WAISLAMU Mkoani Tabora wametakiwa kuunga mkono juhudi zilizoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli za kupambana kikundi la watu wachache ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakinufaika na rasilimali ya nchi hii na kuwaacha watu wengi wakiwa maskini licha ya utajiri waliojariwa na Mungu.
Kauli hiyo imetolewa jana mjini Tabora na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Tabora Ibrahim Mavumbi wakati wa futari iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa huo Bw. Aggrey Mwanri.
Alisema kuwa Rais Magufuli haipaswi kuachiwa pekee vita aliyoanzisha , bali anatakiwa kuungwa mkono na watu wote wenye mapenzi mema na nchi hii kwani kiongozi huyo amesaidia kuwafumbua macho na kuona kuwa wameibiwa sana na walikuwa wakiendelea kuibiwa na kikundi cha watu wachache kwa maslahi yao binafsi na sio ya watu wengi.
Sheikh Mavumbi aliongeza kuwa Rais Magufuli ameonyesha mapenzi makubwa kwa nchi yake na wananchi wake na kukwerwa na umaskini wa wananchi wake uliosababishwa na tamaa ya watu wachache waliokuwa wakinufaika wakati nchi ikibaki na mashimo ambayo wakati mwingine yanaweza kusababisha vifo kwa watu kutumbukia ndani yake.
Alisisitiza kuwa sio vizuri kupuuza juhudi kubwa anaozifanya Rais Magufuli kwa kushirikiana na viongozi wenzake za kusimamia rasilimali za nchi na kutetea haki za wanyonge ambao walikuwa wakidhulumiwa na watu wachache kwa maslahi yao binafisi
Sheikh Mavumbi aliongeza kuwa Rais Magufuli anataka kutupeleka ambapo kila raia wa nchini hii atakunufaika na utajiri wa nchi hii ambao wamejariwa na Mungu.
Alisema kuwa Waislamu wa Mkoa wa Tabora wanamueombea dua katika mapambano yake ya kuhakikisha kuwa rasimali ya hapa nchini zinawanufaisha wanyonge na zinaleta maendeleo kwa wananchi wengi na Tanzania kwa ujumla.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw.Mwanri aliwashukuru Waislamu kwa nia yao njema ya kumuombea na kumuunga mkono Rais Magufuli na Serikali yake katika mapambano hayo ya ukumbozi wa kiuchumi kwa wanyonge.
Alisema kuwa vita hiyo ni kubwa ni vema Watanzania wote bila kujali tofauti za dini, kabila , vyama wakashikamana na kumuunga mkono Rais Magufuli ili hatimaye matunda ya vita hivyo yaweze kuwanufaisha watu wengi.
Mkuu huyo Mkoa alisema kuwa Wakazi wa Mkoa wa Tabora wanamuunga mkono na wako nyuma yake katika mapambano hayo na hawako tayari kuona watu wachache wanabeza juhudi hizo ambazo zinalenga kuwakomboa wanyonge.
Naye Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Misheni ya Tabora Newton Maganga aliwaomba wakazi wa Tabora kuwa kitu kimoja katika kukabiliana na matatizo mbalimbali yanayokwamisha maendeleo bila kujali tofauti zao.
No comments:
Post a Comment