Friday, June 9, 2017

WANANCHI WA IRINGA WAHAMASIKA KUSAJILIWA VITAMBULISHO VYA TAIFA = USAJILI WAANZA RASMI MANISPAA HIYO

Wananchi wa Manispaa ya Iringa, Mkoani Iringa wamejitokeza kwa wingi kusajiliwa Vitambulisho vya Taifa, baada ya zoezi hilo kumalizika katika Wilaya ya Mufindi iliyokuwa na Kata 36 na kuanza rasmi Manispaa ya Iringa. 
Katibu Tawala wa Manispaa ya Iringa ndugu Joseph Chitinka amefanya ziara kukagua maendeleo ya zoezi hilo na kushuhudia mamia ya wananchi waliofurika katika vituo vya Usajili wakijaza fomu za maombi ya Usajili pamoja na kuchukuliwa Picha, alama za vidole na saini ya Kielektroniki. 
Amesema kama viongozi wamefarijika sana kwa namna wananchi walivyojitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo. 
“ Sisi kama Manispaa tumefarijika sana kwa namna wananchi walivyotuunga mkono kwenye zoezi hili kwa kujitokeza kwa wingi na kuacha shughuli zao kuja kusajiliwa. Hii inaonyesha ni kwa namna gani wananchi wanatambua umuhimu mkubwa wa zoezi hili” alisisitiza. 
Zoezi la Usajili na Utambuzi katika Manispaa ya Iringa limeanza rasmi tangu tarehe 08 Juni 2017 kwa wananchi wa Kata za Kitwiru, Ruaha , Igumbilo, Mshindo, Kitanzini, Mivinjeni na Mlandege. Zoezi la Usajili katika Manispaa ya Iringa limepangwa kumalizika tarehe 30 Juni 2017 kabla ya kuanza Usajili katika Halmashauri ya Iringa. Mpango wa usajili katika Manispaa hiyo umepangwa kwa Kata ambapo kila Kata imepangiwa kati ya siku tatu hadi tano za Usajili kutegemeana na idadi ya Watu. 
Usajili wa Vitambulisho vya Taifa unaoendelea mkoani Iringa unahusisha wananchi wote wenye umri wa miaka 18 na kuendelea na Wageni Wakaazi wanaofanya shughuli zao mkoani humo. Katika Wilaya ya Mufindi takribani wananchi 110,000 wamesajiliwa kupata Vitambulisho vya Taifa ambapo kati yao tayari 50,0000 wameshakabidhiwa Vitambulisho vyao. 
Wananchi wanasisitizwa kujitokeza kwa wingi kusajiliwa wakiwa na nyaraka muhimu zinazowatambulisha ikiwa ni cheti cha kuzaliwa, Kadi ya Kupigia Kura, Vyeti vya Elimu ya Msingi na Sekondari, Pasi ya Kusafiria (Passport), Kadi ya Bima ya Afya, kadi ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NNSF, PSPF, GEPF n.k), Nambari ya Mlipa Kodi (TIN) na Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi. 
Takribani wananchi 130,000 katika Manispaa ya Iringa wanatazamiwa kusajiliwa. Mikoa mingine ya Tanzania ambapo zoezi la Usajili linaendelea ni Singida, Arusha, Simiyu, Mbeya,  Dar-es-salaam, Pwani na kwingineko. Wananchi wanahimizwa kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hii kujisajili ili kupata Vitambulisho vya Taifa kwani vitakuwa na matumizi mengi kielektroniki pamoja na kuwatambua wakati wa kupata huduma mbalimbali katika mashirika na Taasisi mbalimbali za Umma. 
 Wananchi wa Mtaa wa Kibwabwa A na B Manispaa ya Iringa wakiendelea na hatua za kujaza fomu za Maombi ya Vitambulisho vya Taifa, wakati Usajili wa Vitambulisho cha Taifa ukiendelea katika Manispaa hiyo. Wananchi mbali na kujaza fomu za maombi papo hapo wanapigwa picha, kuchukuliwa alama za vidole na saini ya kielektroniki ili kukamilisha Usajili wao.
 Baadhi ya wananchi wa Kata ya Kitwilu wakiwa katika kituo cha Usajili wakisubiri kusajiliwa wakati wa zoezi la Usajili wa Vitambulisho vya Taifa.
 Mtendeji wa Kata ya Kitwilu Ndg. Simba Mansul Nyunza akitoa maelezo ya namna zoezi la Usajili linavyoendeshwa katika Kata yake wakati wa ziara ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Iringa Ndg. Joseph Chitinka.
 Watumishi wa NIDA wakiendelea na zoezi
 Mtendeji wa Kata ya Kitwilu Ndg. Simba Mansul Nyunza akitoa maelezo ya namna zoezi la Usajili linavyoendeshwa katika Kata yake wakati wa ziara ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Iringa Ndg. Joseph Chitinka.
 Wakazi wa Manispaa ya Iringa wakiwa katika kukamilisha zoezi la Usajili wa Vitambulisho vya Taifa.
Wakazi wa Manispaa ya Iringa wakiwa katika mistari tayari kwa ajili ya kukamilisha zoezi la Usajili wa Vitambulisho vya Taifa.

No comments: