Wednesday, June 14, 2017

MAFANIKIO YA TANZANIA KATIKA NAFASI YA UENYEKITI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

Na. Immaculate Makilika- MAELEZO 

Februari 2015,  Rais wa Jamhuri ya Kenya Uhuru Kenyatta alimkabidhi Rais mstaafu wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete nafasi ya Uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mkutano wa 16 wa Wakuu wa Jumuiya hiyo Jijini Nairobi Kenya. 

Kutokana na hali ya mgogoro wa kisiasa katika nchi ya Burundi, ambayo ilipaswa kukabidhiwa nafasi ya Uenyekiti wa Jumuiya mwaka 2016, Wakuu wa  Jumuiya hiyo waliamua kwa kauli moja kuwa Tanzania kupitia Rais Dkt. Rais John Pombe Magufuli kuendelea na nafasi hiyo. 

Katika Mkutano wa 18 wa kawaida wa Wakuu wa Jumuiya hiyo uliofanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 20 Mei,2017,  Rais Magufuli alisema katika kipindi cha  Uongozi wa Tanzania katika Jumuiya hiyo  mafanikio mbalimbali yalipatikana ikiwemo utekelezaji wa ajenda ya utengamano katika eneo la ushuru wa forodha linaloshuguhulikia vikwazo vya biashara visivyo na kodi. 

Anasema katika ushirikiano wa kifedha Tanzania imewezesha kuandwa miswada ya uanzishwaji wa taasisi ya fedha ya Jumuiya itakayokuwa Taasisi ya mpito kabla ya kuanzishwa kwa Benki kuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Aidha, Rais Magufuli alisema mafanikio mengine ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ikiwemo mradi wa ujenzi wa barabara ya Arusha - Holili - Taveta hadi Voi, na kukamilika kwa upembuzi wa mradi wa barabara ya Malindi- Lungalunga- Tanga – Bagamoyo. 
Aidha Rais Magufuli alisema pia barabara za Lusahunga- Lusumo- Kigali na Nyakanazi- Kasulu- Rumonge –Bujumbura ziko kwenye hatua mbalimbali za usanifu, ikiwa ni sambamba na ujenzi wa vituo vya ukaguzi mipakani, ambapo vituo 9 kati ya 15 tayari vimeanza kufanya kazi.   

Katika masuala ya amani na usalama, Rais Magufuli alisema  kuwa zimefanyika jitihada mbalimbali zinazosaidia kupunguza uhasama miongoni mwa pande zinazokinzana hususani katika  nchi za Burundi na Sudani ya Kusini. 

“Nitoe pongezi za dhati kwa msuluhishi wa mgogoro wa Burundi, Rais Yoweri Museveni pamoja na mpatanishi wa mgogoro huo Rais Mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa wamefanya kazi kubwa sana,” alisema Rais  Magufuli. 

Rais Magufuli alizitaka pande zinazokinzana katika nchi zenye migogoro katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kutanguliza maslahi ya mataifa yao mbele na kuweka nyuma maslahi binafsi kwa maendeleo ya nchi zao. 
Katika kipindi cha miaka miwili ambacho Tanzania imekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, utawala bora na demokrasia umeimarika kwa ambapo mwaka huu nchi za Kenya na Rwanda zinatarajia kufanya  Uchaguzi Mkuu. 

Aidha katika kipindi hicho pia Jumuiya hiyo imeweza kukuza uhusiano na ushirikiano  na mashirika makubwa ya Kimataif ikiwemo Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika ambapo Jumuiya imeweza kusaini  mkataba wa fedha wenye thamani ya Dola milioni 300. 

“Tumeweza kupunguza matumizi ndani ya sekretarieti kutoka dola milioni 12.6 zilizotumika kipindi kilichopita hadi kufikia dola milioni 9.1 nampongeza  sana Katibu Mkuu WA Jumuiya kwa kubana matumizi hayo” anasema Rais Magufuli 

Kwa upande wake Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni  ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, amebainisha kuwa ustawi wa maendeleo ya wananchi , undugu na ulinzi ni masuala kadhaa ambayo hayana budi kupewa kipaumbele ili ili kuimarisha uhusiano wa nchi za Jumuiya hiyo. 

“Tunapozungumza  kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki, tunazungumzia juu ya ustawi wa maendeleo yetu, familia yetu, nchi zetu na hata soko letu, hivyo yatupasa kuzidisha utangamano kwa maendeleo ya Jumuiya,” anasema Rais Museveni. 

Mkutano huo ulijadili ajenda mbali mbali zikiwemo za namna ya kuwezesha uundaji wa magari katika  Jumuiya ya Afrika Mashariki ili  kupunguza uagizaji wa magari yaliyotumika kutoka nje ya Jumuiya.

Ajenda nyingine ni pamoja na kuzuia ama kuondoa uingizaji wa nguo na viatu vya mitumba katika nchi wanachama kutoka nje. Aidha Viongozi hao pia walijadili namna endelevu ya uchangiaji wa bajeti ya Jumuiya hiyo kwa nchi wanachama. 
  
Akizungumzia suala la Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) ambao haukuweza kusainiwa na Tanzania wakati ikiwa mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Rais Museveni alisemaViongozi wa Jumuiya hiyo walibaini kasoro kadhaa ambazo zingeweza kuleta madhara katika sekta za viwanda za nchi hizo. 

Aliongeza kuwa yeye binafsi ataongoza ujumbe wa wa wataalamu kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki watakaokwenda  yaliko makao makuu ya EU ili kujadili kwa kina juu ya EPA na kufikia ufumbuzi. 

Aidha,Jumuiya ya Afrika Mashariki ni Taasisi ya Kiserikali (inter-Governmental Organization), iliyoanzishwa na nchi za Tanzania, Kenya na Uganda. Mkataba ulianzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki ulisainiwa tarehe 30 Novemba, 1999 na ulianza kutumika rasmi mnamo tarehe 7 julai 2000. 

Nchi za Rwanda na Burundi zilijiunga katika Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 2007. Jumuiya ya awali ya Afrika ya Mashariki iliundwa mwaka 1967 na kuvunjika mwaka 1977 kulitokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kisiasa, kijamii na kiuchumi. 

Ibara ya 5(1) ya Mkataba wa kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki imeainisha madhumuni ya kuanzisha Jumuiya kuwa ni kupanua na kuimarisha ushirikiano baina ya nchi wanachama katika nyanja za kisiasa,  kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, ulinzi na usalama, sheria na mahakama kwa manufaa ya wananchi wa nchi wananchama. 

Katika kufikia lengo hilo kuu, Ibara ya 5(1) ya Mkataba wa kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki imeainisha uendeshaji wa mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utafanyika hatua kwa hatua. Hatua hizo zikiwa ni Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja, Umoja wa Fedha na Shirikisho la Kisiasa. 

No comments: