Saturday, June 24, 2017

SERIKALI YAWASHAURI WANANCHI KUTUMIA NJIA MBADALA YA KUPATA HUDUMA ZA KIBENKI

Benny Mwaipaja, WFM-Dodoma 

Serikali imewashauri wakazi wa Wilaya ya Malinyi mkoa wa Morogoro, kutumia njia mbadala kupata huduma za kibenki ikiwemo kupitia simu za mkononi yaani (simbanking) ya CRDB na Banking on the Wheel ya NMB iliyoko Mlimba kwa kipindi hiki ambacho mchakato wa kufungua matawi rasmi ya benki unaendelea. 

Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Malinyi Dkt. Hadji Hussein Mponda (CCM), aliyetaka kujua ni lini huduma rasmi za kibenki zitaanzishwa katika wilaya ya Malinyi ama kama kulikuwa na mpango wa taasisi za fedha kuanzisha huduma za matawi ya benki yanayohamishika (mobile banking) wilayani humo.

Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa, wilaya ya Malinyi ni moja ya wilaya ambazo zinanufaika na mfumo wa utoaji huduma kupitia mawakala wa Fahari Huduma (Malinyi SACCOS na Zidua Waziri Shop) zinazoendeshwa na benki ya ‘CRDB Bank’ ambapo wateja wanapata huduma za kibenki ikiwemo kufungua akaunti, kuweka na kuchukua fedha, kuomba mikopo na kupata ushauri wa huduma za kifedha. 

“Gharama za kuanzisha na kuendesha tawi kuwa kubwa Benki ya NMB na CRDB zinaendelea na upembuzi yakinifu kwa ajili ya kufungua tawi katika wilaya ya Malinyi utakaotoa mwelekeo wa kufungua tawi au la, kwa sababu Tawi linatakiwa liwe endelevu na kujiendesha kwa faida”. Alisema Dkt. Kijaji.

Dkt. Kijaji aliongeza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa wananchi wa Tanzania kupata huduma za kibenki karibu na maeneo yao na kwamba huduma hizo lazima ziwe na faida kwa pande zote yaani kwa mabenki na wateja pia. 

Aidha Dkt. Kijaji alifafanua kuwa mabadiliko ya mfumo wa fedha nchini ya mwaka 1991, yaliitoa Serikali katika uendeshaji wa moja kwa moja wa shughuli za mabenki nchini ili kuruhusu ushindani huru na kuwezesha kuboresha huduma katika sekta ya fedha.

Katika swali la nyongeza Mbunge wa Malinyi Dkt. Hadji Hussein Mponda (CCM), alitaka kujua namna Jeshi la polisi linavyoweza kuwasaidia wakazi wa wilaya hiyo wanaotembea na fedha nyingi kufuata huduma za kibenki mbali na wilaya hiyo ili wasipoteze mali zao.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Serikali imeendelea kuimarisha usalama katika maeneo hayo ili kuweka ushawishi kwa Taasisi za kifedha kuweza kufungua mabenki ili kupunguza changamoto ya huduma za kibenki.

No comments: