Sunday, June 11, 2017

WADAU WA ELIMU WILAYA YA KILWA WAJENGEWA UWEZO KUHAMASISHA UKUSANYAJI WA RASILIMALI ZA NDANI KUBORESHA SEKTA YA ELIMU

Afisa Mradi wa Elimu kutoka TENMET, Bi. Alistidia Kamugisha akifungua mafunzo ya siku tatu na kuelezea juu ya uhusiano wa ukusanyaji kodi na maendeleo katika sekta ya elimu nchini ili kutafuta ufumbuzi wa changamoto za utoaji wa elimu bora hapa nchini kwenye mkutano uliowakutanisha wanachama wa chama cha walimu Tanzania (CWT/TTU) na wadau wa elimu katika wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.
 Afisa kutoka ActionAid Tanzania, Joyce John akitoa mada kuhusu utetezi wa haki za watoto maashuleni kwenye mkutano uliowakutanisha wanachama wa chama cha walimu Tanzania (CWT/TTU) na wadau wa elimu katika wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.
 Mwalimu Khamis Kikwajuni akichangia mada kuhusu haki za watoto mashuleni pamoja na Umuhimu wa ukusanyaji wa mapato ya ndani kuwekeza katika sekta ya elimu kwenye mafunzo yaliyoandaliwa na TENMET wakishirikiana na ActionAid Tanzania.

Mkufunzi wa Mafunzo, Wakili Dominic Nduguru akitoa mada ya uhusiano wa Makusanyo ya Kodi Na Maendeleo ya Sekta ya Elimu kwa baadhi ya wadau na mbalimbali wa elimu kwenye mkutano ulioandaliwa na TENMET wakishirikiana na ActionAid Tanzania uliofanyika katika wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.

 Baadhi ya washiriki wa mafunzo wakiwasilisha kazi zilizofanyika makundi mbalimbali yaliyokuwa yanajadili haki za watoto mashulen, haki za binadamu, ukwepaji na upotevu wa kodi nchini.
  Meneja wa Mradi wa TENMET,  Nicodemus Eatlawe akichangia mada kuhusu mtazamo wa upatikanaji wa elimu, sera na sheria za elimu hapa nchini Tanzania wakati wa Mafunzo ya wanachama na viongozi wa Chama cha Walimu na Asasi za Kiraia waliokutana wilayani Kilwa.

Mwenyekiti wa Chama cha walimu Mkoa wa Lindi, Bw. Bw.  Mlami Seba akifunga mafunzo kwa wanachama wa chama cha walimu Tanzania (CWT/TTU) na wadau wa elimu yaliyoandaliwa na TENMET wakishirikiana na ActionAid Tanzania.
 Baadhi ya wadau wa elimu wakionesha ujumbe
 Picha ya pamoja ya viongozi waliochaguliwa na washiriki wa mafunzo kuongoza Jukwaa La Elimu Kilwa (JEK). 

Katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto za utoaji wa elimu bora hapa nchini leo Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET) wakishirikiana na ActionAid Tanzania wameandaa mkutano uliowakutanisha wanachama wa chama cha walimu Tanzania (CWT/TTU) na wadau wa elimu katika mkoa wa Lindi wilaya ya Kilwa kwa siku tatu ili kupanga mpango kazi wa utetezi na ushawishi wa masuala ya elimu yatakayoleta matokeo chanya kwenye masuala ya elimu hapa nchini.
Mkutano huu ulikuwa ulingazia changamoto zinazoikabili elimu ya msingi hapa nchini ikiwemo upungufu wa vyumba vya madarasa, upungufu wa ofisi za walimu, upungufu wa vyoo vya wanafunzi, uwiano usiokubalika kitaratibu wa mwalimu na wanafunzi, shule nyingine kukosa kabisa mwalimu wa kike, upungufu wa nyumba za walimu, kutokutosha kwa fedha za ruzuku, utegemezi wa bajeti ya nchi unaoathiri pia bajeti ya elimu na kusababisha Serikali kushindwa kugharimia kiufanisi utoaji wa elimu.

Mgawanyo wa ruzuku usiozingatia mahitaji ya wenye uhitaji maalumu, jinsia na mahitaji ya kijiografia na pia shule changa na zile ambazo ni kongwe. Kuwa na mipango ya kibaguzi kwa shule inayofanya vizuri ndiyo inapewa fedha (payment for results- P4R) kutoka mpango wa BRN bila kujali mizania ya usawa wa mazingira kati ya shule na shule. Kukosekana kwa mafunzo kazini kwa walimu, kutopandishwa madaraja walimu na utolipwa kwa wakati stahiki za walimu wanaohamishwa/kustaafu mfano pesa ya usafiri.

Katika majadiliano washiriki walichangia juu Upotevu wa kodi nchini hususani katika sekta ya madini na viwanda ndio chanzo cha kukosa fedha za kutosha kugharimia sekta ya elimu nchini.
Akizungumza leo Afisa Mradi wa Elimu kutoka TENMET, Bi. Alistidia Kamugisha alisisitiza serikali kuimarisha vyanzo vya mapato yetu kama nchi hasa kwa kukusanya kodi stahiki kwa kila mtu anayepaswa kulipa kodi. Ili tuondokane na utegemezi toka kwa wahisani. Kwa bajeti ya elimu 2016/17 takribani bilioni 277 sawa na asilimia 31% ilitarajiwa kukusanywa kutoka kwa wahisani na washirika wa maendeleo. Hata hivyo hadi kufikia mwezi Machi 2017 wahisani walikuwa wametoa kiasi cha shilingi bilioni 132 tu, sawa na asilimia 47.6%. 

Mkufunzi wa Mafunzo, Wakili Dominic Ndunguru akielezea kuhusu ripoti ya utafiti ya shirikisho la dini (Interfaith standing committee) iliyozinduliwa Mwezi Mei mwaka 2017 kwa kuwashirikisha kamati ya kudumu ya Bunge ya Uchumi na Fedha inaliyoonyesha kuwa Tanzania kwa sasa inapoteza takribani dola bilioni 1.83 sawa na Tsh trilioni 4.09 kwa mwaka kupitia misamaha ya kodi, uhamishaji wa fedha nje ya nchi bila kufuata utaratibu, kushindwa kutoza kodi sekta isiyo rasmi na aina nyingine za ukwepaji kodi.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Mkoa wa Lindi, Bw.  Mlami Seba aliwasisitiza wadau wa elimu kutokata tamaa kufanya ushawishi na utetezi wa upatikanaji wa elimu bora nchini na maslahi ya walimu; Wadau wa elimu wanalo jukumu la kuisimamia serikali katika kutimiza wajibu wake. Pia alichanghia Kila mtu akilipa kodi stahiki kadri ya kile anachozalisha na pia serikali iwekeze kuboresha huduma za jamii na hususani sekta ya elimu. 

Washiriki wa mafunzo hayo waliazimia kuanzisha jukwaa la wadau wa elimu wilayani Kilwa kama njia ya kuendeleza kazi ya ushawishi wa haki ya elimu nchini na wilayani kilwa na kama jukwaa la kuongeza ushirikiano. Washiriki walichagua uongozi na kuazimia utakua chini ya uratibu wa Chama cha walimu wilaya ya Kilwa.

No comments: