Saturday, July 15, 2017

CHAMA CHA RIADHA MKOA WA SINGIDA CHASHAURIWA KUZITAFUTIA UFUMBUZI CHANGAMOTO ZINAZZOWAKWAMISHA WANAWAKE KUSHIRIKI MASHINDANO YA RIADHA

CHAMA cha riadha Mkoa wa Singida kimeshauriwa kuangalia uwezekano wa kuzitafutia ufumbuzi baadhi ya changamoto zinazochangia idadi kubwa ya wanawake kutopenda na kisha kutoshiriki kabisa katika mchezo wa riadha.

Akitoa ushauri huo kwenye viwanja vya michezo vya shule ya msingi Tambukareli,wilayani Manyoni,Mkoani Singida,mmoja wa washiriki wa mashindano hayo,Hamida Nasoro alisisitiza kuwa kutokana na idadi kubwa ya wanawake kutohamasishwa kushiriki katika mashsindano hayo,ndiko kulikochangia mashindano ya mchezo huo wa riadha kuwa na idadi ndogo ya washirki.

“Mashindano haya tumeonekana wanawake wachache sana labda ni kwa ajili ya changamoto mbali mbali ikiwemo wanawake wengi kutopenda kujishirikisha katika mchezo wa riadha kunakotokana na ukuaji wao wa umri”alisisitiza Hamida.

Akizungumza na kituo hiki,Hamida hata hivyo hakusita pia kutoa tahadhari kwa wanawake wanaopenda kushiriki katika mchezo huo wa riadha wasijihusishe katika mahusiano ya kimapenzi kwani endapo wataendelea kufanya hivyo,ndoto zao za mafanikio katika mchezo huo zitapotea.
Hata hivyo Hamida alitumia fursa ya mashindano hayo kuwashauri wanawake wasiopenda kushiriki mchezo huo wajenge utamaduni wa kupenda kushiriki mchezo huo ili waweze kulitangaza soko la mchezo huo kwa wanawake.

Kwa upande wake Diana Alphonce kutoka wilaya ya Ikungi pamoja na kuridhishwa na maandalizi ya mashindano hayo ya riadha,lakini hakusita kuwaomba waandaaji wa mashindano hayo,wawahamasishe watu wengi zaidi ili waweze kujitokeza kushiriki mashindano hayo.

Kwa mujibu wa Diana aliwataka waandaaji hao wa mashindano kuangalia uwezekano wa kuwapatia zawadi washindi wa mashindano hayo ili waweze kuwatia moyo watu wasioupenda mchezo huo ili nao waweze kuona umuhimu wa kushiriki.

“Katika mashindano haya wawe wanatutia moyo hata angalau watupatie zawadi hata kidogo ili kumhamasisha yule ambaye hajashiriki ili awe na moyo wa kushiriki”alisisitiza mshiriki huyo kutoka wilayani Ikungi.

Naye mwanamke mwenye umri wa miaka 48 anayeshiriki katika mbio za kilomita 21 na aliyewahi kushiriki katika mashindano ya mbio za nusu marathon,Zainabu Ramadhani aliyataja malengo ya kushiriki katika mashindano hayo kuwa ni pamoja na kujenga mwili,kuwaunga mkono vijana na kuweka reodi nzuri ya ushiriki wake kwenye mchezo wa riadha.
Baadhi ya washiriki wa mashindano ya mchezo wa riadha wa Mkoa wa Singida walioshiriki mashindano hayo yaliyofanyika katika viwanja vya michezo vya shule ya msingi Tambukareli,wilayani hapa.
Mwanamke mwenye umri wa miaka 48,Zainabu Ramaddhani kutoka wilaya ya Ikungi akishiriki mbio za umbali wa kilomita 21 katika mashindano hayo na kufanikiwa kuchaguliwa kwenda kushiriki mashindano ya kimkoa.(Picha zote Na Jumbe Ismailly)

No comments: