Na Jonas Kamaleki-MAELEZO.
Zaidi ya vijana wapatao 1230 wametoa siri nzito kwa Maaskofu na Mashekhe kutoka katika Kamati ya Kitaifa ya Maadili , Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini Nchini kufichua mtandao haramu wa watu wanaoendesha mauaji na uhalifu mwingine kwenye mikoa 13, nchini kama njia muhimu ya kumpongeza IGP mpya, Saimoni Sirro.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Askofu William Mwamalanga, siri hiyo imetolewa jana na vijana hao katika siku ya tatu mkutano wa kujenga maadili kwa vijana unao fanyika Mbagala, jijini Dar es Salaam na kuwashirikisha vijana wa madhehebu mbalimbali ya dini kutoka katika mikoa ya Pwani, Tanga, Lindi, Morogoro,Dar es Salaam ambapo wameyataja maeneo ya Mkuranga, Rufiji Kigamboni, Kibiti, Msata, Tanga mjini, Pemba na Unguja kuwa maeneo hatari yanayowajengea vijana imani za kigaidi.
Aidha, Askofu Mwamalanga alisema kuwa vijana 147 wa kiislamu wanaohudhuria mkutano huo wamewataja baadhi ya watu ambao ni hatari na wamekuwa wakieneza elimu ya mauaji kwenye misikiti mbali mbali nchini kwa kuiita Serikali ya Awamu ya Tano jina la katili na kwamba elimu hiyo imesambazwa kwa kasi katika mikoa ya Kagera, Tanga, Mwanza, Arusha, Pemba, Unguja, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Morogoro, Iringa, Singida, Dodoma, Pwani na Kigoma huku vikosi vya vijana vikiandaliwa kufanya mauaji mara baada ya mufungo mtukufu wa Ramadhani kama yale ambayo yamekuwa yakifanywa Mukuranga, Kibiti na Rufiji.
Vijana hao wanamuomba IGP Sirro kuwachukulia hatua kali maafisa wa jeshi hilo ambao wanatumia jeshi kupandikiza Umngiki, na kwamba wana imani na IGP Sirro amabaye kwa mujibu wa hao vijana hatamwangusha Rais Magufuli na watanzania kwa ujumla.
Akifunga Mkutano huo Askofu Mwamalanga amemtaja IGP Sirro kama polisi mahiri wa maadili na jemadali mweledi wa mapambano hivyo amewataka vijana kote nchini kumuunga mkono kwa kuwafichua polisi wote wanaoenzi uhalifu. “Tusipofanya hivyo tutakuwa kama pipa zuri tunalo jaza maji wakati tukijua chini limetoboka”,alisema Askofu Mwamalanga na kuongeza kuwa raia wema ni asilimia 99.9 wahalifu ni 0.1 hii ina maana kuwa ukiondoa polisi wahalifu ndani ya jeshi hilo wahalifu ni wachache mno mitaani watayeyuka wenyewe.
Aidha, Askofu huyo amewahimiza vijana na viongozi wa dini kushiriki kwenye mafunzo hayo kote nchini ili wapewe ufahamu wa elimu ya maadili ya kweli ili wawe walinzi wa taifa na kupenda amani na kuweka uchu wa kuchukia rushwa na kujiwekea mitazamo ya kupenda kazi za baraka.
Kiongozi huyo wa dini amekemea vikali nyumba za ibada kugeuzwa eneo la mafunzo ya uhalifu kwani ni aibu kwa msikiti au kanisa kufanya mafunzo ya kigaidi ndani ya nyumba za ibada kufanya hivyo ni ibada ya sanamu, watu wa jinsi hiyo hawana uhusiano wowote na Mwenyenzi MUNGU ambaye kusudi lake ni kuondoa uovu kwa mwanadamu.
Hivi karibuni yametokea mauaji ya viongozi wa Chama Tawala maeneo ya Kibiti, Mukuranga na Rufiji na kufanya wakazi wa maeneo hayo kuishi kwa wasiwasi na mashaka juu ya maisha yao. Wakati akiipishwa kuwa IGP, Kamanda Simon Sirro alisema kupambana na kuondoa uhalifu kwa kushirikiana na raia wema ni moja ya vipaumbele vyake.
No comments:
Post a Comment