Wednesday, June 7, 2017

Waziri Ummy Mwalimu Azindua Huduma Mpya ya Kupandikiza Vifaa vya Usikivu Muhimbili, apiga Marufuku Wagonjwa Kutibiwa Nje ya Nchi

Serikali imesema kwamba kuanzia sasa haitapeleka wagonjwa nje ya nchi kwa ajili ya kupandikiza vifaa vya usikivu kwa kuwa huduma hiyo imeanza kutolewa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Kauli hiyo imetolewa Leo na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu katika hospitali hiyo wakati akizindua huduma ya upasuaji wa kupandikiza vivaa vya usikivu (Cochlea Implant).
Ummy alisema kuwa huduma hizo zitakuwa zikitolewa Muhimbili kwa sababu ina madaktari bingwa wenye uwezo wa kufanya upasuaji huo na vifaa vya kisasa na kuokoa gharama kubwa ambazo zilikuwa zikitumika awali kupeleka wagonjwa nje ya nchi.
Waziri huyo amesema katika hospitali za umma, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kutoa huduma ya upandikizaji wa vifaa vya usikivu na ya pili kutoa huduma hiyo katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki ikitanguliwa na Kenya.
“Nafarijika Tanzania kuwa nchi ya kwanza kutoa huduma hii kupitia hospitali ya umma ambayo ni Muhimbili yenye hadhi ya ubingwa wa hali ya juu. Wenzetu Kenya huduma hii inatolewa kwenye hospitali binafsi na inakadiriwa kugharimu dola 31,000 za Marekani ambazi ni sawa na Sh69 milioni za Kitanzania. Hivyo basi tuna kila sababu ya kujipongeza kwa hatua tuliyofikia,”
Akizungumzia gharama, Waziri amesema kuwa mgonjwa mmoja itamgharimu Sh36.9 milioni kwa ajili ya upandikizaji wa kifaa cha usikivu na kwamba kutolewa kwa huduma hiyo katika Hospitali ya Muhimbili itasaidia kupunguza gharama za matibabu kwa zaidi ya asilimia 60.
Amesema fedha za matibabu zitakazokuwa zikilipwa Muhimbili zitakuwa zikitumika kulipia matibabu kwa wagonjwa wasiokuwa na uwezo. “Ikumbukwe kwamba serikali ilikuwa ikigharamia Sh80 milioni hadi 100 kwa ajili kupandikiza kifaa cha usikivu kwa mtoto mmoja aliyekuwa akipelekwa kutibiwa nje ya nchi,”amesema.
Ummy amesema kuwapo kwa huduma hizo nchini kutawawezesha Watanzania wengi kutibiwa na kuipunguzia serikali gharama ya kupeleka wagonjwa nje kutibiwa na kwamba gharama zitapungua kwa zaidi ya asilimia 60.
Waziri huyo amesema kuwa wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kifedha watapatiwa huduma hiyo kupitia sera ya msamaha kwa watu wasiokuwa na uwezo. “Hospitali ya Muhimbili ina utaratibu mzuri wa kutoa huduma kwa wagonjwa wote wasiokuwa na uwezowa kulipia. Ni vyema wananchi wakatumia utaratibu  huo badala ya kukimbilia kwenye vyombo vya habari kulalamika,” amesema waziri huyo.
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa siku mbili mfulilizo kuanzia tarehe 5 hadi 6 Juni, 2017 kwa kushirikiana na wataalamu kutoka India na Misri wamefanikiwa kufanya upasuaji kwa watoto watano ambao walizaliwa wakiwa na matatizo ya kutosikia.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru amesema kuwa tatizo la usikivu limekuwa likiongezeka katika jamii na kwamba endapo watoto watabainika kuwa na tatizo hilo mapema na kuwekewa vifaa  vya usikivu (Cochlear Implant) wataishi kama watu wengine ambao hawana matatizo na kwamba wasipowekewa vifaa hivyo watakuwa viziwi. “ Ufafiti wa Hospitali ya Muhimbili unaonyesha kuwa kwa mwaka karibu watoto 300 hadi 400 wanahitaji huduma hii hapa nchini. Tunaamini kuwa kuanzishwa kwa huduma hii nchini itawanufaisha wengi,” amesema Profesa Museru.
Profesa Museru ameomba Muhimbili iungwe mkono katika juhudi zake za kuboresha huduma na kwamba iwapo mpango wa kupata madaktari na wauguzi kutoka Cuba utakapokamilika utasaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje.
“Tunaomba Serikali itufikirie sisi Muhimbili katika kuwezesha huduma hizi kuwa endelevu kwa kutenga kiasi cha fedha za kutosha ili kuwalipia Watanzania ambao wanahitaji huduma ya upandikizaji wa vifaa vya usikivu,” amesema Profesa Museru Leo.
Pia, Profesa Museru amefafanua kuwa gharama zilizotumika kwa ajili ya kukarabati, ununuzi wa vifaa tiba, kusomesha wataalamu nje ya nchi, kupanua miundombinu ya utoaji huduma zimegharimu jumla ya Sh13.664 bilioni na kwamba Sh8.855 bilioni zilitumika kununua vifaa vya tiba, Sh 3.858 kwa ajili ya ukarabati na Sh850 milioni kwa ajili ya kusomesha wataalamu.

No comments: