamba wako tayari kumuunga
mkono kwa hali na mali ili nchi ipate maendeleo kwa haraka
Matukio mbalimbali ya picha
zikionyesha Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango akifanya
ziara za kushitukiza katika maeneo muhimu kwa lengo la kuangalia
utaratibu wa ulipaji kodi mbalimbali hususan ya majengo na vituo vya
mafuta ili kubaini kasoro mbalimbali na kutoa maelekezo masuala muhimu
anayoyabaini ambapo jana alikuwa Kigamboni, Jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment