Monday, July 10, 2017

Amil Shivji aelezea filamu ya T-Junction iliyofungua pazia tamasha la ZIFF 2017

Mwandishi na Muongozaji wa filamu katika kampuni ya KIJIWENI Production, Amil Shivji ambaye yupo visiwani hapa Zanzibar na ‘crew’ yake ameelezea kwa kina filamu yake mpya na ya pili katika filamu makala ijulikanayo kama ‘T-JUNCTION’ ambayo usiku wa Jumamosi wa Julai 8,2017 imepata kuwa filamu ya kipekee huku ikishuhudiwa na Rais Mstaafu wa awami ya nne, Dkt. Jakaya Kikwete ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo wa tamasha la filamu la Kimataifa la nchi za Jahazi (ZIFF) ambalo mwaka huu linaadhimisha miaka 20, tokea kuanzishwa kwake.

Akizungumza na wanahabari pamoja na wadau wa filamu katika mkutano maalum wa ZIFF, Amil Shivji amebainisha kuwa, T-JUNCTION ni filamu ya pili ya Kijiweni Productions, na amejisikia furaha na thamani kubwa yeye na ‘Crew’ yake kwa mara ya kwanza kuweza kuzinduliwa kidunia kwenye maadhimisho ya miaka 20 ya tamasha la ZIFF mwaka huu kwani ni fursa ya kipekee katika njia ya mafanikio ya filamu hiyo. 

Amil Shivji amefafanua kuwa, T-Junction inawatambulisha mabinti wawili katika tasnia la filamu akiwemo; Hawa Ally (Fatima) na Magdalena Christopher (Maria) huku pia ikishirikisha sura mpya, Mariam Rashid (Mama Fatima), Sabrina Kumba (Mama Maria) akiwemo pia David Msia (Chine) katika jamii wa waigizaji. 
“Mbali na sura hizi mpya katika filamu hii. Pia tumeweza kuchanganya na waigizaji mashuhuri kama Cojack Chilo akiicheza kama Iddi, mkaka mkimya na mwenye imani. Mzome Mohamed (Mangi) na Tin White akicheza kama Shabani mkaka mchangamfu na mcheshi.” Alieleza Amil Shivji.

Shivji ameendelea kufafanua kuwa, Kuhusu Filamu hiyo ya T-Junction ni kisa kinachowahusu mabinti wawili na jamii zao. Jamii moja ikiishi kiholela huku faraja yao ni kujua wana umoja na furaha. 

Jamii yao inazingatia sana mifumo, kanuni na taratibu za utu. Fatima, kigoli mwenye asili ya kihindi na kiafrika amefiwa na baba yake kutokana na pombe. Anashindwa kumuombolezea maana kwa kweli hawakuwa na ukaribu wowote. Hakupata kuwa karibu nae katika uhai wake, waliishi katika giza la utengano. T-Junction ni filamu inayohusu matabaka katika jamii ya Kitanzania. 
Ambapo jamii ya daraja la chini kabisa wanapambana na misukosuko vinavyowakabili ambapo miongoni mwa mambo hayo na mengine yenye visa vya kukufanya ubaki kinywa wazi na hata wakati mwingine kuangusha chozi ama kucheka kwa kufurahia kwa hali ya juu kwani kila muhusika ameweza kuitendea haki nafasi aliyopangiwa. 

Kijiweni Production: Amil Shivji anabainisha kuwa, kupitia kampuni yao hiyo, wameweza kuendelea kupata mafanikio makubwa ya kufanya vizuri kwa filamu zake mbili Shoeshine na Samaki Mchangani na filamu ya Aisha iliyokuwa na mafanikio makubwa.
Hata hivyo, Amil Shivji amewekwa wazi kuwa, kuwa filamu hiyo ya T-junction kutokana na kisa cha kweli kilichotokea eneo la Upanga. Eneo aliloishi tangu kipindi cha utoto wake. 
Ameendelea kuchunguza ukinzani wa matabaka dhidi ya ukuaji wa maeneo ya mjini kwa kasi. 
“Filamu hii imenichukua zaidi ya miaka 6, kuanzia kuifikilia na hata kuchukua maamuzi ya kuiandaa na hadi nikatimiza malengo yangu kwani ilikuwa ipo kichwani mwangu tokea utotoni mwangu na nimeweza kufanya kitu” ameeleza Amil Shivji. 
Shivji ameongeza kuwa, filamu hiyo iliweza kuwakusanya pamoja zaidi ya watu 30 wakiwa ni wenye ujuzi wa sanaa na watu wenye ujuzi tofauti kutoka tasnia ya filamu kwa takribani siku 20, kuanzia mwezi Februari mpaka mwezi Machi mwanzoni huku upigaji picha (shooting) ukifanyika kwenye maeneo tofauti ya Jiji la Dar es salaam. 
“T-Junction ni filamu ambayo kwa hakika inaonyesha vipaji vilivyopo katika tasnia ya filamu Tanzana. Tunajivunia kwamba baada ya maadhimisho ya kidunia katika tamasha la ZIFF, T-Junction itaonyeshwa kwa mara nyingine katika jijini la Dar se salaam (Tanzania Bara) hasa katika kumbi kubwa za sinema ikiwemo Century Cinemax- Mlimani City mwezi wa Agosti mwaka huu, tunawaomba watanzania na watu wote kuweza kujitokeza kwa wingi kuishuhudia filamu hii kwani imejaa mambo mengi na yenye mafunzo” alimalizia Amil Shivji. 
Kwa upande wao washiriki wageni katika filamu hiyo kwa nyakati tofauti wameelezea kuwa katika hali ya furaha kipindi chote kwani wamejiskia furaha kwa kutazamwa na watu wengi kupitia tamasha hilo ambapo wanaamini nyota zao zitaendelea kung’aa zaidi na zaidi kadri siku zinavyoenda na wanaamini hilo itafanya vizuri.
Mwandishi na Muongozaji wa filamu katika kampuni ya KIJIWENI Production, Amil Shivji akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wadau wa masuala ya filamu (hawapo pichani) mapema leo Julai 9,2017 wakati wa mkutano na waandishi wa Habari.
Mwandishi na Muongozaji wa filamu katika kampuni ya KIJIWENI Production, Amil Shivji akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wadau wa masuala ya filamu mapema leo Julai 9,2017 wakati wa mkutano na waandishi wa Habari.
Muigizaji mpya Hawa Ally alietumia jina la Fatuma akielezea namna alivyoweza kuucheza uhusika kwenye filamu ya T-junction. Kushoto ni Mwandishi na Muongozaji wa filamu katika kampuni ya KIJIWENI Production, Amil Shivji mapema leo Julai 9,2017 wakati wa mkutano na waandishi wa Habari.
Mwandishi na Muongozaji wa filamu katika kampuni ya KIJIWENI Production, Amil Shivji akiwatambulisha Hawa Ally (Fatima) na Magdalena Christopher (Maria) mapema leo Julai 9,2017 wakati wa mkutano na waandishi wa Habari.
Amil Shivji akiwa pamoja na 'Crew' yake pamoja na mgeni rasmi Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dkt. Jakaya Kikwete (katikati)
Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na wasanii wa KIJIWENI PRODUCTION mara baada ya uzinduzi wa tamasha la ZIFF 2017.
Amil Shivji (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dkt. Jakaya Kikwete (katikati) na Baba yake Mzazi, Profesa Issa Shivji mara baada ya uzinduzi huo wa tamasha la 20 la ZIFF 2017. (PICHA ZOTE NA ANDREW CHALE).

No comments: