Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuashiria Uzinduzi Kitabu cha Mwongozo kwa Wapelelezi na Waendesha Mashitaka wa Kesi za Wanyamapori na Misitu kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, wengine pichani ni Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Profesa Jumanne Maghembe (kulia),Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Bw. Alvaro Rodrigues na kushoto ni Muendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali Biswalo Mganga na Naibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais - Ikulu) Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Naibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni Kitabu cha Mwongozo kwa Wapelelezi na Waendesha Mashitaka wa Kesi za Wanyamapori na Misitu kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, katikati ni Muendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali Biswalo Mganga. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais - Ikulu)Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa Uzinduzi wa Mwongozo kwa Wapelelezi na Waendesha Mashitaka wa Kesi za Wanyamapori na Misitu kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais - Ikulu)
Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii.
Makamu wa Rais Samia Suluhu azindua muongozo kwa watumishi katika kesi za wanyamapori.
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka waendesha mashitaka, polisi na wapelelezi wa kesi za wanyamapori na misitu kubadilika katika kazi zao ili kulinda rasilimali hizo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.Aidha, ameitaka mahakama kutoa muongozo kwa watumishi wake kuhusu namna ya kuendesha kesi zinazohusiana na nyara za serikali kwa lengo la kuwa na uwiano sawa katika utoaji amri.
Samia amesema hayo leo mjini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Mwongozo kwa wapelelezi, waendesha mashitaka na Polisi wa kesi za wanyamapori na misitu ulioandaliwa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).
Amesema wote hao wanatakiwa kufanya kazi zao ipasavyo kuhakikisha usalama wa wanyamapori na misitu kwani kwa kupoteza maloiasili hizo kunafanya uchumi wa nchi kushuka na kwamba wasifanye kazi hiyo kwa kuweka mazingira ya rushwa.
Amesema, kazi za kupeleleza na kuendesha kesi za wanyamapori zimekuwa na ushawishi mkubwa wa rushwa kutoka kwa wahusika na kuwataka kufikiria maslahi mapana ya nchi na sio wao binafsi.
"Jamani, msiogope kufa, kifo kipo na kila mmoja wetu atakufa hata mnyama ikiwemo huyo FaruJohn, muhumu ni namna ya kujua aina ya kifo utakachokufa, lakini Jambo la kusikitisha mmekuwa mkiponzwa na fedha, wahenga walisema 'fedha ni sabuni ya roho lakini pia walisema fedha ni fedheha," amesema Samia.
ameongeza kuwa, Rais Magufuli ana lengo kubwa la kulinda maliasili za nchi hii na kwamba kutaka kwake kuwepo kuwepo kwa miongozo hiyo katika mahakama kutasaidia mahakimu na majaji kutoa adhabu na dhamana zinazowiana.
Ameongeza, mara kadhaa kumejitokeza majaji na mahakimu kutoa adhabu zinazotofautiana au masharti yanayo tofautiana katika kesi zenye mazingira sawa.
Aidha amemtaka DPP kufanya namna ya kuwapeka watumishi hao kwenye mbuga za wanyama, vyanzo vya maji na maeneo ya mbali mbali yenye misitu ili kujionea ni kwa namna gani rasilimali za nchi zinavyopotea kwa wanyama kuuawa kwa kukosa maji.
Amesema, mwongozo huo uliotolewa utasaidia kuboresha upelelezi na uendeshaji wa mashitaka na kwamba mapambano dhidi ya ujangili na uhalifu yatakoma na matokeo chanya yatakuwa yakipatikana katika kesi mbali mbali na serikali kuweza kupata mapato yake katika sekta ya utalii.
Akitoa takwimu za sekta ya wanyamapori, Samia amesema, Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) ya mwaka 2009, ilionesha kuwa Tanzania ilikuwa na tembo 109,051 na sensa ya mwaka 2014 ilionesha idadi ya tembo imepungua na kufikia tembo 43,330 ambao sawa na asilimia 60.3 ya tembo wote.
Alisema sababu kuu ya kupungua kwa tembo hao ni ujangili na kwamba takwimu rasmi za Sekretarieti ya Maktaba wa Kimataifa unaoratibu biashara ya wanyama waliohatarini kutoweka (CITES), ilionesha asilimia 70 ya meno ya tembo yaliyokamatwa duniani kote kati ya mwaka 2008 na 2013, yalitokea Afrika Mashariki nchi za Tanzania na Kenya ambapo kiasi kikubwa kilitokea Tanzania.
Kwa mujibu wa sensa ya Taasisi ya International Union for the Conservation of Nature (IUCN) ya mwaka 2013, Tanzania ilishuka hadi namba tatu kwa idadi ya tembo kwa asilimia 13 ya tembo wote waliopo barani Afrika ikiwa nyuma ya Botswana (asilimia 33) na Zimbabwe (asilimia 16).
Naye DPP Biswalo Mganga amesema katika kipindi cha mwaka 2014 na 2017, washitakiwa 100 walihukumiwa kulipa faini ya bilioni 1.1 na vifungo virefu ambazo tayari imeshalipwa serikalini.Aidha, watuhumiwa 80 walihukumiwa kifungo cha miaka 20 na 30 gerezani na faini ya bilioni 164.7 ambayo bado haijalipwa.
Alisema suala la dhamana kwa makosa makubwa yanayohusu wanyamapori waliohatarini kutoweka ikiwemo tembo na faru, watuhumiwa wengi wamekuwa wakitoroka na kusababisha kesi kutoendelea dhidi yao.
Ameongeza mwaka kati ya 2010 na 2015 mashauri 13 yanayohusiana na nyara za serikali zenye thamani ya milioni 800 yalifikishwa katika Mahakama za Mkoa wa Dar es Salaam lakini watuhumiwa wake walitoweka baada ya kupewa dhamana.
Hata hivyo, alisema asilimia 69 ya watuhumiwa hao ni raia wa kigeni na asilimia 31 ni Watanzania; wakati mahakama inapotoa dhamana, moja ya masharti yake ni kunyang'anywa hati zao za kusafiria.Alifafanua kuwa kati ya kesi hizo 13 watuhumiwa waliua jumla ya tembo 300, chui nane, Kobe 210, twiga,kiboko, pundamilia na ndege wa aina mbalimbali wenye thamani ya milioni 800.
Amesema, takwimu zinaonesha kuwa asilimia 70 ya washitakiwa huruka dhamana na kukimbia kesi pindi wanapopewa dhamana kwa hiyo, anajitahidi kuchukua hatua madhubuti kwenye suala la dhamana hasa kwenye kesi zinazohusu meno ya tembo na faru wanaokaribia kutoweka nchin.
No comments:
Post a Comment