Wednesday, June 7, 2017

MAKALA : ASANTE OMOG,TUMEREJEA ALIKOTUTOA RC LIBOLO

Na Honorius Mpangala.

Mchezo wa soka ni mchezo ambao ili ufanikiwe hauhitaji jitihada za mtu mmoja ila jitihada za timu nzima kuanzia wachezaji,viongozi na benchi la ufundi. Klabu ya Simba imeweza kutembea katika tafsiri hiyo ya mafanikio ya soka yanahitaji ushirikiano wa timu nzima ili kufikia malengo waliyojiwekea.

Ni kitu ambacho wapenzi na wadau wengi wa soka hawajafahamu dhana ya viraka vilivyopo katika mpira na mwisho vinaunda mpira mwenyewe. Viraka vya mpira ni sehemu ya kuelezea muunganiko unaohitajika katika watu ili kuleta mafanikio ya kitu kizima na pia utofauti wa rangi katika viraka huelezea timu mbili tofauti katika uwanja zinazocheza mchezo wenyewe.

Msimu wa 2016/2017 umekua bora sana kwa klabu ya simba na kufanya klabu imalize ligi nikiwa nafasi ya pili na kufanikiwa kubeba kombe la Azam Sport Federation Cup ( ASFC) msimu huu katika fainali Kali dhidi ya Mbao fc ya Mwanza.

Maandalizi ya klabu ya Simba waliyoyafanya ndiyo matunda ya walichokipata na kitawaletea mafanikio zaidi kama wakiendekea nacho kwa misimu mingine inayokuja.

Moja ya eneo ambalo klabu ya simba ilikua na changamoto na kujikuta wanashindwa kujishika vizuri ilikua katika eneo la benchi la ufundi,naweza kusema Benchi la simba limetibiwa ipasavyo.

Joseph Omog huyu mkameruni ni moja ya makocha wazuri na wenye kuamini katika nidhamu ya mchezaji mmoja na baadae nidhamu ya klabu kwa ujumla. Hakuna asiyefahamu mafanikio aliyoyapaya Omog akiwa na klabu Fc Leopard ya Congo Brazzaville alipoifikisha katika fainali ya kombe la shirikisho katika fainali waliyocheza dhidi ya Sc vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Omog alijitangaza katika mashindano ya afrika kama ilivyo kwa George Lwandamina wa yanga alivyojitangaza kupitia Mashindano ya ligi ya mabingwa. Kabla ya ujio wa Omog klabu ya simba ilikua klabu iliyokua ikicheza soka safi lisilo na faida kwao kutokana na upungufu wa nidhamu ya mchezo kupitia utimamu wa mwili na kuhimili mikiki mikiki ya ligi kwa dakika tisini za mchezo.

Omog ni kocha mkali anayejua kusimamia nidhamu,aliondoa hali ya utoto na kuweka mkazo wa kutafuta matokeo kwa faida ya klabu na sio mtu pekee.
Awali ilionekana kama utani wakati simba waenda kuweka kambi yao katika hostel za seminary pale bingwa Morogoro na kuweka mazingira ya kujidhatiti kwa klabu.

Kulikua na utofauti mkubwa kati ya uongozi wa benchi la ufundi chini ya Omog na ilivyokua kwa Jackson Mayanja ambako tuliona mikwaruzano ya chini chini kati yake na wachezaji,mfano kile kilichotokea kati ya Mayanja na Hassan Isihaka na Hamis Kiiza.

Zoezi la usajili walilolifanya kwa upande wa wachezaji walifanikiwa japo sio kwa asilimia kubwa na hilo ni kutokana na aina yetu ya utafutaji wa wachezaji wa kutoka nje ambapo walitumia majaribio.

Usajili wa Javier Belasa Bukungu ulipondwa sana na vyombo vya habari lakini amekuja kuwa thibtishia yeye ni mtu wa tofauti ndani ya uwanja.

Mafanikio makubwa kwa klabu ya simba ilikua pale walipojidhatiti kuivamia mtibwa sugar na kuwasajili Shiza Kichuya,Mzamiru Yassin na Mohammed Ibrahim ilikua usajili bora ambao umeleta matunda kwasababu katika mechi ya FA Mohammed Ibrahim ndo mfungaji wa bao la kuwapeleka fainali na Kichuya akafunga la kuipa Ubingwa wa FA achilia mbali magoli yake mawili ya mechi dhidi ya yanga ambayo yalimtengenezea jina zaidi na zaidi Kichuya.

Wakati ligi ikiendelea na kuona jinsi gani imekua ngumu simba walifanya makosa ambayo hawakuyajua awali kama wanakosea, Safu ya ushambuliaji Ikiongozwa na Laudit Mavugo ilikua inazidiwa magoli na viungo wakiongozwa mzamiru,Mo na Kichuya huku wakiwaacha Mavugo,Fred Blagnon na Ibrahim Ajib wakiwa na idadi ndogo ya magoli.

Simba walimwamini sana Mavugo kuliko Blagnon kwasababu tu mienendo ya uwanjani kati ya hawa wawili ila kiukweli mienendo ya Blagnon inafaida zaidi kuliko Mavugo hii iko wazi ila kinacho mfanya awe nyuma ya Mavugo ni chenga na visigino.

Nafasi na kazi ya Mavugo na Blagnon imenikumbusha hali hiyo kwa Washambuliajj wa kiitalia Fransisco Totti na Alessandro Del Piero. Kazi inayoshindikana kwa Mavugo kwa kipindi cha dakika themanini kiliwezekana kwa Blagnon kwa dakika kumi tu awepo mchezoni.

Dakika kumi za Blagnon ziliamua mechi dhidi ya mbao fc katika Michezo miwili.

Miongoni mwa Michezo ambayo simba walitereza na kuonekana kushindwa kutegua mitego yao ilikua dhidi ya African Lyon mchezo ambao walipoteza dakika za mwisho za mchezo,Mchezo dhidi ya mbeya city jijini Dar es salaam ilikua mtihani kwa klabu ya simba. Endapo benchi la ufundi likaweza kugundua jinsi anavyocheza Mavugo katika eneo la ushambuliaji na kumtazama Blagnon anavyocheza watakua na majibu ya maamuzi katika kuwatumia.

Michezo ya ugenini ambayo ilikua na wakati mgumu dhidi ya Kagera sugar,prisons na Toto Afrika kutokana tu na kujidhatiti wakikofanya wapinzani wao na kutengeneza woga wa safu ya ushambuliaji ya simba kwa kumpa muda mwingi Mavugo ambaye wapinzani walishamgundua aina yake ya uchezaji.

Usajili wa dirisha Dogo kwa kumsajili Athanas Wa stand utd haukua na tija sana kwasababu mtu pekee alitetakiwa kupunguziwa muda wa kucheza ni Mavugo na kupata nafasi Blagnon.

Eneo la kiungo liko bora sana kwa viungo wa kati na tatizo linakuwa kwa mbadala wa Ajib na Kichuya kwa viungo wa pembeni. Uwezo wa Jamal Mnyatte na Athanas sio watu wazuri sana ambao unaweza kusema unaweza kuwatengenezea mzunguko katika kucheza.Ndo maana Alipoyumba Kichuya ilishindikana kwa mnyatte aliyelata nafasi ya kucheza inapobidi.

Mwinyi kazimoto anaendelea kuwa mtu mwenye msaada sana kwa klabu katika kutuliza munkali wa wachezaji na kutafuta matokeo unaweza kupata majibu kwa mechi akizotokea benchi na kucheza kama ilivyo kwenye mechi ya mbao ligi kuu.

Nafasi ya beki simba ilifanya vyema japo Mwalimu alikua akibadilika sana katika nafasi ya walinzi wa kati. Method Mwanjali,Juuko Murshid,Abdi Banda, Javier Besela Bukungu, James Kotei hawa wote kwa nyakati tofauti wamekua wakicheza nafasi hizo na kufanya mwalimu kushindwa kupata pacha iliyo bora zaidi kwake. Majeruhi ya Mwanjali,majukumu ya timu ya taifa ya Uganda kwa Juuko Murshid ni kati ya sababu zilipelekea kuyumba kwa nafasi ya ulinzi na kufanya Mwalimu kufanya mzunguko kwa walinzi wake.

Nini kifanyike kwa msimu ujao.

Yapo mambo machache ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi ndani ya klabu hiyo. Moja, uongozi kupeana majukumu ya klabu kulingana na nafasi kiutendaji na sio kuingiliana katika majukumu hayo kunakotoa mkanganganyiko kwa benchi la ufundi na wachezaji pia.

Tumeweza kujionaea klabu hiyo viongozi wake kila mmoja akitaka kuonekana sana mbele ya vyombo vya habari na kuzungumzia klabu bila utaratibu mazuri na kufanya kila mmoja kuonekana anajitengenezea mazingira ya kuwepo katika nafasi ya uongozi kwenye uchaguzi ujao.

Mbili,Utulivu wa benchi la ufundi uliopo wasije kuutibua na kumfanya bundi akatua katika paa la jengo lao kwasababu ya kutotekeleza matakwa ya kocha baadaa ya kumaliza ligi.

Tatu,ziko nafasi zinazogitaji marejebisho ili kufanya simba kung'ara zaidi kama nafasi ya mlinzi wa kulia wanajitaji mtu wa kusaidiana na Bukungu kwasababu aliyekuwepo kashindwa kumpa changamoto na nafasi hiyo itakuwa bora sana kama wataweza kumshawishi Salum kimenya wa Tanzania prisons kujiunga nao.

Nafasi nyingine ambayo wanapaswa kuifanyia maamuzi ni kutazama upya nafasi ya kiungo mkabaji toka nje ya nchi kwasababu James Kotei ameweza kufit eneo la ulinzi kwa kucheza na Juuko hivyo kumwondoa katika mfumo Method Mwanjali anayeonekana kuwa na umri mkubwa na kushindwa kumudu kasi ya ligi.

Upande wa mlinzi wa kushoto ni eneo ambalo kwao halina matatizo kwani uwepo wa Abdi Banda na Mohammed Hussein ni tiba tosha na kinachobaki ni kutuliza akili zao na kutambua thamani ya mashindano wanayoshiriki hasa kwa banda mwenye vitendo visivyo vya kiungwana mchezoni.

Kwa upande wa nafasi ta ushambuliaji simba wana kila sababu ya kuwatazama vizuri vijana wao waliopita klabu ya simba mbaraka Yusuph na waziri junior,pia wana kila nafasi ya kuwatazama vizuri wachezaji kama Stamili Mbonde wa mtibwa sugar.

Kwa upande wa mchezaji wa nje ambaye anaweza kuondoka ni Method Mwanjali na nafasi yake kuchukuliwa na Kotei na kufanya nafasi ya kumsajili kiungo mkabaji wa kumpa changamoto Jonas Mkude.

@Mido sankala

No comments: