Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 27
Juni, 2017 ameagana na wafanyakazi wa iliyokuwa Ofisi ya Rais, Ufuatiliaji wa
Utekelezaji wa Miradi (President’s
Delivery Bureau - PDB) ambao wamehamishiwa katika ofisi na taasisi nyingine
za Serikali kwa ajili ya kuendelea na utumishi wa umma.
Wafanyakazi
hawa ndio walikuwa wakisimamia utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now - BRN).
Mhe.
Rais Magufuli amekutana na wafanyakazi hao Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo
amewashukuru kwa kazi nzuri waliyoifanya wakiwa PDB na amewataka kuendelea
kulitumikia Taifa kwa juhudi na maarifa wakiwa katika ofisi nyingine walizopangiwa.
“Natambua
kuwa nyie ni wafanyakazi wazuri wenye ujuzi na maarifa muhimu kwa ajili ya
Taifa letu. Mmetoa mchango mkubwa mlipokuwa PDB nategemea mtaendelea hivyo na
hata zaidi katika ofisi mbalimbali mlizopangiwa, mkachape kazi kwa kutanguliza maslahi
ya Watanzania” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mkutano
huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
Mhe. Angellah Kairuki na Katibu
Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt.
Laurian Ndumbaro.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na timu ya wataalam wa
masuala ya umeme na ujenzi wa miundombinu ya mabwawa ya maji kwa ajili ya
kuzalisha umeme na kujadiliana nao kuhusu utekelezaji wa mradi mkubwa wa
uzalishaji wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Power
Project) ambao una uwezo wa kuzalisha Megawatts 2,100 za umeme.
Mhe. Rais Magufuli amekutana na
wataalamu hao ikiwa ni utekelezaji wa nia yake ya kuhakikisha mradi huo unaanza
kujengwa haraka iwezekanavyo na kuzalisha umeme mwingi utakaosaidia kuharakisha
maendeleo hapa nchini, hususani ujenzi wa viwanda.
“Kesho Waziri Mkuu wa Ethiopia
Mhe. Hailemariam Desalegn anawatuma wataalamu wake waliojenga mradi
mkubwa wa bwawa la maji la kuzalisha umeme kule Ethiopia, wakiwa hapa mtakutana
nao na mtabadilishana uzoefu, nataka na sisi tusichelewe, tuzalishe umeme
utusaidie kwenye ujenzi wa viwanda” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
IKULU
Dar es Salaam
27 Juni, 2017
No comments:
Post a Comment