Monday, June 5, 2017

WAJUMBE WA BARAZA LAAWAKILISHI WAELIMISHWA KUHUSU HOMA YA INI

 Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akitoa maelezo kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika mkutano wa kushajihisha wajumbe hao kuhusu kifua kikuu, Ukimwi na homa ya Ini katika Hoteli ya Ocean View Kilimani Mjini Zanzibar.
 Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid ambae alikuwa Mwenyekiti wa mkutano huo akiufungua rasmi katika Hoteli ya Ocean View (kulia) Mnadhimu wa Baraza  Ali Salim Haji na (kushoto) Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo.
 Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakifuatilia ufunguzi wa mkutano wa kuwashahishaji kuhusu Kifua kikuu, Ukimwi na homa ya Ini uliofanyika Hoteli ya Ocean View Kilimani Mjini Zanzibar.
 Mratibu wa huduma za homa ya Ini Zanzibar Dkt. Sania Shafi akiwaelezea Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi hali halisi juu ya homa ya Ini katika mkutano uliofanyika Hoteli ya Ocean View Kilimani Mjini Zanzibar.
 Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni Rashid Makame Shamsi akitoa mchango katika mkutano huo.
Meneja Kitengo Shirikishi Kifua kikuu, Ukimwi na homa ya Ini Dkt. Farhat Ahmed akijibu maswali ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika mkutano wa kuwashajihisha kuhusu maradhi hayo katika Hoteli ya Ocean View Kilimani Mjini Zanzibar. Picha na Makame Mshenga.

Na Ramadhani Ali – Maelezao Zanzibar
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameshtushwa na idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na homa ya Ini wakati wananchi wengi hawana uelewa juu ya maradhi hayo na Serikali haijaandaa mikakati imara ya kupambana nayo.
Wajumbe hao walieleza hisia zao wakati wakichangia mada ya hali halisi ya homa ya Ini katika mkutano wa kushajihisha wajumbe hao kuhusu maradhi ya Kifua kikuu, Ukimwi na Homa ya Ini ulioandaliwa na Kitengo Shirikishi cha maradhi hayo katika Hoteli ya Ocean View Kilimani.
Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni Rashid Makame Shamsi alisema wakati homa ya Ini inaongoza kwa kusababisha vifo vingi zaidi ikilinganisha na maradhi mengine haikuzungmzwa katika Bajeti ya mwaka huu ya Wizara ya Afya.
Amesema kukosekana taarifa ya homa Ini ndani ya Bajeti ya Wizara huku wananchi hawana uelewa juu ya homa hiyo itapelekea kuenea kwa kasi na kupoteza maisha ya wananchi.
Mwakilishi wa kuteuliwa Ahmada Yahya ameishauri Wizara ya Afya kupitia Kitengo Shirikishi kutoa taaluma zaidi kwa wananchi ili kuwa na uelewa mpana wa homa ya Ini na njia za kujikinga nayo.
Spika wa Baraza la Wawakilishi ambae alikuwa Mwenyekiti wa mkutano huo ameishauri Kamati ya Bajeti ya Baraza hilo kuangalia uwezekano wa kukipatia fedha Kitengo Shirikishi cha Ukimwi, Kifua Kikuu na homa ya Ini ili kiweze  kukabiliana nayo.
Mratibu wa huduma za homa ya Ini Zanzibar Dkt. Sania Shafi aliwafahamisha  wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa homa hiyo ni janga kama yalivyo maradhi ya Ukimwi na Kifua kikuu hivyo mashirikiano ya pamoja yanahitajika katika kukabiliana nayo.
Aliwaeleza wajumbe hao kuwa njia kuu za maambukizi ya homa ya Ini ni sawa na zile za maambukizi ya Virusi vya Ukimwi lakini virusi vya homa ya Ini vinakasi zaidi.
Alisema mtu anapopata homa ya Ini hupoteza uwezo wa  kufanyakazi kwa vile  Ini linaharibika na husababisha kupata saratani na hatimae kupoteza maisha.
Aliwashauri vijana kujiepusha kufanya  vitendo vinavyosababisha kupata Virusi vya Ukimwi kwa vile maradhi hayo yanauhusiano mkubwa na homa ya Ini.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya kwa kufahamu athari ya homa ya Ini inaendelea kufanya tafiti na hivi karibu itafungua kliniki katika hospitali kuu ya Mnazimmoja kwa ajili kushughulikia homa hiyo.

No comments: