Thursday, June 22, 2017

WATOTO NA VIJANA WA KAMBI YA ARIEL WATEMBELEA MAKUMBUSHO YA KISUKUMA – BUJORA MWANZA


Watoto na vijana 50 kutoka mikoa ya Geita,Mwanza na Shinyanga wanaoshiriki katika kambi ya Ariel 'Ariel Camp 2017’  jijini Mwanza iliyoandaliwa na shirika la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi, wametembelea makumbusho ya kabila la Kisukuma   ‘Sukuma Museum’ ya Bujora Kisesa Mwanza ili kujifunza tamaduni na mila za Kisukuma. 
Kambi ya Ariel imeanza Juni 19,2017 itafungwa Juni 23,2017 ambapo washiriki wanajifunza mambo mbalimbali ikiwemo afya ya ujana na makuzi, lishe, stadi za maisha, elimu sahihi kuhusu VVU na Ukimwi,kushiriki katika michezo sambamba na kubadilishana mawazo. 
Katika siku ya tatu ya kambi hiyo,Jumatano Juni 21,2017 ,watoto na vijana hao walitembelea Makumbusho ya Kisukuma ya Bujora na kucheza michezo mbalimbali katika ufukwe wa Ndorosi katika ziwa Victoria. 
Watoto na vijana hao wakiwa wameambatana na watumishi wa afya,madaktari wa watoto na wafanyakazi wa AGPAHI walijionea zana mbalimbali zinazotumiwa na wasukuma katika maisha yao ya kila siku pia walijifunza historia ya wasukuma. 
Makumbusho ya Kisukuma ya Bujora yalianzishwa mwaka 1968 na padre David Clement Fumbuka aliyeamua kukusanya mabaki mbalimbali ya zana za Kisukuma na kuandika historia ya wasukuma. 
Mwongozaji wa wageni katika makumbusho hayo,Yasinta Salum alisema Fumbuka aliyekuwa raia wa Canada mwenye asili ya Ufaransa alifika kanda ya ziwa mwaka 1952 na kuanzisha chama cha Mtakatifu Sesilia ambacho kazi yake ilikuwa ni kuimba nyimbo za Kilatini kisha kuzitafsiri kwa lugha ya Kisukuma lengo likiwa ni kuangalia namna ya kuchanganya masuala ya dini na utamaduni. 
“Mwaka 1958 ,Padre Fumbuka alifungua kanisa Katoliki hapa Bujora kisha akapata wazo la kuanzisha makumbusho,akaanza kukusanya mabaki ya zana za Kisukuma na kuandika historia ya wasukuma na kufanikiwa kufungua makumbusho haya mwaka 1968”,alieleza Yasinta. 
Alisema makumbusho hayo yamesheheni mambo kadha wa kadha ya wasukuma ikiwemo historia ya falme za kisukuma,utawala wa machifu wa kisukuma,familia za kisukuma na nyumba zao,ngoma na zana walizokuwa wanatumia katika maisha yao ya kila siku. 
ANGALIA HAPA PICHA ZA MATUKIO WAKATI WATOTO NA VIJANA WA KAMBI YA ARIEL WAKITEMBELEA MAKUMBUSHO YA KISUKUMA - BUJORA MWANZA

 
Bango linaloonesha makumbusho ya Kisukuma ya Bujora Mwanza,pichani kushoto ndiye mwanzilishi wa makumbusho hayo David Clement Fumbuka aliyezaliwa mwaka 1922 na kufariki dunia mwaka 1986.
Mwongozaji wa wageni katika makumbusho ya Kisukuma Bujora ,Yasinta Salum akielezea historia ya makumbusho hayo kwa watoto na vijana kutoka mikoa ya Shinyanga,Geita na Mwanza walioshiriki katika Kambi ya Ariel jijini Mwanza.
Yasinta akiendelea kutoa historia ya Makumbusho ya Bujora.
Baada ya kuwapatia historia ya Makumbusho ya Kisukuma Bujora,Yasinta akaanza kuwatembeza wageni wake katika makumbusho hayo.
Mwongozaji wa wageni katika makumbusho ya Kisukuma Bujora ,Yasinta Salum akielezea kuhusu chama cha Mt. Sesilia kilichoanzishwa na Padri David Clement Fumbuka na viongozi wengine wa kanisa katoliki waliofika katika makumbusho hayo.
Watoto,vijana na watumishi wa afya walioambatana na watoto hao wakimsikiliza Yasinta
Yasinta akionesha zana zilizokuwa zinatumiwa na wasukuma katika maisha yao ya kila siku.Hapo kuna zana za kuwashia moto,kuyeyushia chuma na vinginevyo.
Yasinta akionesha zana ya kuwashia moto 'ulimbombo'.
Hapa ni nje ya nyumba iliyokuwa inatumiwa na wahunzi.
Yasinta akiwaonesha wanakambi kifaa kwa ajili ya mchezo wa bao.
Yasinta  akionesha ramani inayoonyesha jinsi falme za Kisukuma zilivyokuwa.
Sehemu ya ramani ya falme za Kisukuma ikionyesha majina ya machifu.
Yasinta akionesha kifaa kinachotumika kuhesabu namba kwa lugha ya Kisukuma.
Watoto na vijana wakipanda katika eneo la kutunzia ngoma za Kichifu.
Yasinta akionesha ngoma zilizokuwa zinatumiwa na Machifu wa Kisukuma.
Kijana muelimisha rika akipiga ngoma ya Kichifu.
Mfano wa nyumba ya Kisukuma.
Nje ya nyumba ya Kisukuma  na vitu mbalimbali ambavyo lazima utakutana navyo ambavyo ni pamoja zizi la ng'ombe na maghala ya chakula.
Haya ni mawe yanayotumika kusagia nafaka  katika familia za Kisukuma.
 Hapa ni ndani ya nyumba ya Msukuma na vitu mbalimbali 
Vijana wakiangalia vitu mbalimbali vinavyopatikana katika nyumba ya msukuma.
Vijana wakiangalia vyungu katika familia ya Msukuma.
Hii ni nyumba ya mganga wa kienyeji/Mganga wa Kisukuma.
Vijana wakiangalia vitendea kazi vya mganga wa kienyeji alivyohifadhi ndani ya nyumba yake.
Vijana wakiangalia vibuyu vya mganga wa kienyeji.
Vijana wakiangalia ngozi za wanyama zinazotumiwa na mganga wa kienyeji.
Kikundi cha ngoma za asili cha Mt. Sesilia- Bujora kikitoa burudani ya ngoma ya Bhucheye inayochezwa wakati wanawake wanapotaka wachumba na wanawake hao hucheza wakiwa wanasaga nafaka kwenye mawe.
Ngoma ya Bhucheye ikiendelea.
Ngoma ya Sogota ikiendelea.Ngoma hii huchezwa na wasukuma wakati wa mavuno.
Mchezaji wa ngoma ya Bhuyeye akicheza na nyoka.
Mcheza ngoma ya Bhuyeye akiingiza nyoka kwenye kaptura yake.
Mmoja wa vijana kutoka kambi ya Ariel akiwa na mcheza ngoma ya Bhuyeye wakiwa wameshikilia nyoka.
HAPA NI KATIKA UFUKWE WA NDOROSI : Vijana wakionesha mapozi ya Ki Miss.
Vijana wakipiga picha ufukweni.
Watoto na vijana wakicheza mchezo wa kuruka. 
Watoto na vijana wakicheza mchezo wa kujifunza umuhimu wa ushirikiano.
Michezo ikiendelea.
Wafanyakazi wa AGPAHI wakicheza na mmoja wa vijana hao.
Mchezo wa mbio za magunia nao ulikuwepo.
Mchezo wa kuruka kamba ukiendelea.
Michezo inaendelea.
Watoto wakiendelea na michezo.
Watoto wanacheza.
Mchezo wa kubembea ukiendelea.
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog

No comments: